27.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 30, 2022

‘IGP SIRRO AINGIZWA MKENGE’

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM


WAANDISHI wa habari walioshuhudia askari waliomshambulia, Mwandishi wa Kituo cha Redio Wapo, Silas Mbise, wameibuka na kupinga kauli ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, wakidai kuwa amepotoshwa.

Kauli za waandishi hao zimekuja siku moja baada ya IGP Sirro kuzungumzia suala hilo mbele ya vyombo vya habari  huko mkoani Arusha na kudai kwamba Mbise alimkaba askari na alikuwa mbishi kutii agizo la askari wa jeshi hilo.

Wakizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa nyakati tofauti waandishi hao waliokuwa eneo la tukio siku hiyo  walisema Mbise hakumkaba askari yeyote bali yeye ndiye alikabwa na askari.

Akielezea tukio hilo mmoja wa waandishi waliokuwepo  katika eneo hilo (jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kiusalama), alisema kilichotokea ni baada ya waandishi kukataliwa kuingia katika eneo ambalo kwa kawaida hufanya mahojiano na makocha baada ya mechi, jambo lililoibua ubishani.

“Katika ubishani huo alitokea askari aliyekuwa amevaa kiraia, alimpiga kibao mwandishi mmoja wa gazeti la Champion na kisha akaanza kusukuma waandishi na kutuambia hamtaingia kwenye eneo hilo.

“Mbise akamwambia sisi ni waandishi na tuna vitambulisho hivyo tuna haki ya kuingia, unafanya hivyo kwa sababu ya cheo chako? Tumia taaluma yako, nadhani kauli hiyo ndiyo iliyomkasirisha yule askari akaanza kumkaba Mbise.”

Alisema wakati askari huyo anamkaba Mbise ghafla wakaongezeka wengine na katika harakati za kujikwamua kukabwa, akajivua shati.

“Alikuwa amevaa kama pull over fulani hivi, sasa kuna askari mmoja akawa anasema ananipiga ananipiga na yule askari aliyevaa kiraia akaondoka.

“Kwa hiyo wakamchukua Mbise na kumwingiza ndani ambako waliendelea kumshambulia kwa mateke mbavuni, kichwani pasipo kujitetea kwa lolote, kiukweli hakumkaba askari bali alivua shati katika kujidefend,” alisema mwandishi huyo.

Mwandishi mwingine  alianza kuelezea tukio hilo akisema:

“Lilitokea wakati tunashuka chini kwenda kufanya mahojiano na makocha na wachezaji wa timu zilizocheza, ili  kuruhusiwa kuingia ndani kuna vitambulisho maalumu tumepewa na TFF.

“Unapofika kwenye mlango wakuingilia kwa sababu wanakuwepo askari wanaolinda usalama, ni lazima kuonyesha kitambulisho ndipo wanakuruhusu, lakini siku hiyo ilikuwa ni tofauti kwani licha ya kuonyesha kitambulisho tulizuiwa,” alieleza shuhuda huyo.

Alisema kitendo hicho kilimfanya kila mwandishi kuhoji lakini askari aliyekuwepo mlangoni wa Suma JKT, alijibu msimamizi ambaye ni askari ndiye aliyemwambia waandishi wasipite eneo hilo, tusubiri hadi afike.

“Tukawa tunasubiri msimamizi afike ambaye alikwenda kuitwa, lakini alivyofika alianza kusema: ‘Sasa nyie mnataka kuingia ndani kufanya nini?  Kauli hiyo iliwafanya waandishi waanze kujitetea na kutaka kufunguliwa mlango lakini msimamizi huyo alikaa katikati kuzuia huku akisema.

“Hakuna mtu yeyote wa kupita hapa, tena mwondoke ninaweza kupiga mtu au kama kuna anayetaka kupigana na mimi aje,” alizungumza hayo huku akisukuma baadhi ya waandishi waliokuwa mbele kwa kutumia mikono yake, hali iliyozua tafrani,” alisema shuhuda huyo.

Alisema askari huyo aliona kuwasukuma haikutosha hivyo akamwambia askari aliyekuwa naye, amshikie vitu vyake ili atumie mikono yake kuwapiga waandishi  kwa sababu hawataki kuondoka.

“Aliporusha kibao cha kwanza kilimpata mwandishi wa kituo cha Redio cha Wapo, Silas Mbise, lakini mwandishi huyo wakati anajitetea kwanini apigwe, ndipo wakaja askari wengine wakamchangia kumpiga na kumwingiza ndani na kuendelea kumpiga huku wakiwa wamemvua shati.”

Alisema baada ya muda wakamchukua na kumpeleka kwenye gari lao ili waende naye kituo cha polisi, lakini Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, aliona tukio hilo na kuhoji kilichokuwa kinaendelea na kuwataka askari hao kumwachia.

Mwandishi mwingine ambaye alishuhudia tukio hilo naye alishangaa kauli iliyotolewa na IGP Sirro na kusema kwamba Mbise ndiye aliyekabwa kwa kukunjwa shati alilokuwa amevaa.

“Akiwa amekunjwa shati na askari kiasi cha kuonyesha kuwa lilikuwa linamuumiza ndipo akajivua na ndio shati wakabaki nalo wale askari,” alisema.

Baadhi ya waandishi wa habari wanaomfahamu Mbise wanasema kwa hulka kijana huyo ni mpole na mnyenyekevu vitu vilivyochangiwa zaidi na imani yake ya kuokoka.

“Ukimwona Mbise utashangaa na haya polisi wanayoeleza, ni mtaratibu mno, ni mtu ambaye hata kupigana hawezi kusema kweli, ni mlokole mno,” alisema  mwandishi mmoja anayefahamu Mbise.

SIRRO ATENGWE, ASULUBIWE

Wakati huo huo Mbunge wa Jimbo la Ubungo ambaye pia ni mwanahabari,  Saed Kubenea, ameandika andiko akishauri waandishi wa habari kote nchini wasusie kuandika habari zinazohusu Jeshi la Polisi.

Katika andiko lake hilo, Kubenea alisema kauli ya IGP Sirro, kuwa mwandishi wa habari, Silas Mbise, aliyepigwa na askari polisi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, alishambuliwa kwa kuwa aliingia kwenye eneo ambalo haliruhusiwi, haikubaliki na imelenga kutetea uhalifu nchini.

“Hii ni kwa sababu, ndani ya Uwanja wa Taifa hakuna mahali kokote ambako kumepigwa marufuku waandishi wa habari kufika,” alisema.

Alisema mwandishi aliyepigwa alikuwa yuko kazini kama ambavyo polisi walikuwa wakifanya kazi zao kitendo cha kumshambulia, au kumzuia kufanya kazi zake, ni uvunjifu wa Katiba.

Alisema hatua ya Sirro kutetea kitendo cha askari wake kupiga mwandishi, kinapaswa kujibiwa mara moja na waandishi na wahariri kwa kuchukua hatua ya kutotangaza, kutochapisha, kusambaza na kupiga picha, habari zote zinazomhusu Sirro na jeshi lake kwa ujumla.

“Kwani hiyo ndiyo silaha pekee ya waandishi ambayo tumekuwa tukiitumia kwa watu wenye kibri na jeuri kama hii ya Sirro kwa miaka nenda rudi,” aliandika Kubenea.

Tukio la Mbise kushambuliwa lilijulikana zaidi baada ya kusambaa video fupi inayoonyesha askari wa Jeshi la Polisi wakimshambulia kwa mateke na ngumi.

Tukio la kushambuliwa kwake huko lilitokea Agosti 8, wakati wa mchezo wa kirafiki baina ya timu ya Simba na Asante Kotoko ya Ghana walipokuwa wakiadhimisha siku ya Simba (Simba Day).

Kilichozua taharuki zaidi na hasa kwenye tasnia ya habari ni kwamba, tukio hilo lilitokea katika wiki ambayo mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima, Sitta Tuma, naye akumbane na kipigo cha polisi akiwa anatekeleza majukumu yake huko Tarime na kisha kumpa tuhuma za kufanya maandamano yasiyo na kibali.

Video inayoonyesha tukio la Mbise kushambuliwa akiwa hana shati, amelazwa chini kwenye korido ya  kuelekea vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji, ilizua mjadala mkubwa katika makundi mbalimbali ya mitandao ya kijamii ya wanataaluma ya habari na wale wa masuala ya haki za binadamu.

Video hiyo inamwonyesha mwandishi huyo akishambuliwa na askari wanne waliokuwa na silaha za moto na virungu ambao walikuwa wakimpiga kwa vibao na mateke kwenye mbavu na kichwani.

Mbise mwenyewe aelezea tukio hilo

Kwa maneno yake mwenyewe, Mbise alisema akiwa na waandishi wengine wa vyombo mbalimbali vya habari walikuwa wanaelekea kwenye chumba cha mkutano, walipofika katika mlango wa kuingilia katika chumba hicho wakakuta umefungwa.

“Mlango ulikuwa umefungwa na kulikuwa na askari mwanamke akatuambia saa hizi hamruhusiwi kuingia, tukawa tumesubiri, wakati tunaendelea kusubiri kuna askari wengine walikuwa wanapita lakini  askari mmoja alitokea nyuma yetu  alikuwa amevaa kiraia alituhoji tunasubiri nini wakati waandishi wanamjibu ghafla akatusukuma, kuna dada mmoja mwandishi akaniangukia,” alisema Mbise.

Alisema baada ya tukio hilo yeye pamoja na waandishi walimuuliza askari huyo sababu za kuwasukuma ndipo aliposimama mlangoni na kusisitiza kuwa hatutaingia ukumbini.

“Nikamwambia tumia taaluma yako, kuna mmoja aliyekuwa amevaa kiaskari akaja akanikwida kwenye ile kripu ndiye anayeonekana ananipiga kwa teke kichwani.

“Hapo ndio akaanza kunipiga,  akanikunja katika kunikunja nikainama  chini kwa sababu alikuwa ananipiga ngumi, kuinama sasa lile fulana akawa ameivuta akabaki nayo mkononi pamoja na kitambulisho …wakanipiga kama ulivyoona wameniingiza ndani na ile ilikuwa ni sehemu tu wakanichukua na wakati wananipeleka kwenye karandinga lao waliendelea kunipiga,” alisimulia Mbise.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,327FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles