32.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 5, 2024

Contact us: [email protected]

Wakulima watendewe haki bei ya korosho



MOJA ya habari iliyopewa uzito kwenye gazeti hili leo, ni uamuzi wa wakulima wa zao la korosho mkoani Mtwara kugoma kuziuza kwa madai ya bei kuwa ndogo.

Kampuni 15 zilituma zabuni za kununua korosho ghafi kwa bei ya juu ya Sh 2,717 kwa kilo moja na bei ya chini ikiwa ni Sh 1,711 ikiwa ni tofauti na msimu uliopita kilo moja ya korosho ilinunuliwa kwa Sh 3,850.

Wakulima hao walifikia uamuzi huu katika mnada wa wazi uliofanyika Kijiji cha Makukwe, Wilaya ya Newala mkoani Mtwara mbele ya Naibu Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji, Omary Mgumba na Mkuu wa Mkoa, Gellasius Byakanwa.

Mnada huo uliendeshwa na utaratibu mpya ambapo wanunuzi walitakiwa kufika wenyewe katika minada wakiwa na barua za zabuni tofauti na misimu iliyopita ambayo walikuwa wakifikisha barua kutoka vyama vikuu.

Uamuzi wa wakulima hao kugoma kuuza zao hilo ambalo ndilo wanalitegemea kuendesha maisha yao ya kila siku, ni dalili ya wazi kwamba kwa muda mrefu wamekuwa wakinyonywa bei kutoka kwa wanunuzi hasa kampuni kubwa ambazo zinanufaika na kuwaacha wakiwa hoi, licha ya kuteseka msimu mrefu wakiwa shambani.

Tunatambua wakulima wa ukanda wa kusini wametaabika kwa kipindi kirefu, hivyo tunaamini msimamo huu utakuwa mkombozi wao wa kuhakikisha wanapata fedha kulingana na kazi ambazo wanazifanya msimu mzima.

Tunakubaliana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Byakanwa ambaye bila kuficha hisia zake, aliwaunga mkono wakulima hao kwa kugomea bei.

Hii ni dalili ya wazi kwamba zama za uonevu dhidi ya mkulima wa korosho zinaelekea kuzikwa sasa.

Ni jambo la kusikitisha kila mwaka wanunuzi eti ndio wamekuwa mabingwa wa kuwapangia bei wakulima, bila kujali maumivu wanayokumbana nayo kila msimu.

Hakuna ubishi korosho za Tanzania zimekuwa zikisifika mno katika soko la dunia, sasa iweje wakulima wabaki wanapiga miayo?

Umefika wakati sasa wakulima wakasimamia thamani ya korosho yetu, ambayo imekuwa na thamani kubwa katika soko la dunia, badala ya kuwaachia watu wachache ambao wananeemeka kupitia migongo yao.

Takwimu zinaonesha kwa mnada huo tu, mahitaji ya zao hili kwa jana ilikuwa ni tani 10, wakati mkoa mzima una tani 2,873 hivyo  wakulima wasikurupuke kwa sababu wanunuzi hawa watarudi tu kwa sababu mzigo upo.

Sisi MTANZANIA tunasema haiingii akilini alime mkulima alafu apangiwe bei na mnunuzi, ndiyo maana tunasisitiza kuwa waendelee kutunza korosho katika ubora unaotakiwa kwa sababu wanunuzi hawa watarudi kwa kuwa wana uhitaji.

Tunatambua namna ambavyo wakulima hawa wanavyotumia gharama kubwa ya kutunza mashamba yao hadi kufikia hatua ya mavuno, sasa iweje wasinufaike na kile walichohangaika nacho msimu mzima?

Wakulima hawa wametaabika miaka mingi, umefika sasa wakati wa Serikali kuhakikisha inawasaidia kwa kila namna ili watendewe haki katika bei inayoendana na thamani ya korosho zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles