31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TAMBWE, CHIRWA WAYEYUKA NJOMBE

  • Beki Mkongo atua mazoezini

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

MATARAJIO ya benchi la ufundi la Yanga kuwatumia washambuliaji wao wa kimataifa, Amis Tambwe na Obrey Chirwa kwenye mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Njombe Mji hayapo tena baada ya daktari wa timu hiyo, Edward Bavu, kuthibitisha bado hawako fiti.

Tambwe na Chirwa wamekuwa nje ya uwanja kwa majuma kadhaa kutokana na kusumbuliwa na majeraha waliyoyapata  wakiwa na kikosi cha Yanga kilichopiga kambi kujiandaa na pambano la Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.

Majeraha hayo yaliwalazimisha wachezaji hao kukosa mechi ya Ngao ya Jamii pamoja na ile ya ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Lipuli ya Iringa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mbali ya kuwa nje ya dimba kutokana na majeraha, Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilimsimamisha kucheza soka Chirwa pamoja na waliokuwa wachezaji wa Yanga, Simon Msuva na Deus Kaseke baada ya kudaiwa   kufanya vurugu na kumsukuma mwamuzi Charles Ludovic wakati wa  mechi ya mwisho ya Ligi Kuu msimu uliopita dhidi ya Mbao FC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kirumba, Mwanza.

Hata hivyo, badaye kamati hiyo iliwaachia  huru Chirwa na Kaseke, huku ikimkuta na hatia na kumwandikia barua ya onyo Msuva ambaye sasa anaichezea Difaa Al Jadida ya Morocco.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Bavu alisema wachezaji hao watakosa mchezo dhidi ya Njombe Mji kutokana na  kutoimarika kwa afya zao.

“Chirwa na Tambwe bado wataendelea kuwa nje kwa muda kutokana na hali zao kutokuwa fiti, hivyo wataendelea kukosekana katika michezo iliyopo mbele ukiwemo na Njombe Mji,” alisema.

Kuhusu winga Baruani Akilimali ambaye pia alikuwa majeruhi, alisema ameanza mazoezi mepesi huku akitarajiwa kuwepo kwenye mchezo dhidi ya Njombe Mji.

“Akilimali ameanza mazoezi mepesi leo (jana) kwa sababu hali yake imeonekana kuwa fiti, hivyo anaweza akacheza mechi inayofuata,” alisema.

Tayari pengo la Tambwe na Chirwa limeonekana kuisumbua Yanga kwani timu hiyo haijafanikiwa kupata ushindi katika mechi zake mbili ilizocheza bila wachezaji hao.

Mechi hizo ni ile ya Ngao ya Jamii ambayo Yanga ilichapwa penalti 5-4 na Simba na Lipuli ilipolazimishwa sare  ya bao 1-1.

Wakati huo huo, Yanga imemshusha nchini Fiston Kayembe kwaajili ya kufanya majaribio katika timu hiyo kabla ya kumsajili wakati wa usajili wa dirisha dogo.

Beki huyo anayeichezea SM Sanga ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), aliwasili nchini juzi ambapo jana alihudhuria mazoezi ya Yanga kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kama  atafuzu majaribio yake, beki huyo atachukua nafasi ya Vincent Bossou aliyemaliza mkataba wake na klabu hiyo baada ya ligi kuu msimu uliopita kumalizika, kisha kugoma kuongeza mwingine kutokana na kutoridhishwa na dau la usajili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles