Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Mratibu wa Mtandao wa Kutetea Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumo, ameeleza kuwa ukosefu wa sheria na sera za kuwalinda na kuwatambua watetezi wa haki za binadamu umesababisha kuzorota kwa hali ya utetezi na ulinzi wa haki za binadamu nchini.
Akizungumza leo, Desemba 10, 2024, jijini Dar es Salaam wakati wa kuadhimisha miaka 40 ya uwepo wa haki za binadamu na miaka 36 ya utekelezaji wake katika Katiba ya Tanzania, Olengurumo alisema kuwa nchi nyingine barani Afrika kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimepiga hatua katika kuwalinda watetezi wa haki za binadamu.
Olengurumo alibainisha kuwa, tangu THRDC ianze kazi yake miaka 10 iliyopita, kumeripotiwa matukio 513 ya unyanyasaji dhidi ya watetezi wa haki za binadamu. Matukio hayo yanajumuisha kukamatwa kiholela, vitisho vya kifo, kufungwa kwa akaunti za benki na taasisi zao, na kuhojiwa uraia wao.
“Sheria za sasa hazitambui wala kuwalinda watetezi wa haki za binadamu, hali inayofanya wengi wao kuwa waathirika wa unyanyasaji,” alisema Olengurumo.
Alisisitiza umuhimu wa kurekebisha sheria zinazominya uhuru wa vyombo vya habari, akionyesha kuwa hatua hizo zimesababisha waandishi wa habari kushindwa kuripoti matatizo ya wananchi kwa uhuru.
Olengurumo aliongeza kuwa vyuo vikuu, ambavyo awali vilikuwa chemchem ya mijadala ya masuala ya haki za binadamu, utawala bora, na demokrasia, vimepoteza nafasi hiyo.
“Hali ya sasa vyuoni haifurahishi; mijadala ya masuala muhimu inakosa washiriki kutoka ndani ya vyuo, hali inayoonyesha kushuka kwa nafasi ya vyuo katika kuchochea mijadala ya kitaifa,” alibainisha.
Kuhusu mfumo wa mahakama, alisema kuwa licha ya kwamba haki za binadamu hazikuwepo awali katika Katiba, majaji waliweza kujenga sheria na mifumo bora iliyosaidia kulinda haki nchini na hata kutumika kimataifa.
Kwa upande wake, mwandishi na mchambuzi maarufu, Jenerali Ulimwengu, alieleza kuwa sheria zinazopitishwa na Bunge zimekuwa zikikandamiza haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari.
“Bila haki za binadamu, haki nyingine zote haziwezi kupatikana. Serikali inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kukuza haki hizi,” alisema Ulimwengu.
Sheikh Ponda Issa, Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, alieleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la mauaji na vitendo vya kikatili vinavyofanyika nchini, akisema kuwa hali hiyo inahitaji hatua za haraka.
“Tumekuwa tukiona miili ya watu ikitelekezwa barabarani, hali ambayo ni ya kikatili na isiyokubalika. Ni lazima mfumo wa haki za binadamu ufanyiwe mabadiliko makubwa,” alisema Sheikh Ponda.