24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mkuu wa ujasusi Marekani ajitenga na utawala wa Trump

WASHINGTON, MAREKANI

MKURUGENZI wa Idara ya Ujasusi Marekani, Dan Coats, amejiuzulu.

Kujiuzulu kwake kumekuja baada ya Rais wa Marekani  Donald Trump kutuma ujumbe kwenye twitter akisema Coats atajiuzulu mwezi Agosti na kwamba atamteua mbunge wa Texas, John Ratcliffe kuchukua nafasi hiyo.

Ratcliffe ni mfuasi kindakindaki wa Trump ambaye iwapo ataidhinishwa ataendana na sera zake.

Trump mwenyewe amemuelezea Ratcliffe kama mtu ambaye  ataongoza nafasi hiyo na kuhimiza taifa kubwa analolipenda.

Coats na Trump wametofautiana mara kwa mara kuhusu Urusi, Iran na Korea kaskazini.

Coats alikuwa mkurugenzi wa idara ya taifa ya ujasusi, aliyekuwa na jukumu kushughulikia mashirika 17 ya ujasusi nchini Marekani likiwemo la CIA na NSA.

Katika kipindi kizima kama Mkurugenzi wa Ujasusi alipingana mara kwa mara na Trump ambaye amekuwa akiyashutumu mashirika ya ujasusi.

Januari mwaka huu Trump aliwashutumu wakuu wa ujasusi kwa kuchukulia kwa urahisi tishio la Iran pasipo kuchukua hatua.

Coats anaingia katika orodha ndefu ya msururu wa maofisa walioacha kazi na kuondoka katika utawala wa Trump.

Aliyekuwa waziri wa ulinzi James Mattis na waziri wa mambo ya kigeni Rex Tillerson ni miongoni mwa  walioondoka katika utawala wa Trump.

Katika barua yake ya kujiuzulu kwa rais, Coats amesema jamii ya majasusi Marekani imekuwa na nguvu zaidi ya ilivyoshuhudiwa wakati wa muda wake wa miaka miwili na nusu ya kuhudumu.

“Kutokana na hilo, ninaamini muda umewadia kwangu mimi kusogea katika ukurasa mwingine wa maisha yangu,” aliandika.

Coats amesema Februari Rais Trump alimuomba abakie katika wadhifa huo, hata hivyo tofauti zao kuhusu sera za kigeni zilionekana kutopatana mara nyingine.

Inaelezwa Coats alitofautiana mara kadhaa na Trump kuhusu Iran, Korea Kaskazini na Urusi

Zaidi walitofuatiana kuhusu Urusi kuingilia kati uchaguzi Marekani, mkataba wa nyuklia wa Iran na jitihada za Trump katika kuidhinisha mtazamo mpya na Korea Kaskazini.

Likimnukuu, gazeti la The Washington Post limeripoti kuwa Coats alitambua kwamba hakuwa na budi bali kuondoka katika wadhifa wake kutokana na uhusiano wake wenye utata na Trump.

Coats ameliambia gazeti hilo kuwa alihisi kutengwa na Rais Trump kuhusu masuala ya usalama wa kitaifa.

Mwaka jana, mkuu huyo wa ujasusi alikiri kuwa Trump hakumuarifu kuhusu mkutano wake wa faragha na rais wa Urusi, Vladimir Putin huko Helsinki.

“Angeniuliza kuhusu namna mkutano huo ulivyopaswa kufanyika, Ningependekeza njia nyingine,” amesema Coats.

Alicheka kwa mshangao aliposikia kuhusu ziara iliyopendekezwa ya rais Putin katika ikulu ya Marekani White House, na kuuambia umati katika hafla moja kuwa : “Hiyo itakuwa ziara maalum.”

Coats ni mwanadiplomasia wa zamani, amehudumu kama mkurugenzi wa idara ya taifa ya ujasusi tangu Machi 2017, alipomrithi James Clapper.

Alizaliwa Jackson, Michigan, alihitimu katika vyuo vikuu viwili kwa shahada ya sayansi ya siasa na sheria miaka ya 60.

Alihudumu kwa mihula miwili kama seneta wa Indiana, kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 na kwa mara nyingine kuanzia 2011 hadi 2017.

Coats pia alihudumu kama balozi wa Marekani kwa Ujerumani kuanzia 2001 hadi 2005 katikati ya muhula wake katika seneti.

Atakayerithi nafasi yake, Ratcliffe ni mfuasi maarufu wa Trump na sera zake. 

Ratcliffe amehudumu kama mbunge wa Texas 4th District tangu mwaka 2015.

Trump amesema Ratcliffe ni mbunge anayeheshimika sana ambaye ataongozana kuhimiza ukubwa wa taifa analolipenda.

Ratcliffe anatarajiwa kuteuliwa kuichukua nafasi ya Coats kama mkurugenzi wa idara ya taifa ya ujasusi endapo uteuzi wake utaidhinishwa.

Mtazamo wa Ratcliffe unatarajiwa kuwiana na wa Trump zaidi katika wadhifa wake mpya.

Wiki iliyopita, Ratcliffe alimtetea Trump wakati wa kutoa ushahidi wa Robert Mueller, aliyeongoza uchunguzi wa miaka miwili kuhusu Urusi kuingilia kati uchaguzi wa Marekani mwaka 2016.

Ratcliffe alisema Mueller hana mamlaka “ya kubaini iwapo Trump ana hatia au kumuondoshea makosa”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles