Na AZIZA MASOUD – DAR ES SALAAM
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeteua wagombea watatu watakaosimama kupeperesha bendera ya chama hicho katika chaguzi ndogo zitakazofanyika katika majimbo ya Ukonga jijini Dar es Salaam, Monduli Arusha na Korogwe Vijijini, mkoani Tanga, Septemba 16, mwaka huu.
Wagombea hao, ambao wameteuliwa kupitia Kikao Maalumu cha Kamati Kuu ya Chadema iliyoketi kwa siku mbili (Agosti 15-16) jijini Dar es Salaam, ni
Asia Msangi atakayegombea katika Jimbo la Ukonga, Amina Saguti Jimbo la Korogwe na Yonas Laiser atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika Jimbo la Monduli.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene, ilieleza kuwa, wagombea hao waliteuliwa baada ya kupokea na kujadiliwa kwa taarifa kuhusu chaguzi za marudio za ubunge na udiwani pamoja na hali ya kisiasa nchini.
“Kamati Kuu ya Chama imefanya uteuzi huo wa wagombea ubunge kwa mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa Katiba ya Chama ya mwaka 2006, toleo la mwaka 2016, ibara ya 7.7.16(q),”alisema Makene.
Alisema kulingana na ratiba iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), kampeni za chaguzi hizo ndogo zinatarajiwa kuanza Agosti 24 hadi Septemba 15 mwaka huu.
Uteuzi wa wagombea wa Chadema umefanyika siku tatu baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutangaza wagombea wake kupitia Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama hicho chini ya Mwenyekiti wake, Dk. John Magufuli, kilichoketi Agosti 14 jijini Dar es Salaam.
Wagombea walioteuliwa na CCM, ambao wote walijiengua Chadema hivi karibuni wakiwa katika nafasi hizo hizo za ubunge isipokuwa Timotheo Mzava ambaye atagombea Jimbo la Korogwe Vijijini ni Julius Kalanga ambaye atagombea katika Jimbo la Monduli na Mwita Waitara Jimbo la Ukonga.
Pamoja na vyama hivyo vikuu vya siasa nchini kutangaza wagombea wao, vyama vingine kama Chama cha Wananchi (CUF) na ACT-Wazalendo bado havijatangaza wagombea wao.
Chaguzi hizo za marudio zinafanyika kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kifo katika Jimbo la Korogwe Vijijini baada ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Steven Ngonyani, maarufu kama Profesa Maji Marefu, kufariki dunia Julai 2, mwaka huu.
Katika Jimbo la Ukonga uchaguzi unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema, Waitara kujivua uanachama wa chama hicho na kuhamia CCM Julai 29, mwaka huu.
Jimbo la Monduli nalo linafanya uchaguzi baada ya mbunge wake, Kalanga aliyekuwa Chadema kujivua uanachama wa chama hicho na kuhamia CCM Julai 31 usiku na kupoteza sifa ya kuwa mbunge.