THERESIA GASPER NA GLORY MLAY
MLIMBWENDE atakayeibuka mshindi kwenye shindano la Miss Sinza litakalofanyika Julai 29, Ukumbi wa Denfrance Sinza, Dar es Salaam, ataondoka na kitita cha Sh 500,000.
Mratibu wa shindano hilo, Nasib Mhinya, alisema mshindi wa pili atapata Sh 400,000 na wa tatu ataondoka na Sh 300,000 huku mshindi wa nne na watano wakipata kifuta jasho cha Sh 200,000 kila mmoja na warembo wengine watapata kifuta jasho cha Sh 100,000 kila mmoja.
Warembo hao jana walitembelea ofisi ya New Habari (2006) Ltd iliyopo Sinza Kijiweni na kujifunza mambo mengi yanayofanywa hapo kuanzia upataji wa habari hadi uchapishaji wake.
Wakati huo huo, warembo hao walitembelea Hospitali ya Palestina na kutoa zawadi mbalimbali zikiwamo sabuni kwa mama wajawazito na wenye watoto wachanga.
Akizungumza na Gazeti hili, Ofisa Uongozi wa Hospitali hiyo, Joyce Magile, alishukuru warembo hao kwa kujitolea kwao hospitalini hapo.
“Tunashukuru sana kwa zawadi hizi mlizozitoa katika wodi hizi za wazazi wakiwemo wajawazito na wale wenye watoto wachanga na tunaomba msiishie hapa na mfanye na kwengine,” alieleza.