24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Msajili akionya Chama cha TPP

Pg 2 sept 8NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

SERIKALI imekionya Chama cha Tanzania Peoples (TPP) kuacha mara moja kujishughulisha na shughuli za kisiasa kwa sababu hakina usajili na kuendelea kufanya hivyo kinavunja sheria.

Akizungumza jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari jana, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alisema vyama vilivyosajiliwa ndivyo vinavyopaswa kuendelea na shughuli mbalimbali za kisiasa kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Alisema hadi sasa ofisi yake inavitambua vyama 22 ambavyo vimekamilisha usajili na vina sifa zote ambapo TPP haitambuliki na ilifutiwa usajili tangu Machi 20, mwaka 2002 kutokana kupoteza sifa ikiwamo kukosa viongozi wa kitaifa.

“Chama cha TPP hakitambuliki na hakipo kwenye orodha ya vyama vyetu kutokana na kukosa sifa na wanachama na viongozi waliokuwapo, awali walipewa taarifa,” alisema Nyahoza.

Alisema TPP ilisajiliwa rasmi mwaka 1993, lakini kutokana na sababu mbalimbali ilishindwa kufikia matakwa ya vyama vya siasa na msajili aliamua kuiondoa kwenye orodha yake.

Nyahoza alisema kabla ya kufutiwa usajili, taratibu mbalimbali zilifuatwa ambapo pamoja na chama hicho kujitetea, utetezi wao haukuwa na mashiko na waliamua kukiondoa katika orodha ya vyama vya siasa.

Alisema kutokana na kufutiwa usajili huo TPP hawakushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na hata ule wa 2010, hivyo wanashangaa kuibuka sasa na kudai wao hawatambui kufutiwa usajili.

“Kwa niaba ya Msajili Jaji Francis Mutungi, napenda kuwatahadharisha wanasiasa na baadhi ya vyama vinavyoibuka kuacha kuvunja sheria na kuheshimu sheria zilizopo chini ya msajili,” alisema Nyahoza.

Alisema wahusika waliosajiliwa na ofisi ya msajili ndio wanaoruhusiwa kuendelea na kampeni ambazo ni za kistaarabu na zenye amani.

“TPP hakipo kwa mujibu wa sheria, kifungu cha 7 (3) cha sheria ya vyama vya siasa sura ya 358 kinakataza taasisi kufanya kazi kama chama cha siasa bila ya kusajiliwa na msajili wa vyama,” alisema Nyahoza.

Pia alisema kifungu cha 8 (b) cha sheria ya vyama vya siasa kama ilivyorekebishwa mwaka 2009 kinakataza mtu yeyote kufanya shughuli za kisiasa kwa jina la chama ambacho yeye si mwanachama.

Akizungumzia kuhusu kampeni zinazoendelea hivi sasa, alisema ofisi yake inaendelea kushughulikia matamko ya gharama ya uchaguzi ambapo wakurugenzi husika wanaendelea kukusanya fomu kwa vyama mbalimbali.

Alisema hadi sasa vyama vyote vilivyopo kwenye usajili vinaendelea vizuri, lakini alivitahadharisha kuacha matumizi ya lugha chafu.

Alivitaja baadhi ya vyama vinavyotambuliwa kuwa ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha NCCR – Mageuzi, Demokrasia Makini (MAKINI), Chama cha Haki na Ustawi (CHAUSTA), Chama cha Kijamii (CCK) , Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA), na vingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles