29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Matumizi mifuko plastiki yaja kivingine

NORA DAMIAN Na  FRANCIS GODWIN 

DAR/IRINGA 

-DAR ES SALAAM

ZIKIWA zimepita siku 15 tangu Juni Mosi zilipoanza kutumika kanuni za usimamizi wa mazingira zinazopiga  marufuku mifuko ya plastiki, imebainika watumiaji na wazalishaji wameirudisha sokoni kivingine.

Kabla ya kuanza kwa marufuku hiyo, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, alisema katika kutekeleza sheria ya kupiga marufuku vifungashio hivyo, mifuko ambayo inatumika kufungia maji (kandoro) na barafu, nayo pia haitaruhusiwa.

Kutokana na mifuko hiyo kurudi sokoni, Ofisi ya Makamu wa Rais imetoa taarifa kwa umma ikisema “baada ya kuanza kwa utekelezaji wa katazo la kutumia mifuko ya plastiki baadhi ya wazalishaji na wasambazaji wamebadilisha mifuko laini ya plastiki isiyokuwa na mishikio na kuitumia kama vibebeo vya bidhaa. 

“Hii ni kinyume na kanuni ya 8. Kanuni ya 9 inatoa msamaha kwa baadhi ya vifungashio vya plastiki kwa ajili ya huduma za afya au ambavyo vinatumika kwenye kufungashia bidhaa za viwandani au sekta ya ujenzi au sekta ya kilimo au vyakula au usafi na udhibiti wa taka. 

“Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linaandaa viwango vya vifungashio hivi ambavyo vitaainisha kiwango cha unene na uwekwaji wa lakiri na kutambulisha bidhaa iliyofungashwa kabla ya kuuzwa. 

“Ofisi ya Makamu wa Rais ina utahadharisha umma kuwa ni makosa kisheria kubadili matumizi ya vifungashio hivyo kuwa mifuko ya kubebea bidhaa. Adhabu stahiki zitatolewa kwa watengenezaji, waingizaji, wasambazaji na watumiaji wa vifungashio vya plastiki vilivyozalishwa ama kuingizwa nchini na kutumika kama vibebeo vya bidhaa,” inaeleza taarifa hiyo.

Pia ilibainika kuwa mifuko hiyo inatumiwa na mama ntilie kufunika vyakula wakati wakipika.

Hali hiyo iligundulika baada ya Kamati ya Kukagua Mifuko ya Plastiki katika Manispaa ya Ilala kufanya ukaguzi katika Soko la Kariakoo na kushuhudia mama lishe wakiitumia kufunikia vyakula. 

Mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni mwanasheria wa manispaa hiyo, Ally Kwikazanya, alisema wanaendelea kupita maeneo mbalimbali kutoa elimu na kuangalia maendeleo ya marufuku hiyo.

“Moja kati ya changamoto tulizokutana nazo kwenye ukaguzi ni akina mama lishe kuendelea kutumia mifuko ya plastiki kwani wengine wanaitumia kufunikia vyakula, tunaendelea kuwaelimisha kwamba mifuko hiyo hairuhusiwi,” alisema Kwikazanya.

Akizungumza na MTANZANIA, Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Manchare Heche, alisema vifungashio vinapobadilishwa matumizi, vinapoteza maana ambayo Serikali ilikuwa inaitarajia.

“Mifuko iliyosamehewa kwa ajili ya vifungashio inatakiwa itumike tu kwa kazi ya kifungashio, lakini inapobadilishwa matumizi na kutumika kwa kazi nyingine tunapoteza maana kabisa.

“Mtu anachukua mfuko wa mkate anautumia kubebea vitu vingine kama nyama au matunda, suala ambalo ni kinyume na taratibu,” alisema.

VIFUNGASHIO VYA MIWA

Heche alisema Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linaendelea kuandaa viwango vya mifuko itakayotumika kama vifungashio vya bidhaa mbalimbali ikiwamo miwa na nyingine. 

“Inaandaliwa utaratibu wake namna ya kuiweka, kwa sasa hivi inaweza kuendelea kutumika (akimaanisha iliyopo sasa) na viwango vikishakuwa tayari, tutataja kama hiyo ya miwa inatakiwa iwe na unene gani,” alisema.

 Hata hivyo, alisema licha ya mifuko hiyo kuendelea kutumika, lakini haitakiwi kutupwa ovyo na kuonya kuwa atakayebainika atakuwa ametenda kosa.

“Haimaanishi kwamba hiyo iliyosamehewa iwe inatupwa tu ovyo, tutakuwa hatujafanya kitu, watumiaji wana wajibu wa kuitupa kwenye maeneo ambayo yametengwa kisheria, ukitupa kienyeji unaweza kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema.

MAENDELEO YA KAMPENI 

Akizungumzia maendeleo ya kampeni hiyo, Heche alisema inaenda vizuri kwani kumekuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali.

“Watu wametii, timu ya wataalamu wetu walikuwepo kwenye maeneo ya nchi, viongozi wa dini wametusaidia kutoa elimu,” alisema.

Kwa mujibu wa Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za Kupiga Marufuku Mifuko ya Plastiki, kitendo cha kumiliki au kutumia mifuko ya plastiki adhabu yake ni faini isiyopungua Sh 30,000 lakini isiyozidi Sh 200,000 au kifungo kisichozidi siku saba au vyote kwa pamoja.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, kitendo cha kuzalisha au kuingiza nchini mifuko ya plastiki adhabu yake ni faini isiyopungua Sh milioni 20 na isiyozidi Sh bilioni moja au kifungo kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.

Kitendo cha kusafirisha nje mifuko ya plastiki adhabu yake ni faini isiyopungua Sh milioni 20 au kifungo kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.

Kuhifadhi au kusambaza mifuko ya plastiki, adhabu yake ni faini isiyopungua Sh milioni 5, lakini isiyozidi Sh milioni 50 au kifungo kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.

Hapi aja na marufuku yake

Katika hatua nyingine, Mkuu wa  Mkoa wa Iringa, Ally Hapi, amesema mtu akikumbwa na mfuko wa plasiti usio na nembo ya Shirika la Viwango (TBS), atachukuliwa hatua.

Alitoa kauli hiyo baada Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mafinga, Chalresy Makoga, kudai wafanyabiashara   kugeukia matumizi ya  mifuko   hiyo ya plastiki yenye  rangi nyeupe.

Pia aliziagiza halmashauti zote za  mkoa wa Iringa  kuendelea  kutoa   elimu na  kuwachukulia  hatua   wale  wote  ambao  wanatumia  mifuko ya plastiki  kufungashia  bidhaa.

Mkuu wa Wilaya ya  Mufindi, Jamhuri Wiliam,  alimkabidhi Hapi mifuko ya plastiki iliyosalimishwa na wananchi akisema ilisalimishwa katika ofisi za halmashauri na wafanyabiashara .

Wiliam alisema Wilaya ya  Mufindi  ilitoa elimu kwa   wananchi  juu ya  zuio la matumizi ya  mifuko  hiyo na   hadi  sasa   wameanza matumizi ya  mifuko mbadala   inayotengenezwa  na  vikundi vya wajasiriamali kutoka ndani ya  wilaya  hiyo kwa  kutumia  karatasi kutoka  kiwanda cha Mgololo  kilichopo wilayani  hapo .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles