Na Winfrida Mtoi, Dar es salaam
Homa ya pambano la ngumi la ubingwa wa dunia lililopewa jina la ‘Queen of the Ring’, linalowakutanisha mabondia wa kike, Zulfa Macho na Halima Vunjabei, imezidi kupanda baada ya kila bondia kutamba kuibuka malkia wa taji hilo.
Mzuka wa mabondia hao umepanda baada ya waandaaji wa mchezo huo, leo kutambulisha mkanda unaogombaniwa mbele ya waandishi wa habari.
Pambano hilo la raundi 10, linatarajia kufanyika Jumapili hii Aprili 11, 2021 kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es salaam huku kukiwa na mapambano kibao ya utangulizi ya wanaume na wanawake.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika Gym ya City Mall, Dar es Salaam, mabondia hao, wametamba kuwa hakuna maneno mengi zaidi ya kutwangana ulingoni.
“Pambano hili halijawahi kutokea Tanzania, naomba uzima nifike siku ya mchezo, napenda kuwaahidi Watanzania na mashabiki wangu kuwa mkanda huu utabaki kwa Halima Vunjabei kutokana na mazoezi niliyofanya,” amesema bondia Halima.
Kwa upande wake Zulfa, amesema kutokana na maandalizi yake ya miezi kadhaa, yanatosha kabisha kuondoka na taji hilo na anaamini watu wake wanahitaji ushindi.
Mratibu wa pambano hilo, Kapteni Selemani, Semunyu, amesema maandalizi yanaendelea vizuri na mchezo huo utakuwa na mvuto mkubwa kutokana na aina ya mabondia wanaopigana.
“Peaktime tumeamua kulifanya pambano hili la kipekee na tumeweka kiingilio cha kuanzia h. 10,000 ili kila mmoja ajitokeze kuja kuwasapoti wanawake hawa wenye vipaji vya juu,” amesema Kapteni Semunyu.