24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo watwishwa zigo Z’bar

Pg 2*Wamo Dk. Salmin Amour, Mwinyi, Amani Karume

*Zitto amtaka Magufuli atangaze hali ya hatari

*Jumuiya ya Madola yaingilia kati

Na Waandishi Wetu, Zanzibar/Dar

JUHUDI za kusaka suluhu kwa ajili ya kutatua mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar zinaendelea, baada ya vigogo kadhaa wa kitaifa na kimataifa kuongezwa katika timu ya mazungumzo.

Taarifa kutoka visiwani huko zinasema, katika kufanikisha mchakato huo imeundwa kamati maalumu inayowashirikisha marais wote wastaafu wa Zanzibar kwa lengo la kutafuta suluhu ya pamoja.

Katika kamati hiyo wamo, Rais Mstaafu Alhaj Ally Hassan Mwinyi, Dk. Salmin Amour Juma, Amani Abeid Karume na mjumbe maalumu kutoka Jumuiya ya Madola (Commonwealth), Rais Mstaafu wa Nigeria, Goodluck Jonathan.

Jopo la vigogo hao limekuja kuongeza nguvu ya kutafuta suluhu, baada ya wagombea urais wawili wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein (CCM) na Maalim Seif Sharif Hamad (CUF) kunukuliwa kwamba wameanzisha mazungumzo hayo juzi.

Mtanziko huo wa kisiasa wa Zanzibar umekuja, baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kutangaza kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25.

Kutokana na hali hiyo MTANZANIA ilimtafuta Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, ambaye alisema kuwa hatua ya kuundwa kwa kamati hiyo ni kutafuta mwafaka ili kulinda amani ya Zanzibar.

“Kamati hii imeundwa kwa kuwashirikisha marais wote wastaafu wa Zanzibar kwa lengo la kutafuta suluhu ya pamoja,” alisema kwa kifupi Jussa.

Zanzibar imewahi kuongozwa na marais saba hadi sasa huku rais wa kwanza akiwa ni marehemu Sheikh Abeid Aman Karume, Abood Jumbe, Ali Hassan Mwinyi, Idrisa Abdulwakil, Salmin Amour Juma, Aman Abeid Karume na rais wa sasa Dk. Ali Mohamed Shein.

Uchaguzi wafutwa rasmi

Taarifa kutoka Zanzibar zinaeleza kuwa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa tamko la kisheria la kufuta uchaguzi huo.

Tamko hilo linaonekana kutilia nguvu tamko la kufutwa kwa Uchaguzi huo lililotolewa na Jecha ni la Novemba 6, mwaka huu lenye namba CXXIV 6587.

Goodluck Jonathan atishwa mzigo

Nchi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth) zimemteua Rais mstaafu wa Nigeria, Goodluck Jonathan na kumpa  jukumu jipya la kutafuta ufumbuzi wa mkwamo huo wa kisiasa katika visiwa vya Zanzibar.

Kabla ya uteuzi huo, Jonathan aliongoza Jopo la Uangalizi la Jumuiya ya Madola (COG) katika Uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu.

Jumuiya ya Madola inaundwa na nchi 53 zilizowahi kutawaliwa na Uingereza, Tanzania ikiwamo kama nchi mwanachama.

Taarifa ya jumuiya hiyo iliyotolewa ilieleza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, ambao ulishuhudia Dk. John Magufuli akiwa Rais wa Tanzania wa awamu ya tano, huku timu hiyo ya uangalizi ikiridhia uchaguzi huo wa Jamhuri ya Muungano, kwamba ni halali.

“Jumuiya ya Madola ambayo ina historia ya kusuluhisha migogoro katika kisiwa hicho, imeashaanza juhudi za kimataifa za kuutatua mgogoro huu wa sasa kwa kumteua Jonathan kama mwakilishi wake maalumu,” ilieleza taarifa hiyo iliyotumwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Kamalesh Sharma.

ZITTO NA MAGUFULI

Naye Kiongozi wa  Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amemshauri Rais Dk. John Magufuli kuingilia kati mgogoro huo na kutangaza hali ya hatari visiwani humo.

Zitto ambaye ni Mbunge mteule wa Jimbo la Kigoma Mjini, alitoa  ushauri huo jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

“Njia bora anayotakiwa kutumia Dk. Magufuli baada ya kutangaza hali ya hatari, ni kuunda serikali ya mpito na baadaye kufanya marekebisho ya Katiba itakayowezesha kufanyika kwa uchaguzi mwingine.

“Katiba na sheria zinaonesha wazi kwamba, kwa sasa Zanzibar haina rais wala serikali, hivyo yeyote anayejipa mamlaka hayo ni sawa na mtu aliyefanya mapinduzi na huo ni uhaini,” alisema Zitto.

Pamoja na kumsifia Dk. Magufuli kwa mwanzo mzuri wa kufanya ziara za kushtukiza Wizara ya Fedha na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), lakini ameshtushwa na kutozungumzia mvutano huo tangu kuapishwa kwake.

“Tunampongeza Rais Dk. Magufuli kwa hatua alizoanza kuchukua, hatuwezi kumfurahia kwa kutembelea Wizara ya Fedha na Hospitali ya Muhimbili, huku akiacha nchi ya wenzetu wa Zanzibar ikiwa si shwari,” alisema Zitto.

Alisema kuna dalili za pande mbili za Chama Cha Wananchi (CUF) na CCM kuvutana kuhusu matokeo ya uchaguzi uliofutwa, hivyo ni vyema Rais Magufuli akaingilia kati kwa sababu Katiba inampa mamlaka hayo.

“Tatizo la Zanzibar si la kikatiba, bali limetokana na utashi wa kisiasa na ndiyo sababu ya upande wa CCM kujikuta umekubali kurudiwa uchaguzi, huku CUF wakigomea uamuzi huo na kushinikiza matokeo ya uchaguzi uliopita yatangazwe.

“Hata hatua ya Mwenyekiti wa ZEC kufuta uchaguzi huo yalifanyika kwa kukiuka Katiba, huku akijua hakuna kifungu cha sheria kinachompatia mamlaka ya kufuta uchaguzi.

“Sheria inasema inapotokea mvutano katika uchaguzi, mwenyekiti analazimika kukutana na Makamu Mwenyekiti wa ZEC na makamishna wake wanne ambao watajadiliana na kama ikibainika kuna sehemu zilikuwa na matatizo wataamua kurudia katika eneo hilo,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa ZEC, eneo lilikuwa na matatizo zaidi ilikuwa ni majimbo ya Pemba hivyo ilitakiwa, mwenyekiti huyo kutangaza kurudia uchaguzi katika maeneo hayo pekee na si kufuta uchaguzi wote.

Akizungumzia kuhusu kuungana na wabunge wa vyama vya upinzani, alisema atashirikiana na wabunge watakaokuwa tayari kutetea maslahi ya wananchi na Taifa kama Ilani ya chama chake inavyoainisha.

Zitto ambaye katika Bunge la 10 alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema atakuwa tayari kufanyakazi katika kamati yoyote ya Bunge atakayoteuliwa na Spika wa Bunge.

Kiongozi huyo alisema chama hicho kimepanga kuifanya Halmashauri ya Kigoma Ujiji kuwa ya mfano, baada ya Chama hicho kupata viti vingi katika halmashauri hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles