Derick Milton, Simiyu
AGOSTI 8, 2019 ilikuwa ni mwisho wa Maonesho ya Siku Kuu ya Wakulima Kitaifa (Nanenane) yaliyokuwa yanafanyika katika Viwanja vya Nyakabindi, nje kidogo ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.
Maonesho hayo yalihitimishwa rasmi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akimwakilisha Rais Dk. John Magufuli, ambapo yalifunguliwa Agosti Mosi na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Maonesho hayo ya 27, yanatajwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kutoka hapa nchini, kutokana na kuhudhuriwa na wananchi wengi pamoja na washiriki zaidi ya 400 kutoka serikalini na taasisi binafsi.
Ukubwa wa maonesho hayo unatokana na serikali ambayo kupitia Wizara ya Kilimo ilizindua programu tano zinazolenga kukifanya kilimo kiwe cha kisasa, kibiashara zaidi ili kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya viwanda mwaka 2025.
Lengo ni kumbadilisha mkulima aweze kulima kibiashara zaidi.
Waziri Hasunga anasema programu hizo zimejikita katika kumsaidia mkulima kulima kisasa kwa kutumia kanuni bora za kilimo, kuongeza tija mazao yake, pamoja na upatikanaji wa soko la uhakika.
Programu hizo zilizozinduliwa ni pamoja na mkakati wa kitaifa wa usimamizi upotevu wa mazao baada ya kuvunwa, bima ya mazao kwa wakulima, pamoja na mifumo mitatu ya kieletroniki inayolenga kuboresha na kurahisisha ufanyaji wa biashara za bidhaa zitokanazo na kilimo nchini.
Mifumo hiyo ni pamoja na ile ya kuomba vibali vya kuingiza na kuuza mazao nje ya nchi, leseni na usajili (Agricultural Trade Management Information Syatem – ATMIS), mfumo wa soko la bidhaa la kieletroniki (Tanzania Mercantile Exchange – TMX) pamoja na mfumo mwingine ni ule wa usajili wa wakulima nchini.
Mkakati bima ya mazao
Mkakati huu ulizinduliwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, utakaokuwa chini ya utekelezaji wa Shirika la Bima ya Taifa (NIC) ambapo utaanza na mazao mawili ya kibishara; pamba na kahawa.
Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Dk. Elirehema Doriye, anasema bima hiyo itawasaidia wakulima katika magonjwa, ukame, wanyama vamizi wa mazao na mafuriko.
Dk. Doriye anasema bima hiyo pia itamkomboa mkulima kutoka katika kilimo kizamani kwenda cha kisasa bila ya kuwa na hofu ya kupoteza mtaji alioweka shambani ikiwa pamoja na kupata mkopo katika benki za kibiashara na kilimo.
Waziri Hasunga anasema uzinduzi wa bima ya mazao ni mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo kwani itawasaidia wakulima wakati wa majanga mbalimbali yanayowakabili kwa sasa.
“Nilipoteuliwa katika wizara hii nilijiwekea malengo, mojawapo ni kuwa na Bima ya Kilimo, nimefurahi kwamba Shirika la Bima la Taifa limekuwa la kwanza kutekeleza.
“Mmeanza na zao la pamba katika Mkoa wa Simiyu na mtaenda kwenye kahawa Kagera ni jambo zuri, lakini nataka ifikapo mwakani muwe mmeshayafikia mazao yasiyopungua matano ya kibiashara ili wakulima wawe na uhakika wa uwekezaji katika kilimo,” anasema Hasunga.
Waziri Hasunga anasema wakulima watanufaika na aina tatu ya bima, bima mseto – inahusika na mazao yatakayoathiriwa na ukame, upepo mkali, wadudu, moto, radi, barafu, mafuriko na tetemeko.
“Bima ya pili ni hali ya hewa, ambayo itahusika na ukame na mvua zilizozidi na ya tatu ni bima ya maeneo maalumu, hii inahusika na upungufu wa mazao, yaani mkulima alitarajia kupata magunia kadhaa lakini kutokana na hali ya hewa akavuna pungufu, bima hii itamuhusu,” anasema.
Mfumo wa usajili wa wakulima
Mfumo huu ulizinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akifunga maonesho hayo Agosti 8, mwaka huu, ambapo lengo la mfumo huo ni kujulikana idadi halisi ya wakulima nchini ili serikali iweze kuwahudumia vizuri.
Akitoa maelezo ya mfumo huu, Hasunga anasema kupitia usajili wa kieletroniki, wakulima wote wanasajiliwa kulingana na mazao wanayozalisha ikiwa pamoja na eneo la kilimo.
Anaeleza kuwa mfumo huo utaiwezesha serikali kutambua wakulima gani wanahitaji nini, wanalima nini? Wanalima maeneo yenye ukubwa gani, changamoto zao na wanaweza kusaidiwa nini kwa wakati gani?
“Wizara tunataka kujua tunao wakulima wangapi na wanalima nini na eneo lenye ukubwa gani, hii itatusaidia hata kuweka mikakati ya kiutendaji ndani ya wizara, lakini hata katika bajeti ili kuhakikisha wote tunatatua changamoto zao,” anasema Hasunga.
“Tunataka pia mtu yeyote aliyeko nje na ndani ya nchi akitaka kujua Tanzania kuna wakulima wangapi, katika pamba wangapi? kahawa, korosho wangapi, ajue na eweze kupata hizo takwimu kwa urahisi,” anaeleza Hasunga.
Kuzuia upotevu wa mazao wakati wa mavuno
Mkakati huu uliozinduliwa na Makamu wa Rais unalenga kupunguza upotevu wa mazao wakati wa mavuno hadi kuhifadhiwa kwa asilimia 50.
Kwa mujibu wa takwimu za hali ya kilimo zilizotolewa na Hasunga, mazao ya chakula hupotea baada ya kuvunwa kwa asilimia 25 hadi 40.
Takwimu hizo ambazo zimetolewa na Shirika la Chakula Duniani (FAO), na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) zinaonyesha mazao ya nyanya hupotea kwa asilimia 20 hadi 50 na magimbi asilimia 10 hadi 60.
Mazao mengine ni ndizi asilimia 20 hadi 80, papai asilimia 40 hadi 100 na mazao ya mizizi ni asilimia 12 hadi 27, matunda na mboga mboga asilimia 18 hadi 32, mahindi 15.5 na mtama asilimia 12.5.
Sababu kubwa zinazotajwa na watalaamu wa kilimo zinazomfanya mkulima apoteze mazao mengi wakati wa kuvuna ni ukosefu wa elimu ya jinsi gani anaweza kuvuna vizuri mazao yake kulingana na mazigira aliyonayo.
Mbali na hilo, sababu nyingine ni kutokuwapo kwa miundombinu rafiki wakati wa usafirishaji mazao kwenda kuhifadhi, kutokuwa na sehemu sahihi za kuhifadhi chakula, ukosefu wa masoko pamoja na kutokujua kuongeza dhamani baadhi ya mazao.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usalama wa Chakula kutoka Wizara ya Kilimo, Josephine Amolo, anasema mkakati huo utatekelezwa kwa muda wa miaka 10 kuanzia mwaka huu hadi 2029.
Anasema kupitia malengo tisa ya mkakati huo, mkulima atafikiwa popote alipo kijijini, kupitia kwa maafisa ugani na kilimo ambao watapewa elimu na mafunzo ya jinsi gani watamwezesha mkulima kupunguza upotevu wa mazao yake.
“Mkakati unalenga zaidi katika kutoa elimu kwa wakulima, maafisa ugani na kilimo, kutengeneza teknolojia rahisi kulingana na mazingira ya wakulima waliopo ili waweze kuzitumia katika kupunguza upotevu huo wa mazao.
“Tunataka kuwaelimisha wakulima jinsi gani wanatakiwa kuvuna mazao yao bila ya kupotea, kama ni mchele, viazi, matunda wataweza vipi kuvuna kitalaamu kwa kutumia teknologia ambazo wanazo uko vijijini,” anasema Amolo.
Mfumo soko la bidhaa kieletroniki
Wizara ya Kilimo inasema changamoto za masoko, kuhangaika na bei katika mazao ya biashara kama pamba, kahawa, tumbaku na korosho, mwarobaini wake ni mfumo wa Tanzania Mercantile Exchange – TMX.
Mfumo huu uliozinduliwa na Majaliwa, unalenga kufuta changamoto kubwa ya wakulima hapa nchini katika kutafuta masoko ya kitaifa na kimataifa.
Waziri Hasunga anasema kupitia mfumo huo, Tanzania itaweza kuuza mazao yake katika masoko makubwa yote duniani, hasa mazao matano ya kimkakati ya kibishara.
Anasema kupitia mfumo huo dunia itajua kuwa Tanzania kwa wakati gani imezalisha nini na kwa kiwango gani na zao hilo lina ubora wa kiasi gani hivyo, itamsadia mfanyabishara popote alipo kununua bidhaa husika.
“Kwa mfumo huu tutaweza kuitangazia dunia kuwa tumezalisha korosho kiasi fulani zenye ubora fulani na zinapatikana katika mikoa fulani katika maghala haya, mfumo huu utatusaidia kupata soko zuri duniani,” anasema Hasunga.
Aidha, anaeleza kuwa kupitia mfumo huo itapunguza madalali ambao wamekuwa wakisababisha kujulikana kwa bei halisi katika soko la dunia, ambapo bidhaa itatangazwa moja kwa moja katika soko la dunia.
“Katika biashara kuna mambo mengi, wapo watu wanajiita madalali wamekuwa wakisababisha tusipate bei halisi ya mazao ya wakulima wetu, sasa hii inaenda kukomesha, tunataka Tanzania tutambulike kidunia kuwa tunazalisha mazao kadhaa,” anasema Hasunga.
Mfumo kuomba vibali kuingiza na kuuza mazao nje ya nchi
Kwa muda mrefu, wafanyabiashara wa mazao ya wakulima kutoka ndani na nje ya nchi wamekuwa wakitumia mfumo wa kuandika barua za maombi ili wapatiwe vibali, leseni na usajili kwa ajili ya kuuza mazao nje ya nchi.
Licha ya kuandika barua, bado kumekuwapo mzunguko mrefu kwa mfanyabiashara huyo kutakiwa kusafiri kwa ajili ya kupeleka barua hiyo ambayo mzunguko wake unakuwa mrefu hadi kupatikana vibali hivyo.
Watalaamu wa uchumi wanasema katika dunia ya sasa ya Sayansi na Tekonolojia, ambayo mtu anaweza kufanya biashara kupitia mtandao huku akiwa amelala nyumbani, mfumo huo unarudisha nyuma kilimo chetu.
Kuendelea kutumia mfumo huo wa zamani, hakuwezi kumkomboa mkulima na kusaidia kubadilisha kilimo kiwe cha kibiashara, na badala yake mkulima ataendelea kubaki maskini huku akitumia nguvu kubwa katika uzalishaji.
Waziri Hasunga anasema mfumo huo utamsaidia mtu yeyote anayetaka kufanya biashara ya mazao ya kilimo popote alipo aweze kutuma maombi ya kupata kibali, lesni au sajili na akafanikiwa kupata kwa muda mfupi kupitia mtandao.
“Mfanyabishara hatalazimika tena kusafiri umbali mrefu na badala yake atatumia mtandao kukamilisha mahitaji yake yote yanayotakiwa katika kuingiza na kuuza mazao nje ya nchi,” anasema Hasunga.
Anabainisha kuwa wizara yake imepania kuhakikisha kilimo nchini kinabadilika kinakuwa cha kisasa na kibiashara na kuweza kuwakomboa wakulima kutoka katika umaskini.