23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

MUHIMBILI YAWEKA HISTORIA KWA KUPANDIKIZA MGONJWA FIGO

NA TUNU NASSOR -DAR ES SALAAM

HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Hospitali ya BLK ya India, kwa mara ya kwanza imeweka historia ya kufanikiwa kupandikiza figo kwa mgonjwa aliyesumbuliwa na maradhi hayo.

Upandikizaji huo uliofanyika Novemba 21, mwaka huu, chini ya jopo la wataalamu kutoka katika hospitali zote mbili, ulifanyika kwa mwanamke mwenye umri wa miaka 30, baada ya kupewa figo na ndugu yake mwenye umri wa miaka 27.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema upasuaji huo mkubwa ni juhudi zinazofanywa na Serikali katika kupunguza rufaa za wagonjwa wanaohitaji kupata huduma hiyo nje ya nchi.

“Upasuaji huu umeokoa fedha ambazo zingelipwa nje ya nchi kugharamia matibabu hayo na badala yake fedha hizo zitumike kuleta maendeleo katika maeneo mengine yenye uhitaji,” alisema Ummy.

Alisema kuanzishwa kwa huduma hii nchini kutaleta nafuu kwa wagonjwa wengi zaidi kupata matibabu na hivyo kuokoa maisha ya wengi.

“Matibabu nje ya nchi ilitugharimu shilingi milioni 80 hadi 100 kwa mgonjwa mmoja na tulikuwa tukipeleka wagonjwa 35 kwa mwaka, hivyo mnaweza kuona kiasi cha fedha ambacho tutakuwa tunakiokoa kwa kufanya upasuaji nchini,” alisema Ummy.

Alisema takriban wagonjwa 400 wa figo wanafanyiwa utakasishaji wa damu (renal dialysis) katika vituo mbalimbali vya tiba hapa nchini na asilimia 60 wanaweza kuhitaji huduma ya kupandikiza figo.

Pia aliwataka wananchi kujiunga katika mifuko ya bima ya afya ili kuweza kupata matibabu kwa urahisi.

“Haya matibabu gharama yake hapa nchini ni shilingi milioni 21 kutoka kumwandaa mgonjwa hadi upasuaji, sasa kama mtu hana bima ya afya itakuwa ngumu kwake kumudu gharama hizi,” alisema Ummy.

Alisema katika bajeti ijayo ya Serikali atahakikisha fedha zinatengwa ili kuendeleza huduma hiyo iwe ya kudumu.

Alisema kutokana na kuongezeka kwa wagonjwa wa figo nchini, Serikali imeanzisha vituo vya utakasishaji wa damu katika hospitali za rufaa na za kanda ili kuwasogezea karibu huduma hiyo kwa wagonjwa wa mikoani.

Pia alisema kupandikiza viungo katika mwili wa binadamu kunahitaji sheria inayoruhusu jambo hilo kufanyika, lakini katika hatua hii walitengeneza kanuni namba 232 zilizochapishwa katika gazeti la Serikali zinazowezesha kufanyika kwa upasuaji huo.

Alisema imeandaa kamati ya watu tisa watakaosimamia na kuhakikisha kuwa hakuna biashara ya viungo inayoingia katika upandikizaji.

“Kwa kushirikiana na jopo la wataalamu tunaandaa muswada wa sheria ambayo sasa itaturuhusu kufanya upandikizaji wa viungo vya binadamu, ikiwa ni pamoja na kumwezesha mtu kubeba mimba kwa niaba ya mwingine,” alisema Ummy.

Naye Mkurugenzi wa MNH, Profesa Lawrence Museru, alisema wamemshauri Ummy kuweka kipengele kinachomruhusu mtu anayetarajiwa kufa kutoa viungo vyake kwa ajili ya matibabu ya wengine.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Hospitali ya BLK, Dk. Hardev Bhatyal, alisema wataendelea kushirikiana na MNH na taasisi nyingine za afya nchini katika kuwajengea uwezo wataalamu wa afya.

“Mkituhitaji tupo muda wowote, tunawakaribisha kwa sababu safari hii ya ushirikiano ndio kwanza imeanza,” alisema Dk. Bhatyal.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles