33.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mishahara hewa yatafuna mil 500/- Pwani

Mhandisi Evarist NdikiloNA GUSTAPHU HAULE, PWANI

SERIKALI mkoani Pwani imepata hasara ya Sh milioni 534 kwa kuwalipa watumishi hewa 150 waliopatikana, baada ya kufanya uchunguzi wa kina kupitia halmashauri mbalimbali mkoani hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, alisema pamoja na kubaini idadi hiyo, bado kazi ya uhakiki inaendelea.

Alisema katika idadi hiyo, watumishi 28 walihakikiwa na sasa wanalipwa mishahara yao kama kawaida, huku watumishi 70 wamesimamishiwa mishahara yao kwa sababu ya utoro kazini, wakati watumishi 34 walishastaafu, lakini wameendelea kulipwa.

Ndikilo alisema hadi sasa Sh milioni 242.7 zimerudishwa Hazina na watoro waliobainika wamelipwa milioni 366.

“Mkoa wa Pwani tumepata hasara ya Sh milioni 534 kutoka kwa watumishi hewa 150, tunaendelea kufuatilia ili kujua nani alikuwa anapokea fedha hizi, na kama mkurugenzi au mweka hazina wa halmashauri husika alikuwa anachukua, kibarua chake kitakuwa kimeisha hapo,” alisema Ndikilo.

Alisema Serikali ya Mkoa wa Pwani imekabidhi majukumu hayo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili wachunguze kwa kina mhusika aliyehusika kupokea.

“Inashangaza kuona yupo mtumishi ambaye ni mwalimu anapokea mshahara tangu mwaka 2006, lakini hafanyi kazi yoyote, na leo hii anajitokeza katika kuhakiki na kusema kuwa yeye ni mtumishi halali, jambo hili halivumiliki hata kidogo,” alisema.

Hata hivyo, aliwatahadharisha viongozi, watendaji wa halmashauri wakiwamo wakurugenzi kuwa endapo watabainika kufanya ujanja wa kutafuna fedha za watumishi hewa, hatua kali zitachukuliwa ikiwamo ya kufikishwa mahakamani mara moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles