NA KULWA MZEE -MOROGORO
NAIBU Msajili wa Mahakama Kuu, Augustino Rwizile, amesema msamaha unaotolewa na rais kwa mfungwa, unahusu adhabu tu na si amri nyingine zilizotolewa na mahakama wakati wa hukumu, ikiwamo kulipa fidia.
Hayo yalibainishwa jana ikiwa ni siku ya tatu ya mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari za mahakamani, yaliyoandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na kufadhiliwa na Benki ya Dunia.
‘’Mtu anapohukumiwa kwenda jela na kutakiwa kulipa fidia, ikatokea akapata msamaha wa rais akatoka jela, kinachosamehewa hapo ni adhabu, lakini amri nyingine zinaendelea kwa utekelezaji.
‘’Fidia aliyoamuliwa kuilipa anatakiwa kuilipa, na njia rahisi fidia ilipwe kwanza baada ya adhabu kutolewa, inayoweza kubatilisha adhabu na amri hizo ni Mahakama ya Rufaa baada ya rufaa kuwasilishwa na mrufani akashinda, maamuzi ya kubatilisha yakatolewa,” alisema Rwizile.
Alisema mtuhumiwa anapofanya kosa la jinai, akamwathiri mtu mwingine, hukumu ikitolewa akatiwa hatiani, anaamuliwa kulipa fidia kwani hilo ni takwa la kikatiba.
Pia alisema katiba inaelekeza watoa haki wasifungwe kupita kiasi na makosa ya kiufundi japo kanuni nyingine zinaelekeza huo utaratibu.
“Kuitupa kesi kwa sababu ya makosa ya kiufundi ni kukiuka katiba. Katiba inakataza isipokuwa kanuni nyingine zina huo utaratibu,” alisema.
Akizungumzia dhana ya kutenda haki kwa wakati, Rwizile alisema inakwazwa na kuwepo kwa idadi ndogo ya majaji wa Mahakama Kuu.
“Majaji wa Mahakama Kuu wanatakiwa wasipungue 30, sasa hivi waliopo ni majaji 69, lakini mahitaji ya Mahakama Kuu ni majaji 120, namba ya majaji ni ndogo,” alisema.