NAIROBI, KENYA
MWANAHARAKATI wa upinzani nchini Kenya, Miguna Miguna, amedai maafisa wa polisi wamemfungia katika choo kichafu na kumnyima haki za msingi za mawasiliano, dawa, chakula na maji kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Jomo Kenyatta (JKIA).
Tofauti na matarajio ya wengi kuwa Miguna angerejea hapa bila kusumbuliwa amekumbana na masaibu tele uwanjani hapo tangu awasili Jumatatu jioni.
Katika tarifa yake jana, Dk. Miguna alisema polisi wamemfungia ndani ya choo kichafu na kidogo bila kuwapo kwa vitu vya msingi, tuhuma ambazo hata hivyo hazikuweza kuthibitishwa mara moja kwa vile polisi wamezuia wanasheria na waandishi wa habari kumfikia.
“Sijapewa chakula, maji wala dawa mbali ya haki yangu ya kuonana na mwanasheria. Chumba karibu na eneo la kuondokea abiria la terminal 2 hakifai,” alisema.
“Sipati fursa ya kwenda kuoga na sijaoga tangu Jumapili, Machi 25. Choo ninamoshikiliwa hamna maji,” alisema katika taarifa hiyo.
“Kuna maji moto pekee chooni kiasi kwamba nashindwa kunawa uso na kupiga mswaki,” alisema.
Mwanasheria huyo aliyeiburuza Serikali mahakamani, alilaani kuendelea kushikiliwa licha ya kuwa mahakama ilishatoa uamuzi wa kumwachia na kumruhusu kuingia Kenya bila masharti.