Derick Milton, Simiyu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, Melkzedeck Humbe amemtaka mkandarasi mpya wa ujenzi wa stendi ya ya kisasa ya halmashauri hiyo kukamilisha ujenzi ndani ya miezi miwili.
Hatua hiyo imekuja zikiwa zimepita siku 18 tangu Mkurugenzi huyo avunje mkataba na Kampuni ya Kings Builders ambayo ilikuwa ikishirikiana na Kampuni ya Helen Construction Co.Ltd za Dar es Salaam ambazo zilikuwa zikijenga stendi hiyo.
Humbe amesema hayo leo Jumatano Oktoba 30 wakati wa utiaji saini ya makubaliano na Kampuni mbili za ujenzi, Mumangi Trans and Construction Ltd na Pek Brothers (T) Ltd zote za mkoani Mara, ambazo zitakamilisha ujenzi huo.
Amesema mkandarasi huyo mpya atakamilisha ujenzi wa mradi huo ndani ya siku 60 kwa gharama ya Sh bilioni 2.1.
“Kazi ambayo atakamilisha ni jengo la abiria na utawala, kufunga taa 80 kwenye eneo la stendi na barabara ya kilometa 1.8 inayozunguka stendi hiyo hadi eneo la Ikulu ndogo, pia tumemtaka afanye kazi hii usiku na mchana,” amesema Humbe.
Awali, Meneja wa Tarura katika halmashauri hiyo, Mathias Mgolozi ambao ndiyo wasimamizi wa mradi huo, alisema ujenzi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia (IMF) na mkataba wa ufadhili unaisha Desemba 31, mwaka huu na wana uhakika wakandarasi hao watakamilisha ndani ya muda huo.