25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MNADA MAHEKALU YA LUGUMI WAKWAMA KWA MARA YA TATU

Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

NYUMBA mbili za mfanyabiashara Said Lugumi zimeshindwa kuuzwa, baada ya wateja waliojitokeza kutofikia bei elekezi iliyopangwa na Serikali.

Mnada huo uliofanyika kwa mara ya tatu jana, ulihusisha nyumba iliyoko Mbweni JKT, Wilaya ya Kinondoni na nyingine iliyoko Upanga, Wilaya ya Ilala.

Kabla ya kuanza mnada huo, watu waliotaka kununua nyumba hizo walijisajili katika daftari maalumu, kisha kulipa fedha taslimu Sh milioni mbili.

Mnada huo ulianza saa tano asubuhi na kushuhudiwa na watu wachache, huku ulinzi ukiwa umeimarishwa.

Katika nyumba ya kwanza walijitokeza watu watatu waliotaka kuinunua kwa Sh milioni 510, wakati ile iliyoko Upanga, walijitokeza watu wawili waliotaka kuinunua kwa Sh milioni 650.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono, Scholastika Kevela, alisema viwango hivyo havilingani na bei elekezi iliyopangwa na Serikali.

“Shilingi milioni 650 bado iko chini, sisi tumepewa bei elekezi na ni siri kati ya Serikali na dalali, nikiitaja hadharani nitakuwa nimevunja sheria za mnada.

“Endeleeni kuongeza fedha mkifikia bei elekezi tutawauzia nyumba,” alisema.

Hata hivyo, hakuna mteja aliyejitokeza kutaka kuongeza fedha na mnada uliahirishwa hadi wakati mwingine.

“Tutaendelea kurudia mnada hadi watakapopatikana wateja, kwa sababu ni lazima nyumba hizi ziuzwe ili kodi ya Serikali ipatikane,” alisema.

WATEJA

Mmoja wa wateja waliojitokeza kutaka kununua nyumba ya Upanga, Idd Kibula, alisema bado anaitaka nyumba hiyo, hivyo ataendelea kujipanga ili aweze kuinunua.

“Mnada ukirudiwa nitakuja tena kwa sababu bado tunaitaka nyumba hii,” alisema Kibula

SHIKA AINGIA MITINI

Dk. Louis Shika hakutokea katika mnada huo kama ilivyokuwa imetarajiwa na wengi.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika mnada walisikika wakisema kuwa walifika kumuona Dk. Shika.

“Mimi nilijua Dk. Shika ataibuka tena leo (jana) ndiyo maana nimeamua kuja ili nimshuhudie,” alisema dereva bodaboda aliyejitambulisha kwa jina la Nassor Haruni.

MINADA ILIYOPITA

Katika mnada wa kwanza uliofanyika Septemb 9, mwaka huu, Kampuni ya Yono ilifanikiwa kuuza nyumba iliyoko Upanga kwa Sh milioni 700.

Hata hivyo, Serikali haikuridhika na bei hiyo na kuamua kufanya tathmini upya ili iuzwe tena.

Mnada wa pili ulifanyika Novemba 9, mwaka huu na Dk. Shika alifanikiwa kununua nyumba zote kwa gharama ya Sh bilioni 3.2.

Nyumba ya kwanza iliyoko Mbweni kitalu namba 57 yenye ukubwa wa mita za mraba 1,500 iliuzwa kwa Sh bilioni 1.1, iliyofuata kitalu namba 47 yenye ukubwa wa mita za mraba 1,500 iliuzwa kwa Sh milioni 900.

Nyumba ya Upanga, iliyoko kitalu namba 701, yenye ukubwa wa mita za mraba 400, iliuzwa kwa Sh bilioni 1.2.

Hata hivyo, Dk. Shika alishindwa kulipa asilimia 25 ya fedha zote ambazo ni Sh milioni 800, hatua iliyosababisha akamatwe na kuwekwa ndani.

Aliwekwa ndani katika Kituo cha Polisi Salender, kisha kuhamishiwa Kituo cha Polisi Kati, alikokaa kwa siku mbili kisha kuachiwa.

Lugumi anadaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Sh bilioni 14 na Kampuni ya Yono ilipewa kazi ya kuuza mali zake ili kufidia deni hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles