30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, March 26, 2023

Contact us: [email protected]

Hasunga: Benki ziwafikie wakulima vijijini ili kujenga uchumi imara

Grace Shitundu, aliyekuwa Simiyu

MAONESHO ya Nanenane kitaifa  yamemalizika wiki hii katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Katika maonyesho hayo taasisi mbalimbali zilishiriki zikiwamo za kifedha.

Miongoni mwa masuala yaliyozungumzwa na kushauriwa kwa nyakati tofauti, ni taasisi hizo kuhakikisha wakulima wanajiunga na mfumo wa kifedha kwa kuwa na akaunti katika benki mbalimbali.

Alipotembelea banda la Benki ya NMB, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, aliwataka kuhakikisha wanawafikia wakulima wadogo walioko vijijini ili kuleta tija katika kilimo.

Anasema kilimo ndio nguzo ya uchumi wa nchi na katika kuelekea uchumi wa viwanda ni lazima kilimo kiimarishwe hivyo, unahitajika uwekezaji wa kutosha.

“Tukiimarisha kilimo tutapata malighafi za viwanda, kwa sababu viwanda vyote tunavyovisema asilimia 60 malighafi yake inatokana na mazao.

“Tumeona ni lazima twende katika uchakataji, na benki kama NMB tunaitegema kutuunga mkono ujenzi wa viwanda na kuhakikisha tunaongeza thamani ya mazao yetu,”anasema.

Anasema kama wanataka kuondoa umaskini ni lazima wananchi wawe katika mfumo jumuishi, lakini kasoro iliyopo walio na akaunti benki ni wachache.

“Benki zijitahidi kufikia wakulima wote wadogo hasa walioko vijijini na watoe elimu ili asilimia 90 ya wakulima wawe katika mfumo wa fedha, itakuwa ni rahisi kujenga uchumi imara.

“Ni vizuri benki zikiendelea kuunga mkono kilimo kuanzia katika uzalishaji, kuongeza thamani, kuwaunga na masoko mazuri lakini pia katika ujenzi wa viwanda.

Hasunga anasema wakulima wa pamba ni wengi lakini asilimia 99 hawana akaunti benki hivyo, kuhakikisha wakulima wote wa pamba kulipwa kupitia benki.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, anasema Simiyu pekee inalima pamba kwa asilimia 55 hivyo, hakuna haja ya wakulima hao kutokuwa na akaunti.

“Yaani una watu 385,000 wanalima pamba, halafu wenye akaunti ni watu 15,000 hata benki akifunga bure ni lazima atapata faida kwa sababu fedha za pamba zitakapolipwa zitapita huko, atauza ng’ombe, kuku, huko kote atapata fedha na akiwa amepewa elimu ya kutosha ataweka benki.

Pia anaitaka benki ya NMB kuangalia namna ya kuwasaidia wakulima wanaojiunga na vikundi.

Anasema kukiwa na vikundi na wakawa na akaunti ni rahisi wao kukopa na kuendeleza shughuli zao za kilimo, ufugaji au uvuvi.

Anasema lakini ni vyema vikundi hivyo vikakopeshwa mashine au teknolojia badala ya fedha taslimu.

“Vikundi vingi vinapokuwa havina fedha huwa na ushirikiano mzuri lakini wakishapata fedha iwe hata milioni 10 vita inaanza hivyo, ni vyema kuwakopesha mashine,” anasema Mtaka.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, anaitaka benki ya NMB kuhakikisha wakulima wanakuwa na akaunti.

Anasema fursa hiyo ni kubwa kwani kwa mikoa ya Mara na Simiyu tu wana watu wapatao 350,000 wanaohitaji kujiunga na benki ili sekta ya kilimo iweze kusonga mbele.

Anasema kuna fursa kubwa katika kilimo kwani huko ndio kwenye watu wengi, na hivyo wasibabaishwa na maneno kwamba katika kilimo kuna hasara.

“Kilimo sasa hakina hasara, tayari Shirika la Bima limeweka bima ya mazao kwahiyo unapowekeza huko unakuwa na uhakika wa kupata faida.

Mkuu wa Kilimo Biashara wa NMB, Isack Masusu, anasema benki hiyo ina matawi 229 na tayari imeshawafikia wakulima moja kwa moja.

“Kuna maafisa wa benki walioelimishwa kuhusu kilimo na namna ya kuwahudumia wakulima,” anasema Masusu.

Anasema NMB ni wadau wakubwa wa kilimo nchini, wanafanya kazi  nyingi na wakulima wadogo, wa kati, wakubwa na wadau wote wanafanya kazi katika mnyororo wa thamani, wakiwamo wale wanaofanya biashara za mazao, wanaochakata na wale wanaouza na kuingiza mazao nje ya nchi.

Anasema pia wanafanyakazi ya kuwezesha uwekezaji katika viwanda vinavyoweza kuchakata na kuongezea thamani mazao ya wakulima.

Masusu anasema wanatoa huduma mbalimbali ikiwamo kumpeleka mteja  benki ili aweze  kujua benki inaweza kusaidia nini katika huduma za fedha.

“Mara nyingi tunafungua akaunti za wateja wa aina zote, wakulima wadogo, wafanyabiashara ndogondogo, kampuni na hata taasisi za serikali.

“Pia huduma ya mikopo yote ya biashara ya kununua na kuuza na kutoa mikopo ya muda mrefu kwa ajili ya kuwekeza katika kilimo.

Anaongeza: “Unaweza kuwekeza katika kilimo kwa kupanua shamba lako, kununua mashine kama matrekta, Combine Harvester kwenye zao la mpunga, mashine za kuchakata, kusaga na kukoboa mpunga,”anasema.

Mkuu huyo wa Kilimo Biashara anasema pia wanaweza kupata mashine za kuweka madaraja katika mazao, jambo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likirudisha nyuma soko la mazao nchini, kwa kuonekana hayana viwango vinavyohitajika.

Anasema wanafanya kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha ikiwamo Benki ya Kilimo nchini TADB, TIB na Shirika la Bima la Taifa (NIC) ambalo limezindua bima ya mazao.

Anaeleza kwamba benki yao haichagui mazao ya kusaidia bali ni ya kila aina.

“Sisi hatuchagui, tunawekeza katika kila aina ya zao ambalo tunaona  tunaweza kuwekeza katika mnyororo wa thamani, na hiyo ni kuanzia shambani.

“Tunawaelimisha wakulima kujiunga katika vikundi ili waweze kukopesheka na kuleta tija katika kilimo, kwani hapa nchini huwezi ukazungumzia biashara yoyote pasipo kutaja kilimo, kuna wafugaji, wakulima na wavuvi wanaosababisha biashara kuendelea,”anasema Masusu.

Anaongeza: “Kama sisi tunataka kwenda hatua nyingine, ni lazima tuwa na ushirika utakaosaidia kuzalisha mazao yenye ubora, kuvutia wanunuzi waweze kuja kununua.

“Kuna wakati mnunuzi anaweza kuja kununua akashindwa kurudi kwa sababu kinakuwa hakipo tena.

Anasema Benki ya NMB itaendelea kuunga mkono sekta ya kilimo kwa sababu ndiko walipo Watanzania wengi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,195FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles