NA FRANCIS GODWIN -IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amenusurika kifo, huku askari wawili wakijeruhiwa vibaya katika ajali iliyohusisha teksi.
Ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa 12.25 asubuhi eneo la nje ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Barabara ya Pawaga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema katika tukio hilo, askari polisi Antony Mwita alijeruhiwa wakati akijitosa kumwokoa Masenza asigongwe na gari hilo dogo aina ya Toyota Carina lenye namba za usajili T 479 CKZ, ambalo liliparamia wananchi waliokuwa katika maandalizi ya kuanza mazoezi ya viungo yaliyofanyika Uwanja wa Samora.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Iringa mjini, Abed Kiponza, aliyekuwa mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, alisema kuwa alikuwa hatua kama 15 kutoka eneo la ajali na aliona gari hilo likiwavaa watu hao, ambao walikuwa kando ya barabara.
Kiponza alisema kama si askari huyo kumsukuma kwenye mtaro RC Masenza basi gari hilo lingemgonga.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, aliwataja majeruhi ni askari mwanamke wa Jeshi la Magereza, Greety Mwakipesile ambaye inadaiwa alivunjika mguu na Mwita aliyeumia usoni.
Kwa mujibu wa Kasesela, Masenza yupo salama na alijumuika na wananchi katika mazoezi hadi mwisho.
Aidha Kasesela alimpongeza Mwita aliyefanya jitihada kumwokoa RC Masenza na askari wengine walioshiriki kumkamata dereva wa gari hilo pasipo kutumia nguvu yoyote na kuwataka wananchi kuiga mfano huo wa ukamataji salama.