28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

MNANGAGWA Mitihani 12 ya mrithi wa Zimbabwe

 

HARARE, ZIMBABWE

LICHA ya Rais wa Kwanza wa Zimbabwe, Robert Mugabe, kutohudhuria sherehe za kuapishwa mrithi wake, Emmerson Mnangagwa, kiongozi huyo mpya wa taifa hilo amesema anamchukulia mkongwe huyo wa siasa za Afrika kama baba yake na mshauri wake mkuu.

Mnangagwa, anayetambulika zaidi kama mamba kutokana na ukali wake na aina za siasa zake, aliyasema hayo jana mjini Harare, Zimbabwe, baada ya kuapa mbele ya maelfu ya wananchi wa taifa hilo waliojitokeza kwenye uwanja wa taifa wa mpira.

Rais huyo atakayeliongoza taifa hilo mpaka mwaka kesho ambapo uchaguzi mkuu utafanyika, ameshika madaraka baada ya jeshi la nchi hiyo kumuweka kizuizini Mugabe, kisha kutokea shinikizo la kumtaka mkongwe huyo ajiuzulu. Awali aligoma, mpaka pale Bunge lilipotaka kujadili hoja ya kumtoa madarakani na kumshtaki, ndipo alipoandika barua ya kung’atuka.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wachambuzi walidhani mahusiano ya wawili hao yatayumba, hivyo kauli ya Mnangagwa kwa sasa inafungua mjadala mpya.

“Alituongoza kwenye mapambano ya kupata uhuru wetu, alikuwa kiongozi kwenye wakati mgumu na wenye changamoto nyingi.

 

“Namshukuru Rais Mugabe kuongoza Zimbabwe kwa usahihi tangu tumepata uhuru, hata kama kutakuwa na makosa aliyowahi kufanya, kivuli chake kisifutwe kwasababu ana mchango mkubwa. Binafsi Komredi Mugabe anabaki kuwa Baba na mshauri wangu,” alisema.

 

Mitihani 12 ya Mnangagwa

 

Mnangagwa pia alieleza mambo zaidi ya 12 atakayosimamia kwenye utawala wake, ikiwa ni pamoja na kufufua uchumi wa Zimbabwe, kuboresha mauzo ya nje, kuvutia wawekezaji, kuboresha sekta ya fedha, kuboresha mahusiano ya kidiplomasia na kuhakikisha nchi hiyo inatolewa vikwazo mbalimbali vya kiuchumi iliyowekewa na mataifa mbalimbali.

 

Aliwahakikishia wananchi wake kuwa, atailinda Katiba ya nchi hiyo, wananchi na kupambana na kundi lolote litakalotaka kuiharibu Zimbabwe.

“Hatuwezi kubadili historia yetu, licha ya kuwapo mambo mengi tunayoweza kuyafanya leo. Sitaruhusu mtu yeyote aifanye nchi hii katika mazingira magumu ya ushirikiano na mataifa ya nje.

“Nchi yetu itaimarishwa tangu pale palipowekwa msingi na Komredi Mugabe. Dunia inapaswa kufahamu kuwa suala la kumiliki ardhi ni muhimu kwetu.”

Aliongeza kwa kusema changamoto inayowakabili kwa sasa ni matumizi bora ya ardhi ambayo yatachochea mapambano dhidi ya njaa.

“Tume ya Ardhi itashughulikia na kutatua masuala yote, wamiliki wa zamani wa ardhi watatambuliwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi.”

Akizungumzia uchaguzi mkuu wa mwaka 2018, alisema: “Nathibitisha uchaguzi ujao utafanyika kama ulivyopangwa na wa kidemokrasia. Tutaheshimu sheria na mikataba yote ya Umoja wa Mataifa. Nitaimarisha umoja wa nchi bila kujali tofauti za kisiasa. Uchumi wa nchi utaendeshwa kwa sera ya kilimo ambayo itaongeza ajira,” alisema.

Pia alisema, msingi mkubwa alionao sasa ni kuhakikisha anavutia wawekezaji nchini humo pamoja na sera shirikishi zenye tija katika masoko. Amesisitiza kuwa, atahakikisha anapambana na vitendo vya ulaji rushwa na watakaobainika sheria itachukua mkondo, na kuimarisha nidhamu ya utumishi wa umma, hivyo hakutakuwa na utendaji wa mazoea.

Serikali yake pia itahakikisha inaongeza tija katika usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi, kutunga sheria za uendeshaji wa benki, uhusiano mzuri na mataifa ya kigeni na kuomba kuondolewa vikwazo vilivyowekwa dhidi yao.

“Uwekezaji wowote kutoka nje ya nchi utakuwa salama hapa Zimbabwe,” alisema Mnangagwa.

Mbali na raia wa Zimbabwe, viongozi wengine wa Afrika waliohudhuria kuapishwa kwa Mnangagwa ni Rais wa Zambia, Edgar Lungu, Ian Khama (Botswana), marais wa zamani Zambia, Kenneth Kaunda na Rupia Banda.

Wengine ni Waziri wa Mawasiliano na Huduma za Posta, Siyabonga Cwele, Makamu wa Rais wa Namibia, Nickey Iyambo, rais wa zamani wa Namibia, Sam Nujoma na Rais wa Msumbiji, Felipe Nyusi.

KAULI YA SADC

Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imesema iko tayari kushirikiana kwa karibu na kiongozi mpya wa Zimbabwe na serikali yake. Rais wa Afrika Kusini na Mwenyekiti wa SADC, Jacob Zuma, hawajahudhuria sherehe hizo. Hata hivyo, alitoa udhuru.

MNANGAGWA NI NANI?

Emmerson Dambudzo Mnangagwa alizaliwa Septemba 15, 1942, katika kijiji cha Shabani, ambacho mwaka 1982 kilibadilishwa jina na kuitwa Zvishavane, kilichoko katika Jimbo la Midlands.

Alisoma Shule ya Msingi Lundi. Familia yake ilikuwa inaishi Zambia, ambako alihitimu elimu ya msingi ya darasa la nne, baadaye alijiunga na Shule ya Bweni ya Mumbwa kusoma darasa la tano na sita.

Baadaye alichaguliwa kujiunga na Shule ya Biashara ya Kafue kusomea ujenzi, ambapo ilimpa nafasi ya kwenda Chuo cha Ufundi cha Hodgson. Hata hivyo, mwaka 1960 alifukuzwa chuoni hapo kwa tuhuma za kujihusisha na harakati za kisiasa ambazo zilipigwa mafuruku.

Alijiunga na kundi la UNIP, ambalo lilikuwa vuguvugu la wanafunzi chuoni hapo katika harakati za siasa. Alihitimu elimu ya sekondari na kidato cha tano na sita akiwa gerezani, iliyomwezesha kwenda kusomea shahada ya sheria akiwa gerezani. Mwaka 1972 alihitimu shahada ya uzamili katika sheria katika Chuo Kikuu cha London.

Mnangagwa ni miongoni mwa wanajeshi waliopigana vita ya Chimurenga dhidi ya Waingereza. Pia amewahi kuwa Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Zimbabwe (CIO).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles