27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Majambazi yaua watu wanne Tanga

Kamanda wa Polisi Mkoa wa TangaNA AMINA OMARI, TANGA

WATU wanaodaiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za moto, wamewaua watu wanne na kujeruhi wengine  wawili  katika tukio la uporaji mkoani Tanga.

Majambazi hao, wakiwa na bunduki aina Sub Machine Gun (SMG) na bastola, walivamia duka la mfanyabiashara Hamoud Ali lililopo Mtaa wa Swahili jijini hapa juzi saa moja usiku na kupora Sh milioni 2.7.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paul, alisema majambazi hao waliingia dukani kama wateja.

Alisema baada ya kuingia dukani, ghafla walitoa bunduki aina ya SMG na bastola, kisha kuamuru watu wote waliokuwano ndani walale chini.

“Wakati biashara inaendelea, waliingilia kama wateja, ghafla walibadilika na kutoa silaha na kupiga risasi watu wanne ambao walifariki dunia papo hapo. Risasi nyingi ziliwapata sehemu za vichwani,” alisema Kamanda Paul.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Ahmed John, Vitus Manfred ambaye ni dereva wa Mahakama ya Wilaya ya Tanga, Athumani Seya na Ali Mpemba ambaye ni mfanyakazi wa duka hilo.

Kamanda Paul aliwataja majeruhi kuwa ni Wilson Msikizi na Hamis Mkonga ambao walijeruhiwa vibaya na kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Alisema hadi sasa jeshi hilo halijafanikiwa kukamata mtu hata moja na kuwaomba wananchi wasaidie kutoa taarifa.
Kutokana na hali hiyo, Kamanda Paul alitangaza donge nono kwa mwananchi atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa majambazi hao.

Walioshuhudia tukio hilo, walililaumu Jeshi la Polisi kwa kuchelewa kufika eneo la tukio na kusababisha majambazi kuondoka kirahisi.

Mmoja wa mashuhuda hao, Juma Hamidu, alisema kama polisi wangefika mapema, wangeweza kuwakamata kutokana na eneo hilo kuwa wazi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbaruk, alivitaka vyombo vya ulinzi viwe na vifaa vya kisasa ili kukabiliana na matukio ya uhalifu pindi yanapotokea.

“Hili ni tukio la tatu la uporaji wa fedha katika Jiji la Tanga kutokea katika siku za karibuni, hadi sasa hakuna taarifa zozote zilizoelezwa kama kuna wahalifu wamekamatwa, hali hii isipodhibitiwa haraka wananchi wanaweza kuingiwa na hofu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles