28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MO DEWJ AUNDIWA JOPO LA VIGOGO WATANO

NA ZAINAB IDDY

UONGOZI wa Simba umetangaza kamati maalumu ambayo imepewa jukumu la kutafuta mwekezaji atakayenunua asilimia 50 ya hisa ili kukamilisha azma ya klabu hiyo kujiendesha kisasa.

Hatua hiyo inatokana na klabu hiyo kubadili mfumo wake wa uendeshaji kutoka ule wa wanachama uliodumu kwa miaka mingi hadi kuwa wa hisa.

Kamati hiyo inaundwa na watu watano ambao ni Wakili Damas Ndumbaro, Mbunge wa Ilala, Musa Hassani ‘Zungu’.

Pia yumo Abdallah Lazak Badru, Yusuph Majib na  Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jaji  Thomas Mihayo.

Mfanyabiashara maarufu na mwanachama wa klabu hiyo, Mohamed Dewji, anapewa nafasi kubwa ya kupewa fursa hiyo, baada ya kuweka wazi kuwa yuko tayari kununua hisa zenye thamani ya Sh bilioni 20.

Wanachama wengi wa Simba wanamuunga mkono bilionea huyo kukabidhiwa timu yao kutokana na mchango wake uliowezesha kusajiliwa kwa  wachezaji kadhaa wapya wenye ubora msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akiwemo aliyekuwa kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima.

Akizungumza wakati akitangaza kamati hiyo Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Simba, Dk. Arnold Kashembe, alisema kamati hiyo itafanya kazi yake katika kipindi cha siku 45 kabla ya kuwasilisha jina la mshindi katika kamati ya utendaji.

“Tumeunda kamati hiyo ambayo itakuwa huru kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria za nchi na baada ya kuona wote hao ni wazuri katika masuala ya kisheria pamoja na kifedha kwa maana ya uuzaji na ununuzi wa hisa.

“Kamati hiyo inatarajia kukutana kwa mara ya kwanza kati ya Jumatano na Alhamis, baada ya hapo wataweka mikakati yao juu ya vipi wataanza majukumu yao ya kumpata mwekezaji mkubwa, lengo likiwa ni kuifanya timu yetu iendeshwe kisasa zaidi,” alisema.

“Baada ya kamati hiyo kumpata mwekezaji kwa asilimia 50, itapeleka jina lake kwenye kamati ya utendaji kabla ya kuitishwa mkutano wa wanachama ambao ndio utakaoidhinisha iwapo kama apewe hisa hizo au la.

“Kama wanachama watapitisha jina la mwekezaji huyo aliyepatikana, hapo ndipo mfumo rasmi wa uendeshaji wa klabu utakapoanza, kati ya asilimia 50 zitakazobaki zitatolewa asilimia 10 na kupewa wanachama wote hai, huku zile asilimia 40 zitauzwa kwa wanachama kulingana na uwezo wa mhusika, lakini yule mwekezaji mkubwa kwenye hisa hataruhusiwa kuja kuchukua katika zile 40% za wanachama,” alisema Kashembe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles