*Dk. Nchimbi, Sitta wachukua fomu na kurudisha
NA PATRICIA KIMELEMETA, DAR ES SALAAM
VITA ya kuwania uspika wa Bunge la 11, imeanza kupamba moto ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku vigogo kadhaa wa chama hicho wakichukua fomu za kuwania nafasi hiyo.
MTANZANIA ambayo ilikuwa imepiga kambi katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam ilishuhudia makada hao wakikabidhiwa fomu na Katibu wa NEC, anayeshughulikia Oganaizesheni, Dk. Mohamed Seif Khatib jana mchana.
Waliojitokeza kwa siku ya jana ni pamoja na Spika wa Bunge la tisa, Samuel Sitta, aliyekuwa mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes, Leonce Mulenda, Dk. George Nangale na Profesa Costa Mahalu.
Wengine ni aliyekuwa mgombea urais wa CCM, Muzamil Kalokola ambaye alishindwa kurejesha fomu wakati wa mchakato wa ndani ya CCM na kudai msafara wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete ndiyo ulimchelewesha.
Mbali na hao, wengine waliochukua fomu ni Banda Sonoko, Simon Rubugu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (CC), Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye pamoja na Sitta walizijaza na kuzirudisha jana hiyo hiyo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Umma, Itikadi na Uenezi ilieleza kuwa mchakato huo umetoa muda tofauti kwa makada wa CCM ambapo wale ambao si wabunge, wametakiwa kuchukua fomu kuanzia jana saa sita mchana na kuzirejesha leo kabla ya saa 12 jioni.
“Kwa wana-CCM ambao ni wabunge wateule wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaoomba kuteuliwa kugombea uspika na unaibu Spika wa Bunge hilo, wanatakiwa kuchukua fomu kuanzia Novemba 11, mwaka huu (jana), saa sita mchana na kuzirejesha Novemba 14, mwaka huu kabla ya saa 12 jioni,” ilieleza taarifa hiyo ya CCM.
Katika mnyukano huo, vigogo kadhaa wamekuwa wakitajwa kuwania nafasi hiyo huku upinzani mkali ukitarajiwa kuwa kwa Spika anayemaliza muda wake, Anne Makinda, Sitta, Job Ndugai, Mussa Azzan Zungu na Dk. Nchimbi.
Sitta atamba
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Sitta, alisema ameamua kuwania nafasi hiyo kwa kuwa anajiona ana sifa ya kuliongoza Bunge la 11.
Alisema pamoja na hali hiyo, ana uzoefu alioupata wakati akiongoza Bunge la tisa lililojulikana kama ‘Bunge la Kasi na Viwango’ pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba.
Sitta ambaye pia alikuwa Waziri wa Uchukuzi katika Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, alisema amejipima na kuona anafaa na ndiyo maana amechukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.
“Bunge la kipindi hiki lina changamoto nyingi wakati wa kuliongoza, hivyo basi lazima kuwe na Spika makini ambaye ataweza kushirikiana na wabunge ili kuhakikisha hoja za msingi zinazotolewa zinafanyiwa kazi na Serikali, jambo ambalo linaweza kusaidia wananchi kurudisha imani.
“Ninaamini ninaweza, nitaliongoza kwa misingi ya demokrasia, hasa katika kipindi hiki cha mfumo wa vyama vingi,” alisema Sitta.
Alisema katika kipindi hiki zimejitokeza siasa za ukanda ambazo zimesababisha wananchi kupiga kura za ukanda, ukabila na udini, hivyo anatakiwa awepo Spika wa Bunge atakayeweza kuwarudisha wananchi kuwa kwenye kundi moja la Utanzania ili waweze kulijenga taifa.
Sitta alisema kitaaluma yeye ni mwanasheria mwenye namba 687 wa Mahakama Kuu, hivyo basi ataweza kutumia taaluma yake pale ambapo anaona kuna hoja zenye mgogoro wa kisheria ili aweze kupata ufumbuzi.
Wakati wa mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba, Aprili mwaka jana chini ya Sitta, vyama vya upinzani vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, viliasisi Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kuahidi kusimamia katiba ya wananchi iliyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba.
Kutokana na hali ya mambo ndani ya Bunge hilo, wajumbe wa vyama hivyo walilazimika kususia Bunge hilo na kutoka nje na kuwaacha wajumbe wengi wa upande mmoja kutoka CCM.
Pamoja na hali hiyo, Sitta, alisisitiza kuwa Bunge hilo halitaahirisha shughuli zake hadi hapo muda wa siku 60 uliokuwa umepangwa utakapokamilika.
DK. NCHIMBI
Akizungumza jana, Dk. Nchimbi alisema kuwa ameamua kuwania nafasi hiyo baada ya kujiona ana vigezo vya kuongoza Bunge hilo.
Alisema lengo la kuchukua fomu hiyo ni kutaka kutatua changamoto za wananchi, hasa wakati wa kupitishwa miswada mbalimbali ambayo imelenga kuleta maendeleo kwa wananchi.
“Nitashirikiana na wabunge ili kuhakikisha tunawatumikia wananchi katika kuleta maendeleo,” alisema Dk. Nchimbi.
Aliongeza kuwa mkakati wake ni kuhakikisha kuwa mijadala inayojadiliwa na wabunge na kupitishwa inalenga kuleta masilahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Alisema kutokana na hali hiyo, anawaomba wabunge kumchagua ili aweze kuwatumikia wananchi kupitia nafasi hiyo.