24.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

MNH yatumia mil 500/- kusomesha wataalamu wa figo, masikio

prof-lawrence-museruNa VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imetumia Sh milioni 528 kusomesha wataalamu wa afya 27 watakaotoa huduma ya upandikizaji figo na vifaa vya masikio (cochlea) katika Hospitali ya Apollo nchini India.

Kundi hilo la wataalamu linajumuisha madaktari bingwa wa figo, madaktari wa usingizi, wauguzi wa chumba cha upasuaji na ICU, maabara, tiba ya mionzi, madaktari, wauguzi na wataalamu wa kuongea.

Akizungumza na waandishi wa habari jana hospitalini hapo, Kaimu Mkurugenzi wa MNH, Profesa Lawrence Museru, alisema fedha hizo zinajumuisha gharama za mafunzo, nauli, fedha za kujikimu na gharama nyinginezo.

Alisema MNH itaanza kutoa huduma hizo Januari mwakani ambapo idadi ya wagonjwa wanaosafirishwa nje ya nchi kufuata matibabu hayo itapungua.

“Hadi sasa kuna wagonjwa zaidi ya 120 wanaosafishwa figo kila siku, zaidi ya asilimia 80 wanahitaji huduma ya kupandikizwa figo, mgonjwa akipelekwa nje ya nchi hugharimu kati ya Sh milioni 40 hadi 60.

“Serikali inakusudia pia hospitali za Bugando, Mwanza, KCMC, Dodoma na Mbeya nazo zitoe huduma ya kusafisha figo kwa sababu mahitaji ni makubwa ya upandikizaji,” alisema Museru.

Akizungumzia tatizo la usikivu, alisema ni kubwa na kila mwaka zaidi ya watoto 100 hupatiwa huduma ya kupandikizwa vifaa hivyo.

“Gharama za matibabu hayo nje ya nchi ni kubwa kwani mtoto mmoja hugharimu kati ya Dola 80,000 hadi 90,000, sawa na Sh milioni 80 hadi 100,” alisema.

Aidha, alisema MNH inatarajia kutumia Sh bilioni 3.4 kuongeza vyumba vya upasuaji kutoka 12 hadi 20 na eneo la huduma za uchujaji wa damu kwa wagonjwa wa figo litapanuliwa kwa kuongeza vitanda kutoka 17 vya sasa hadi vitanda 42.

“Tutaongeza pia mtambo wa kuchuja maji (water-treatment plant) na vyumba vya wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu vipya vinne (ICUs),” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles