29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mkutano SADC kutengeneza ajira 5,000 kuingiza Sh bilioni 10

Na Waandishi wetu

-Dar es Salaam

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Faraji Mnyepe, amesema mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), utakaofanyika nchini mwezi Agosti, unatarajiwa kuingiza zaidi ya Sh bilioni 10 na kutengeneza ajira 5,000.

Dk. Mnyepe alisema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa wizara hiyo na wamiliki na wafanyabiashara wa hoteli.

Aliwataka Watanzania kuchangamkia fursa hiyo katika mkutano huo ambao unatarajiwa kuhudhuriwa na marais takibani 16 na watu zaidi ya 1,000.

Pia aliwataka wamiliki na wafanyabiashara wa hoteli kuzingatia mwongozo wa Serikali uliotolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusiana na suala la ubadilishaji wa fedha za kigeni kwa kuwataka kuwaelekeza wageni kubadilishia fedha zao benki na katika hoteli ambazo zimeidhinishwa.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, aliwataka wamiliki na wafanyabiashara wa hoteli jijini Dar es salaam kutumia fursa hiyo.

Aliwataka kutoa huduma bora kwa weledi na uzalendo usiotiliwa shaka ili waweze kunufaika na uwepo wa ugeni huo.

 “Ninyi ni watu muhimu sana katika ugeni huu wa SADC, tushirikiane kuufanya mkutano huu kuwa wa mafanikio kwa ukarimu na uzalendo wetu, kufanya hivyo kutatufanya kuingiza kipato katika biashara zetu kwa kuwa tukifanya vizuri watakumbuka kila watakapokuwa wanakuja Tanzania,”alisema.

Alisema ataendelea kukutana na wadau mbalimbali na wafanyabiashara wa sekta binafsi ili kuhakikisha fursa ya kufanyika kwa mkutano wa SADC inawanufaisha wadau mbalimbali wakiwemo wajasiriamali na wafanyabiashara.

Hivi karibuni akitangaza mkutano huo wa 39 wa SADC, Profesa Kabudi alisema utatoa fursa za utalii, hoteli, usafirishaji, vyakula na nyingine nyingi ambazo zinatokana na uwepo wa ugeni huo mkubwa.

Pia fursa nyingine itakayoweza kutumiwa na Watanzania ni kwa soko la Kariakoo kujiandaa kupokea ugeni huo kwani Profesa Kabudi amesema baadhi ya nchi zinazohudhuria mkutano huo, huchukulia Kariakoo kama Dubai.

Alisema kwa sasa Tanzania ndiyo inayouza bidhaa nyingi katika soko la SADC ikilinganishwa na nchi zote za Afrika Mashariki, hivyo ni vyema kutumia fursa ya mkutano huo kukuza masoko ya bidhaa za ndani.

Profesa Kabudi alisema mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Agosti 17 na 18 na kabla yake kutatanguliwa na mkutano wa mawaziri na makatibu wakuu wa mambo ya nje kutoka nchi wanachama, utakaofanyika kuanzia Agosti 9 hadi 16. 

Alisema Julai 22 hadi Julai 26 yatafanyika maonesho maalumu ya maadhimisho ya awamu ya nne ya wiki ya viwanda ya SADC kwenye eneo la Mlimani City, manyesho ambayo pia yatatoa fursa kwa Watanzania. 

Alisema maonesho hayo yatatoa fursa kwa watafutaji wa masoko ya bidhaa, waagizaji na wazalishaji kujua namna ya kufika katika nchi wanachama za SADC na namna ya kushirikiana kibiashara.

Mara ya mwisho mkutano kama huu ulifanyika Tanzania mwaka 2003/2004 ambapo Rais wakati huo, Benjamin Mkapa alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa jumuiya hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles