25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

KAMPENI ZA UDIWANI VURUGU ZATAWALA

  • Zitto naye apata msukosuko Tunduru

Na WAANDISHI WETU

KAMPENI za lala salama katika uchaguzi mdogo wa marudio ya udiwani kwenye kata 43 jana ziliingia dosari, baada ya pande mbili hasimu kisiasa, CCM na Chadema, katika maeneo tofauti, wafuasi wake kurushiana mawe kiasi cha baadhi yao kujeruhiwa vibaya.

Miongoni mwa maeneo ambayo yalikumbwa na kadhia hiyo ni Kata ya Mbweni, iliyopo Jimbo la Kawe, Dar es Salaam, ambako wafuasi wa CCM na Chadema walipigana mawe kiasi cha kuharibu magari na baadhi ya watu kujeruhiwa vibaya.

Shuhuda wa tukio hilo aliliambia MTANZANIA Jumamosi kuwa, vurugu zilizuka saa 10:30 jioni, wakati msafara wa CCM ukielekea katika kampeni za udiwani katika kata hiyo na kupita mahali ambako Chadema walikuwa wakifanyia mkutano wao.

“Msafara wa CCM ulipita karibu na eneo ambalo Chadema walikuwa wakifanyia mkutano wao, katika eneo hilo ndipo kwenye njia ya kwenda ofisi za CCM, sasa msafara ulivyofika hapo watu wa Chadema wakaanza kurusha mawe.

“Baada ya mashambulizi kuzidi ambapo magari mawili yalivunjwa vioo, CCM nao walijibu mashambulizi kwa kurusha mawe kwa upande wa Chadema, ambapo nako kuna vitu vimeharibika na wengine wamejeruhiwa,” alisema shuhuda huyo.

Pia katika katika kampeni hizo za Kata ya Mbweni alikuwamo Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, ambaye hivi karibuni alijiunga na CCM, aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho, Humphrey Polepole.

Kafulila si tu alifika kuongeza nguvu katika kampeni hizo, bali kutambulishwa rasmi kujiunga na CCM, baada ya hivi karibuni kutangaza kuachana na siasa za upinzani kwa kile alichodai kuwa amegundua kwa sasa si jukwaa salama la mapambano dhidi ya vita ya ufisadi.

Kafulila, ambaye alikuwa amevalia shati la bluu bahari na suruali nyeusi, tofauti na baadhi ya viongozi aliokuwa ameambatana nao ambao walikuwa kwenye sare ya rangi ya chama hicho, kijani, alitambulishwa rasmi na Polepole huku akisema yeye ni mkazi wa eneo hilo la Mbweni.

Mbali na Kafulila, ambaye alipewa nafasi ya kuzungumza, Masha naye alifanya hivyo na zaidi alilaani kitendo cha wafuasi wa vyama hivyo kupigana mawe na kusema wahusika wanapaswa kuchukuliwa hatua kali.

“Mimi nimeshakuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, kitendo kama hiki kinapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Masha.

Akizungumzia tukio hilo, Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, alisema watu wasiofahamika  walivamia na kuvunja vifaa vyao vya muziki vilivyopangwa kutumika katika mkutano wa kampeni za udiwani wa Kata ya Mbweni, wilayani Kinondoni.

Jacob, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ubungo(Chadema), alisema wakati watu wakiwa pembeni wakisubiri viongozi na wanachama kufika eneo hilo, ghafla lilitokea gari dogo lililobeba vijana hao ambao walishuka na kufanya uharibifu huo.

“Walivunja muziki wote uliokuwa uwanjani, kisha kuvunja kioo cha gari la matangazo lililokuwa likitumika kuhamasisha watu kuhudhuria mkutano huu,” alisema Jacob.

Alisema hadi sasa bado hawajawatambua   watu hao na kwamba, hali ya utulivu ilirejea katika eneo hilo baada ya polisi kuwasili.

Mbali na kadhia hiyo iliyowakumba akina Kafulila, mwanasiasa mwingine machachari ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe, naye msafara wake ulipopolewa mawe huko Tunduru, mkoani Mbeya.

Habari kutoka Tunduma zinaeleza kuwa, msafara wa Zitto, ambaye ni  Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT – Wazalendo, ulivamiwa na wafuasi wa CCM na kumjeruhi  mmoja wa viongozi wa chama hicho.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana kwa njia ya simu, Msemaji wa chama hicho, Abdalah Khamis, alisema msafara wao ulivamiwa katika Kata ya Lukumbule – Tunduru, wakati wakielekea kwenye ofisi za chama chao.

“Wametuvamia na kumjeruhi vibaya kiongozi wetu mmoja kwa mawe, wamemchakaza sana, ndio tunafuatilia taratibu tuendelee na mikutano,” alisema Abdallah.

Hii si mara ya kwanza kutokea kwa vurugu hizo tangu kipyenga cha kampeni za uchaguzi huo kilipopulizwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Oktoba 27, mwaka huu, ambapo katika maeneo kadhaa kumeshuhudiwa vurugu za hapa na pale, hususan katika mikoa ya Arusha na Dar es Salaam.

Zitto: Wanaohama hawadumazi upinzani

Awali kabla ya kufikwa na mkasa huo, MTANZANIA Jumamosi lilifanya mahojiano maalumu na Zitto kuhusiana na kitendo cha wanasiasa kuhama vyama, ambapo alisema si jambo geni na hawawezi kuzorotesha siasa za upinzani nchini.

Ingawa alisema kuhamahama ni haki ya kikatiba, lakini wao kama wapinzani wana kazi ya kutengeneza wanachama wapya, kizazi kipya ili kujenga vyama vitakavyoongeza mabadiliko ya kisiasa nchini.

“Kuhama kwa wanasiasa ni funzo kwetu na kwa wanasiasa vijana kuwa wanachama kunatokana na uthabiti na itikadi na imani waliyonayo, hata hivyo tunawatakia kila la kheri.

“Kwetu ni funzo, lazima tutengeneze wanasiasa wanaokuwa na sababu za kiitikadi na umadhubuti ili tuweze kupunguza watu wanaohama kutoka chama kimoja kwenda kingine,” alisema.

Aidha, akimnadi mgombea wa udiwani katika Kata ya Reli, Manispaa ya Mtwara- Mikindani, Mwajuma Hassan Ankoni, Zitto alisema serikali ni chanzo cha kuzorotesha usafirishaji wa zao la mbaazi linalolimwa kwa wingi mikoa ya kusini.

Alisema hali hiyo imesababisha wakulima kukosa soko na kufikia hatua ya kuuza mbaazi kilo moja kwa Sh 150.

Katika msimu uliopita mbaazi ziliuzwa kwa Sh 1,500 na kushuka kwa kasi, huku baadhi ya maeneo wakishindwa kuziuza kabisa.

“Serikali iliwaambiwa wananchi kuwa kuna soko India, wananchi wakalima kwa wingi zaidi, sasa zimekosa soko. Hili suala ni la kidiplomasia ndiyo maana India hawataki kuchukua mbaazi zetu. Hii ni aibu kwa serikali,” alisema Zitto.

Aidha, mgombea wa kiti hicho cha udiwani alisema ana uwezo wa kushirikiana na wananchi kuleta maendeleo kama alivyofanya kipindi akiwa mwenyekiti wa serikali za mitaa.

VITA YA MANENO

Aidha,  kampeni za sasa, kama zilivyo nyingine nyingi zilizopita, nazo zimetawaliwa na vita ya maneno ambayo  imewaibua baadhi ya makada wa vyama hivyo, akiwamo aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu),  Stephen Wasira na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Wasira amshukia Nyalandu

Mbunge wa zamani wa Jimbo la Bunda, mkoani Mara, Steven Wasira, aliibuka katika kampeni za uchaguzi wa udiwani Kata ya Mhandu, Wilaya ya Nyamagana, Mkoa wa Mwanza na kudai kuwa, kitendo cha  aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu kuhamia Chadema, ni sawa na mzimu unaokataa kwao.

Wasira, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, alitoa kauli hiyo wakati akimnadi mgombea udiwani wa CCM katika Kata ya Mhandu, Costantine Sima.

Alisema Chadema kisijidanganye kuwa kumpata Nyalandu kimelamba dume, ilhali Nyalandu alikimbia kwao Singida na kwenda kupokea kadi ya uanachama Mwanza.

“Nyalandu anadai amekwenda Chadema kutafuta Katiba Mpya…,  ipi hiyo? Wakati tukiwa kwenye Bunge la Katiba mwaka 2015 yeye alikuwa anatalii Marekani na Aunt Ezekiel, sasa leo anatafuta katiba ipi huyu!  Akiwa kwenye Bunge la Katiba kumbukumbu zinaonyesha hakuwahi kutoa wazo lolote kuhusu Katiba Mpya kwa sababu ya kuponda raha nje ya nchi, lakini sasa anataka kudanganya wananchi.

“CCM ndio imelamba dume kwa kuzoa vigogo lukuki wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi,” alisema.

Aidha, aliwaomba wananchi wa Kata ya Mhandu kutodanganyika na ulaghai wa Chadema na vyama vingine vya siasa, hivyo wamchague mgombea wa CCM, Costantine Sima, ili ashirikiane na madiwani wenzake wa CCM na serikali kuwapatia maendeleo wanayotarajia awamu hii ya tano.

Alisema iwapo wananchi wasipomchagua mgombea huyo, itakuwa ni sawa na simu isiyokuwa na laini yenye mtandao, hivyo ni vigumu kuwa na mawasiliano.

Chadema walia uhuni, uvunjifu wa sheria

Kwa upande wake, Chadema mkoani Arusha kimelalamikia uvunjifu wa sheria, ikiwamo maadili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, unaofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aidha, chama hicho kimetamba kulinda kura zao katika marudio ya uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika katika kata nane zilizopo mkoani Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Meya wa Jiji hilo, Calist Lazaro (Chadema), alisema kitabu cha maadili ya uchaguzi cha Mwaka 2015, chini ya kifungu cha 12A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 kinakataza baadhi ya vitu katika kipindi cha kampeni, CCM kimeendelea kuvunja masharti hayo.

“Miongoni mwa tuliyokatazwa ni mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya wasichanganye ziara za kikazi na shughuli za kiuchaguzi na wasitumie vyombo au watendaji wa serikali katika shughuli za uchaguzi kwa manufaa yao, kutangaza katika vyombo vya habari au kwa namna yoyote misaada au ahadi ya aina yoyote,” alinukuu na kuongeza:

“Imekatazwa kutoa ahadi za shughuli za maendeleo ya jamii, kwa mfano kujenga barabara, kusambaza maji na mambo mengine kama hayo, serikali ihakikishe viongozi na watumishi wa umma hawatumii madaraka au rasilimali za serikali kwa shughuli za kampeni za uchaguzi kwa manufaa ya chama chochote,” alisema.

Alisema licha ya kukatazwa kufanya hivyo, wameona wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri ambao ni wasimamizi wa uchaguzi wakiingilia uchaguzi kwa kutoa ahadi mbalimbali na kufanya kazi nyingine ambazo hazikuelezwa katika wakati huu.

“CCM imekiuka kanuni hizo za maadili ambapo jana, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amegawa bati katika soko la kwa Morombo, Kata ya Muriet na kuwaomba wananchi ambao kata zao zinarudia uchaguzi huo wasidanganyike na ahadi au misaada inayotolewa.

“CCM wamezidiwa mpaka wanavunja sheria na utaratibu. Hii ni aibu kwa CCM na Serikali kwa ujumla, kwamba kwa mara nyingine wanavunja utaratibu ambao walijiwekea wao wenyewe, tunakwenda kushinda, wamechanganyikiwa hawajui la kufanya,” alisema.

Lema: Wahuni wamepanga kutuvamia

Wakati huo huo, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), alisema kuna mkakati umepangwa na CCM kwa kushirikiana na kundi la wahuni kuvamia ngome za Chadema leo, baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara unaotarajiwa kufungwa na Kinana.

“Jumamosi kwenye ngome ya Chadema iliyopo Muriet baada ya mkutano wa kufunga kampeni za CCM, Green Guard wameelekezwa na kiongozi mmoja wa mkoa waje wafanye fujo, wawapige na kusambaratisha watu watakaokuwepo ili hiyo ngome isitumike kama mahali pa kuratibu uchaguzi Jumapili.

“Hatutakimbia ofisini kwetu, tutakaa tusubiri, njooni na mapanga, bunduki, mtatukuta na hatutakimbia makazi yetu. Leo (jana) asubuhi nimewatumia ujumbe mfupi wa maandishi IGP na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa kuwaeleza hali ya Arusha na naomba kumueleza IGP tena kuwa, Jeshi la Polisi Arusha linafanya kazi ya CCM,” alisema Lema.

Alidai kuwa, tangu kuanza kwa kampeni hizo, kuna matukio ambayo viongozi na wafuasi wa chama hicho wamefanyiwa, ikiwamo kuvunjiwa gari, kupigwa na mapanga na kuwa wana RB zisizopungua tisa ambapo wahusika wa matukio hayo wametajwa kwa majina, ila hakuna aliyewahi kukamatwa na kuhojiwa na Polisi.

“Wamesema watachukua kata hizi kwa nguvu, siyo mbaya, wanaweza wakajaribu, ila tumejaribu kueleza vilio vyetu kwenye vyombo vya habari na tunaonekana wajinga, tunamsihi na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, asithubutu hata kidogo kwa kufikiri askari walioko nyuma yake na mipango ya gizani na mikakati anayofanya wakati amezungukwa na bunduki akafikiri inaweza ikampa uimara katika uhalifu anaotaka kuufanya.

“Namuomba Mungu uchaguzi uende kwa haki na usalama, ninawataka vijana wetu na wanachama wa Chadema wawe wapole, wasikilize kisasi cha damu, lakini wasiwe wajinga wakauawa kwa mapanga huku wakiwa wamepiga magoti,” aliongeza Mbunge huyo.

Naye Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Elisa Mungure, alisema wamejipanga na wana uhakika wa kushinda katika zote nane ambazo asilimia zake ziko kwenye mabano kuwa ni Maroroni (85), Makiba (88), Ambureni (95), Leguruki (78), Muriet (90), Moita (87), Musa (80) na Ngabobo (85).

Alisema miongoni mwa sababu zinazowafanya washinde ni kutokana na madiwani waliokuwapo awali ambao walinunuliwa na kuhamia CCM, kurudishwa kuwania nafasi hizo.

Sirro:  Polisi tumejipanga

Wakati wanasiasa wakielekea kukamilisha kampeni zao kwa mivutano, Jeshi la Polisi nchini limesema limejipanga vyema kuimarisha ulinzi kwenye vituo vyote vya uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, alitoa rai kwa wananchi waliokwenye maeneo hayo kushiriki uchaguzi huo kwa amani na utulivu.

“Wakishapiga kura, warejee majumbani mwao na kwenye maeneo yao ya kazi kuendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa huku wakisubiri kutangazwa kwa matokeo,” alisema IGP Sirro.

Aidha, akizungumzia vurugu zilizotokea jana kwenye Kata ya Saranga, kati ya pande mbili za Chama cha Wananchi (CUF), alisema bado Jeshi hilo halijapata taarifa kamili.

Kayombo: Uchaguzi Kata ya Saranga palepale

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, John Kayombo, amesisitiza uchaguzi wa madiwani katika Kata ya Saranga uko palepale, licha ya vifaa vya uchaguzi kuteketea kwa moto  uliowashwa na watu wasiojulikana katika Ofisi ya Mtendaji wa kata hiyo usiku wa kuamkia leo.

Kayombo alisema tayari wameshatoa taarifa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambapo wameahidi kuleta vifaa hivyo kati ya jana na leo.

“Uchaguzi utafanyika tu, tumeshaangalia nini ambacho hatuna, NEC wametuonyesha ushirikiano, kwa ujumla vifaa vya uchaguzi ambavyo tulikuwa tumekwishapanga tayari kwa ajili ya kwenda kwenye vituo vyetu 126 vimeungua, kwa hiyo tuna vifaa vichache sana vilivyobaki, ni 20 tu,” alisema.

Aidha, Kayombo amevitaja vifaa vilivyoungua kuwa ni pamoja na masanduku ya kupigia kura 108, nyaraka za uchaguzi na za Mtendaji wa Kata na vitendea kazi vya Mtendaji, ambavyo thamani yake bado haijajulikana.

Mikoa hiyo inayofanya uchaguzi wa marudio ni Geita, Mwanza, Dodoma, Ruvuma, Tabora, Songwe, Mbeya, Rukwa, Lindi, Mtwara, Iringa, Singida, Simiyu, Arusha, Tanga, Kilimanjaro,  Dar es Salaam, Manyara na Morogoro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles