21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

MNEC Jumaa apigia chapuo maslahi bora kwa walimu

Na Gustafu Haule, Mtanzania Digital

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa(MNEC) kupitia Jumuiya ya Wazazi, Hamoud Jumaa, amesema anatamani kuona Serikali ikiwapa kipaumbele walimu ili wawe watumishi wa kwanza nchini kupata maslahi bora.

Jumaa ametoa kauli hiyo leo Juni 9, wakati akizungumza na walimu wa Shule ya Msingi Msisiri B iliyopo Kinondoni Mkwajuni pamoja na walimu wa Shule ya Msingi Ilala Boma iliyopo Kata ya Ilala pamoja na viongozi mbalimbali wa chama na  jumuiya.

Kauli ya Jumaa imekuja mara baada ya kutembelea mradi wa shule mpya ya Msingi Ilala Boma inayojengwa kwa gharama ya Sh milioni 306 pamoja na shule ya Msingi Msisiri B iliyopo Kinondoni inayojengwa kwa gharama ya Sh milioni 400 fedha ambazo zimetolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Katika mkutano huo, Jumaa amesema kuwa walimu ni watumishi pekee ambao wamekuwa daraja la kuwavusha watu wengine wakati wao kila mwaka wakibaki hapohapo jambo ambalo lazima liangaliwe upya.

Amesema,kuwa watumishi wote wanaofanyakazi katika taasisi za Serikali pamoja na zile binafsi wanapitia mikono ya walimu na kwamba ya miaka miwili wanakuwa na maisha mazuri kuliko walimu.

“Natamani kuona walimu wanakuwa watumishi wa Kwanza kupewa kipaumbele na katika hili nitaishauri Serikali kuona namna ya kufanya jambo kwa walimu wetu ili tuwape nguvu ya kufundisha wanafunzi kwa molari ili kutoa vijana bora ambao watalisaidia Taifa letu,”amesema Jumaa.

Aidha,Jumaa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amekuwa msikivu na anafanyakazi kubwa hapa nchini hivyo anaimani hata hili la walimu atalifanyiakazi kwa wakati.

Amesema,katika kipindi cha miaka miwili alichokaa madarakani amefanya mengi mazuri na makubwa kwa Taifa letu na kwamba sekta ya elimu pekee ameiboresha na Sasa inakwenda vizuri.

Jumaa, ameongeza kuwa mpaka sasa tayari zimejengwa Shule 400 kote nchini na madarasa mapya 15000 yamepatikana lakini bado anaendelea kuweka juhudi ili kusudi ifikapo 2023 hawe amefikia malengo ya kuboresha elimu nchini.

Katika hatua nyingine Jumaa ,ameridhishwa na ujenzi wa Shule hiyo huku akipongeza uongozi wa Shule kwa usimamizi mzuri na ametaka wazisimamie fedha hizo vizuri ili kufanya mradi huo ukamilike kwa wakati.

Hatahivyo,amewaomba walimu hao kusimamia kikamilifu maadili ya wanafunzi na wakemee vitendo viovu ambayo sio maadili ya nchi yeti kwani kufanya hivyo itasaidia kuzalisha vijana bora na wasomi wenye maadili ya kusaidia Taifa.

Diwani wa Kata ya Ilala Saady Kimji,amemshukuru Mnec huyo kwa hatua ya kufanya ziara Mkoani Dar es Salaam huku akisema atahakikisha miradi yote ya maendeleo inafanikiwa.

Kimji,amesema Rais Samia ametoa kipaumbele kikubwa katika elimu na Kata ya Ilala ni wanufaika wakubwa hivyo ameahidi kumuunga mkono Rais kwa juhudi anazofanya.

Katibu Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam, Iddy Livanu,amesema Jumuiya ya Wazazi katika Mkoa wake ipo salama na wanafanyakazi kubwa ya kuhakikisha CCM inaendelea kushika dola katika chaguzi zake zijazo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles