Elizabeth Joachim, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni za Madini Pangea (Pangea Minerals Limited), Bulyanhulu na North Mara, Asa Mwaipopo (55), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka tisa yakiwamo kughushi, utakatishaji fedha na kujipatia Dola za Marekani 840,000.
Akisomewa mashtaka hayo leo Jumanne Oktoba 23, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na mawakili wa serikali Faraja Nchimbi na Jacqline Nyantori, wamedai mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda mashtaka hayo Aprili 11 mwaka 2008 na Juni 30 mwaka 2017.
Mshtakiwa huyo pia anadaiwa kutenda makosa ya kula njama, kuongoza uhalifu wa kupangwa, kughushi, ukwepaji wa kodi na utakatishaji wa fedha.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka ulidai upelelezi bado haujakamlikika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 31, mwaka huu ambapo upande wa utetezi umeomba upelelezi uharakishwe.