33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MNYIKA, BULAYA WATIMULIWA BUNGENI

 

Gabriel Mushi, Dodoma

Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson amewafukuza ndani ya Ukumbi wa Bunge wabunge wa Chadema, John Mnyika (Kibamba) na Ester Bulaya (Bunda Mjini) kwa kutoheshimu kiti na kusababisha usumbufu wakati wa kupitisha Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji mwaka 2018/19.

Mnyika alitimuliwa bungeni baada ya kulazimisha kuwasilisha hoja ya kutaka kuzuia mchakato wa kuhitimisha bajeti hiyo.

Mvutano ulijitokeza baada Naibu Spika kumuita Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Juma Aweso kujibu hoja za baadhi ya wabunge waliochangia mjadala wa bajeti ya wizara hiyo.

Kabla ya kuanza kuzungumza, Mnyika alisimama na kuomba kutoa taarifa ambapo Dk. Tulia alimruhusu.

“Naomba kupewa nafasi ya kutoa hoja ambayo inaruhusiwa kutolewa wakati wowote waziri anapohitimisha hoja. Kwa mujibu wa kanuni ya 69, fasili ya kwanza mbunge anayependa kutoa hoja anaweza kuomba hoja iliyopo mezani iahirishwe, pia atataja mjadala uahirishwe hadi wakati gani na kutoa sababu, naomba nipewe nafasi ya kutoa hoja hiyo kwamba bajeti hii iahirishwe,” amsema Mnyika.

Baada ya kumaliza kusema hayo, Dk. Tulia alisema: “umeshamaliza, kaa kwanza. Nikisimama mimi hutakiwi kusimama”.

Aidha, akifafanua taarifa hiyo ya Mnyika, Dk. Tulia alisema licha ya Mnyika kutumia fasili ya kwanza ya kanuni hiyo namba 69, fasili ya pili inampa uhuru kwa Spika kukata hoja iliyotolewa na mbunge kuwa hoja iliyopo mezani iahirishwe.

“Spika anaweza kuamua hivyo iwapo akiona hoja hiyo haina mashiko katika ubora wa uendeshaji wa shughuli za bunge au pia anaweza kusema iamuliwa kwa kupigwa kura,” amesema.

Hata hivyo, wakati Dk. Tulia akiendelea kutoa ufafanuzi, Mnyika alisimama kutaka kuendelea kutoa ufafanuzi wa hoja yake:  “nataka kueleza sababu, nipe nafasi,”.

Dk. Tulia: “Kaa chini, nikiwa nimesimama hutakiwi kusimama. Basi kwa sababu wabunge hamtaki kusikiliza ninachosema, mimi ndiye naendesha kikao hiki, Aweso endelea…”

Naibu spika baada ya kumruhusu Naibu Waziri Aweso, baadhi ya wabunge walipiga kelele na kuondoa utulivu ndani ya Bunge hali iliyomlazimu Dk. Tulia kuwataka wabunge hao kuwa na adabu kwa sababu amesimama kutoa utaratibu lakini hawataki kumsikiliza.

“Wabunge muwe na adabu kwa kitu kidogo, kwa sababu nimesimama niwape utaratibu hamtaki kunielewa. Mnyika naomba utoke nje….” Alisema.

Aidha, baada ya Mnyika kutolewa nje ya ukumbi wa Bunge, Bulaya alionekana kuendelea kuongea hatua iliyomfanya kumfukuza ukumbini hapo kwa kutoheshimu kiti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles