24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mjue Mtunzi; Upande wa pili wa Watunzi wa Riwaya nchini

Na Joseph Shaluwa

SANAA ya filamu na muziki wa kizazi kipya ni miongoni mwa sanaa zenye nguvu na zinazojulikana na wengi zaidi hapa nchini. Ukimtaja Ali Kiba, Diamond, Ray, Jux, Zuchu, JB, Kajala, Wolper na majina kama hayo yanajulikana kwa kasi zaidi.

Lakini kuna upande wa pili wa utanzu wa Fasihi Andishi, ambapo humu kuna vichwa vingi vinavyofanya vema kwenye medali hiyo. Isivyo bahati thamani na heshima yao haikuzwi au haiwekwi kwenye mzani unaotakiwa katika jamii.

Joseph Shaluwa.

Kwa uchache ukiambiwa utaje majina ya watunzi wa riwaya wa kizazi cha sasa, huwezi kuacha majina kama David Shalali, Hafidh Kido, Wilbard Makene, Hussein Molito, Hassan Ally, Hassan Mboneche na  Joseph Shaluwa.

Hawa ni baadhi tu ya watunzi wa kizazi cha sasa ambao wapo kwenye Umoja wa Riwaya Wenye Dira Tanzania (UWARIDI), umoja ambao upo chini ya Rais wake, Hussein Tuwa ‘Bingwa wa Taharuki’.

Katika kutafuta thamani yao kama waandishi ndipo UWARIDI ikabuni Tamasha la Mjue Mtunzi, ambalo lengo lake hasa ni kuwakutanisha wasomaji na watunzi wao (fanani na hadhira).

MJUE MTUNZI kwa mara ya kwanza lilifanyika Februari 23, 2020 katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule ya Sayansi na Teknolojia, Sayansi – Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

Washiriki wa Mjue Mtunzi Msimu wa kwanza.

Huu ni msimu wa pili, ambapo mwaka jana lilipumzishwa kwa sababu ya janga la ugonjwa wa UVIKO 19. Katika tamasha la mwaka huu, litafanyika Julai 3, 2022, siku ya Jumapili katika Ukumbi wa NSSF – MAFAO HOUSE, Ilala – Boma jijini Dar es Salaam.

Mgeni rasmi ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Profesa Adolph Mkenda, huku MC akiwa ni mkongwe Taji Liundi. Mdhamini mkuu ni Elite BookStore, muuzaji mkubwa wa vitabu nchini Tanzania.

Katibu Mwenezi wa UWARIDI, Maundu Mwingizi amezungumza nami na kunieleza mambo kadhaa kuhusiana na tamasha hilo kwa mwaka huu.

UWARIDI NI NINI?

“Ni Umoja wa Waandishi wa Riwaya Wenye Dira Tanzania – UWARIDI. Tunaongozwa na Hussein Tuwa kama Rais wetu, Katibu Mkuu Ibrahim Gama, Katibu Mwenezi ni mimi – Maundu Mwingizi na Mhazini, Lilian Mbaga. Lakini pia tunaye mjumbe wa Kamati Kuu, ndugu Fadhy Mtanga.

“Ni umoja unaosimamiwa na wanachama wenyewe. Unawasaidia watunzi kujitambua, kutambulika na kuthaminiwa katika jamii ya wasoma vitabu. Mfano mzuri ni hili tamasha letu la Mjue Mtunzi. Kwa hakika linatuheshimisha watunzi.”

UNAZUNGUMZIAJE TAMASHA LA MJUE MTUNZI?

“Naishiwa maneno lakini niseme, linazidi kupanda hadhi mwaka hadi mwaka. Angalia… ni mwaka wa pili huu tunafanya, lakini kuna hatua kubwa tumepiga.

“Kwanza mgeni rasmi ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Adolph Mkenda, MC wetu mwaka huu ni wa viwango vya juu zaidi, mkongwe Taji Liundi lakini pia hata ukumbi wetu – ni wa hadhi ya juu zaidi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Profesa Adolf Mkenda.

“Ni full kiyoyozi, nawashauri watu waje na makoti yao, maana siyo kwa ubaridi ule! Mwenyewe nimeshakwenda mpaka pale NSSF na nimeshuhudia ‘mufindi’ ulipo mle ndani. Ni tamasha zuri, la kistaarabu.

“Lakini hata mdhamini wetu ni mkubwa na ni mdau wa vitabu nchini. Tumedhaminiwa na Elite BookStore. Kwahiyo unaweza kuona ni kwa namna gani ni tamasha lenye hadhi ya juu.”

WATU WATARAJIE NINI KWENYE TAMASHA HILO?

“Kwanza dhamira kubwa ni kuwakutanisha na watunzi wao. Kutakuwa na watunzi watatu watakaokaa kwenye kiti cha MJUE MTUNZI siku hiyo, ambao wataelezea maisha yao na baadaye watajibu maswali ya mashabiki wao.

“Kama mtakumbuka mwaka 2020, walikuwa ni Hussein Tuwa, Lilian Mbaga na Lelo Mmasy. Kwa kawaida huwa watunzi wawili wanatoka ndani ya Uwaridi na mmoja nje ya Uwaridi. 

“Mwaka huu kuna bonge la surprise. Watu waje watawaona watunzi wao. Pia kuna matukio ya kupiga picha kwenye zulia jekundu, lakini pia huwa kuna soko kubwa la vitabu siku hiyo. Kutakuwa na meza nyingi za wauza vitabu ambao wamekubaliwa kufanya hivyo na uongozi, hivyo basi andaa tu pesa yako ya vitabu,” anasema.

Hussein Tuwa

WANAOZUNDUA VITABU 

“Katika msimu uliopita, walizindua watunzi wawili tu – Joseph Shaluwa (CHOTARA) na Fadhy Mtanga (RAFU). Mwaka huu mambo ni moto zaidi, kwani watazindua watunzi; Hassan Mboneche (WARAKA), Wilbard Makene (KABRASHA LA RAIS), Hussein Molito (CHAWA),  Hassan Ally (KWAHERI), Hafidh Kido (HAWARA),  David Shalali (SALOME WA SADAKA) na Joseph Shaluwa (HILIKI YA TUNU).

WASOMAJI WANAWAFIKIAJE?

“Tunapatikana kwenye pages zetu kwenye Facebook @Mjue Mtunzi,  na Instagram @MjueMtunzi na Twitter @MjueMtunzi. 

VITABU VITAKAVYOZINDULIWA VITAPATIKANA WAPI?

“Kwanza siku ya uzinduzi palepale ukumbini, utapata vitabu hivyo na saini kabisa za waandishi wenyewe, lakini baadaye vitaanza kuuzwa katika maduka mbalimbali hasa maduka yetu washirika ya Kona ya Riwaya – Kinondoni Block 41, Come & Read BookStore – Ununio na Kwa George – Posta Mpya. 

“Sehemu nyingine ni maduka ya Elite BookStore, Creative Ideas, Kariakoo karibu na Jengo la Toyota. Mikoani utaratibu utawekwa baadaye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles