26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

MJANE WA KOMBA ALILIA MAFAO YA MUMEWE CCM

Na PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM


MJANE wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi, marehemu Kepteni John Komba, Salome Komba, amejitokeza hadharani na kumwomba Rais Dk. John Magufuli, kumsaidia  ili aweze kulipwa mirathi ya mume wake Sh milioni 75.

Komba ambaye alikuwa Muhamasishaji na Mkurugenzi wa Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT), inayomilikiwa na CCM alifariki dunia mwaka juzi katika Hospitali ya TMJ baada ya kufikishwa hospitalini hapo kwa matibabu.

Akizungumza na na kituo cha Redio cha Times FM  cha jijini Dar es Salaam  kupitia kipindi cha Maisha Mseto, Salome alisema fedha hizo ni mirathi inayotokana na bendi ya TOT ambayo mumewe alikua mkurugenzi wake tangu alipokuwa kada wa chama hicho hadi alipofariki mwaka 2015.

Alisema mara baada ya mumewe kufariki, aliweza kufuatilia mirathi hiyo ambayo mpaka sasa amelipwa Sh milioni 4.5 badala ya Sh milioni 75,  ambapo hadi sasa familia bado inadai kiasi hicho cha fedha.

Alisema kutokana na hali hiyo, aliweza kuzungumza na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na kumweleza kama anadai fedha hizo na amelipwa Sh milioni 4.5 tu.

“Namwomba Rais John Magufuli ambaye pia  ni Mwenyekiti wa CCM, kunisaidia kupata mirathi ya mume wangu ambayo ni sh milioni 75 ninazodai kwa sababu waliweza kunilipa sh milioni 4.5,” alisema Salome.

Alisema marehemu kabla ya kufariki alikuwa anaipenda CCM na kabla alidiriki kuhamasisha wasanii wenzake kuhusiana na kampeni.

Alisema kutokana na hali hiyo, alimwomba Rais kumsaidia suala hilo kwa sababu ni jasho la mumewe  na ni haki yake kwa kazi alizozifanya wakati wa uhai wake na kwa jinsi alivyoweza kujitoa ndani ya chama hicho na kwamba mpaka anafariki alikuwa mwana CCM.

Katika hatua nyingine, Salome alisema kuwa ameamua kugawa bure nakala za vitabu vinavyoelezea maisha ya marehemu mumewe kwa sababu Watanzania hawana utaratibu wa kujisomea.

Kutokana na madai hayo MTANZANIA ilimtafuta Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rodrick Mpogolo alikiri bendi hiyo kumilikiwa na chama hicho tawala huku akimtaka mwandishi kuwasiliana na mkurugenzi wa bendi hiyo kuhusu madai ya fedha za mirathi za mjane huyo.

Alisema kutokana na hali hiyo, hawezi kusema chochote kwa sababu suala hilo halihusiani na masuala ya kisera ndani ya chama, bali yanahusiana na fedha, hivyo ni vema  uongozi wa TOT ukakaa na kuliangalia suala hilo na kutoa taarifa.

“TOT ni bendi inayojitegemea ambayo ina uongozi wake akiwamo mkurugenzi, hivyo ni vema wenyewe wangelizungumzia suala hilo kuliko chama kwa sababu si suala la kisera bali ni suala linalohusu fedha na malipo,”alisema Mpogolo.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kutokana na hali hiyo, chama hakitakuwa na majibu ya moja kwa moja kwanini hajalipwa hadi leo bila ya kufuatilia suala hilo kutoka uongozi wa TOT.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles