24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mkwasa kuongezewa mkataba Stars

Mkwasa-CharlesJUDITH PETER NA JENIFFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) linafikiria kumpa mkataba wa kudumu kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa, pamoja na viongozi wengine wa benchi la ufundi baada ya kusaidia kuinua kiwango cha wachezaji ambao wameonekana kufurahia uwepo wake ndani ya kikosi hicho.

Viongozi wengine wa benchi la ufundi wanaofikiriwa ni Kocha Msaidizi, Hemed Morocco, kocha wa makipa Peter Manyika, Meneja Omary Kapilima na Mshauri wa benchi la ufundi, Abdallah Kibadeni ‘King’.

Habari ambazo MTANZANIA limezipata zimedai kuwa shirikisho hilo lilikutana na wachezaji wa Stars mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Nigeria ‘Super Eagles’ na kuwauliza kama wanaridhika kuendelea kufundishwa na kocha huyo.

Imedaiwa kuwa wachezaji walisifia uwezo wa Mkwasa wakidai wanamuelewa vizuri mambo anayofundisha pamoja na kufurahia uwepo wake kwenye kikosi hicho, jambo ambalo linaonekana kuwaingia kichwani viongozi hao wa TFF ambao wanaendelea kufanyia kazi uamuzi wa kuwapa mikataba ya kudumu.

Chanzo hicho kimedai kuwa TFF pia imeridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na Stars Jumamosi iliyopita, kwani kimeashiria mwelekeo mzuri wa timu hiyo ambayo inakabiliwa na kibarua kigumu kwenye kundi G ambalo linaundwa na timu nyingine za Misri na Chad.

Wakati huo huo Mkwasa amesema badala ya Watanzania kumpongeza kwa ajili ya kikosi chake kufanya vizuri dhidi ya Nigeria, wanatakiwa kuwaombea ili wabadilishe na kumaliza kabisa zama za kufanya vibaya kwa timu hiyo.

Alisema kilichobakia sasa ni sala tu kutoka kwa Watanzania, kwani bado wana mtihani mzito kurudisha sifa ya timu hiyo.

“Pongezi zinatosha nawaomba Watanzania watuombee, tunachopambana hapa ni kufanya vizuri na kufanikiwa kupata nafasi ya kucheza Fainali za Afrika, lakini vilevile timu yetu imepoteza sifa yake muda mrefu sana hivyo tunajaribu kadiri ya uwezo wetu kuirudisha,” alisema Mkwasa.

Mkwasa alisema bado wanakabiliwa na safari ndefu ya kufanya vizuri kwenye michuano mingine ya kimataifa, hivi sasa akili zote zimehamia kwenye mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Malawi.

“Tuna kibarua kigumu mbele tutakabiliana na Malawi Oktoba, tuna muda mchache wa kujiandaa hasa ukizingatia wachezaji watakuwa kwenye klabu zao kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu,” alisema.

Stars ikifanikiwa kuifunga Malawi katika hatua hiyo ya awali, itacheza na Algeria Novemba mwaka huu.

Ushindi wa Stars dhidi ya Algeria utakuwa umeipa nafasi ya kupangwa kwenye makundi ya kuwania kucheza fainali hizo nchini Urusi 2018.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles