24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Migogoro ya kisiasa na dalili za kukosa uvumilivu

mutungiNA DEUS KIBAMBA

KUFUATIA mgogoro wa kisiasa unaoendelea ndani ya Chama Cha Wananchi (CUF), nimepata wasaa wa kutafakari juu ya mgogoro huo na mingine ndani ya vyama vingine vya siasa Tanzania sasa na siku za nyuma huku nikihusisha migogoro hiyo na kushuka kwa kiwango cha uvumilivu wa kisiasa na kuvumiliana katika jamii yetu.

Imenifikirisha jinsi Profesa Lipumba kuandika kwa hiari yake kuomba kujiuzulu kutoka katika nafasi yake ya uenyekiti wa CUF mwaka jana na jinsi ilivyochukua muda kwake kujibiwa kuwa amekubaliwa na Mkutano Mkuu wa chama kuondoka katika nafasi hiyo. Nimetafakari sababu alizozitoa profesa huyo mbobevu wa masuala ya uchumi wakati wa kuondoka na wakati wa kutaka kurejea kwake kitini.

Nimejiuliza jinsi alivyoamua kurejea ofisini kwa ‘nguvu’ na kutumia wafuasi wake kuruka geti na kuingia katika ofisi za CUF kukalia tena kiti cha Mwenyekiti huku walinzi wa chama chake wakipokwa bunduki na silaha nyingine ili wasijibu mapigo ya kuingia kwao ofisini kwa nguvu.

Imenifikirisha pia jinsi Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kilivyokaribia kumeguka vipande vipande mara mbili au tatu siku za nyuma.

Kwanza, nimetafakari sana wakati viongozi vijana wa Chadema wakiongozwa na Profesa Kitila Mkumbo na Zitto Kabwe walivyotofautiana na kambi ya Mwenyekiti Freeman Mbowe kuhusu haja na namna ya kuongoza chama hicho kwa awamu. Nimejikumbusha jinsi kambi ya Mwenyekiti Mbowe ilivyomeguka baadaye baada ya kumpoteza Katibu Mkuu wake na ambaye pia alikuwa pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi, Ukawa baada ya Dk. Wilbroad Slaa kujiuzulu ukatibu Mkuu wa chama mwishoni mwa kampeni za uchaguzi mwaka 2015. Nimetafakari kiasi juu ya visababishi vya kubwaga manyanga kwa Profesa Ibrahimu Lipumba na Dk. Wilbroad Slaa na jinsi zilivyofanana au kutofautiana na sababu zilizowaondoa Zitto na Kitila Chadema.

Mtu unaweza kujiuliza, kwa yale aliyoyafanya Profesa Lipumba na kambi yake ya wafuasi Je, tutegemee kitu kama hicho kutokea Chadema? Kama la, nini kitazuia?

Nimejikumbusha jinsi mgogoro ulivyowahi kuikumba NCCR – Mageuzi wakati wa uongozi wa Augustino Mrema na akina Mabere Marando na jinsi ulivyokigharimu chama hicho hadi kuzaliwa kwa chama cha TLP ambacho Mrema anakiongoza hadi leo. Maswali mengi yamekuja nilipokumbuka jinsi hata NCCR iliyosalia baada ya Mrema kuondoka ilivyokumbwa na Mlolongo wa migogoro hadi kufikia kuathiri ushiriki wa chama hicho katika umoja wa Ukawa na katika uchaguzi mkuu baada ya Makamu Mwenyekiti wa chama kutuhumiwa kusaliti na kufukuzwa chamani.

Kwa mchambuzi wa masuala ya siasa za vyama, hivi nini kinaweza kusababisha Makamu Mwenyekiti wa chama atofautiane na mwenyekiti hadi kujitokeza hadharani kupinga uamuzi wa chama katika kiwango tulichokishuhudia? Je, vikao havikai kukubaliana juu ya masuala ya msingi? Kama vinakaa, Je kwa nini hoja hizi za kutofautiana huwa hazijitokezi katika hatua hiyo?

Kwa fikra duni, mtu unaweza ukasema kutofautiana ni utamaduni wa vyama vya upinzani. Hata hivyo, itakumbukwa kuwa CCM nayo imewahi kukumbwa na migogoro lukuki ikiwamo kupishana kauli na kutofautiana kwa vigogo wake wakuu. Kwa mfano suala la Katibu Mkuu wa zamani, Marehemu Horace Kolimba kusema CCM imepoteza mwelekeo lililosababisha mpasuko mkubwa hadi kumgharimu vibaya mtendaji huyo mstaafu wa chama tawala ambaye aliishia kupoteza maisha yake.

Katika miezi ya karibuni, nimemsikia Katibu Mkuu wa sasa wa CCM Abdulrahman Kinana amejitokeza hadharani akisema viongozi wa Serikali wana tatizo la kutowasikiliza wananchi kauli ambayo imeleta tafsiri tofauti tofauti nchini. Karibuni zaidi, Rais mstaafu na Mwenyekiti za zamani wa CCM Ali Hassan Mwinyi ameripotiwa akisema nchi inakwenda ndivyo sivyo huku gazeti moja likikoleza maneno yake kwa wino mweusi kwa kufananisha nchi yetu na gari bovu.

Haya yote ni mambo yanayoonesha kuwa chama tawala cha CCM pia kimekuwa kikitofautiana vikali katika baadhi ya mambo ya msingi. Lakini Je tofauti ya madhara ya kutofautiana inalingana kati ya chama tawala na upinzani? Naweza kusema hapana!

Kuhusu uvumilivu wa kisiasa, nimegundua dhahiri kuwa kuna kushuka kwa uvumilivu. Kwa mifano michache tu, watu sasa wanasikika wakisema hadharani kuwa mtu aliye na mawazo tofauti katika chama fulani na aondoke akatafute chama kingine. Aidha, kutolewa kwa makatazo ya mikutano ya vyama kama lile la hivi karibuni kuwa siasa sasa basi kwa kuwa uchaguzi umekwisha ni kana kwamba siasa inaishia katika uchaguzi.

Zaidi ya yote, kuzuiwa kwa mikutano ya vyama inayofanyika hadharani na wakati mwingine inayofanyika ndani ya kumbi za mikutano siyo tu dalili ya kutoweka kwa uvumilivu wa kisiasa bali pia ni ishara ya awali ya uvunjifu wa katiba katika ibara ya 18, 21 na nyinginezo.

Sambamba na hilo, kuna kutoweka kwa uvumilivu wa kijamii kumesababisha kushambuliwa na wakati mwingi kuuliwa kwa watuhumiwa wa makosa ya wizi na ukibaka mitaani kwetu pamoja na lile la mauaji ya watafiti wa masuala ya udongo katika Kijiji cha Mvumi, Dodoma kwa hisia kuwa walikuwa ni Mumiani wanaohusishwa na mfanyabiashara mashuhuri kijijini hapo.

Ikumbukwe pia kuwa miongoni mwa wanasiasa, kumekuwa pia na hisia za kutoaminiana hadi kufikia kutuhumiana kuwekeana sumu katika maji, vinywaji au chakula wakiwa katika shughuli za kisiasa. Fikiria jinsi Watanzania walivyoaminishwa kuwa Waziri wa Sasa wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe alikuwa ameugua kutokana na kulishwa sumu.

Kumbuka jinsi tulivyoambiwa kuwa hali katika chama hata kimoja cha Mapinduzi ilikuwa mbaya mpaka baadhi ya wanachama walikuwa wakienda uani na maji ya kunywa ili kuepuka kuwekewa sumu katika vimiminika hivyo endapo wataacha mezani.

Hebu fikiria, hisia zilizojitokeza kuhusu mazingira yaliyosababisha kuuawa kwa Mbunge wa zamani wa Tarime Marehemu Chacha Wangwe na tuhuma za kuhusika kwa vigogo wa Chadema katika maafa hayo. Mwaka jana tu, kulitokea fununu kuwa ajali iliyompata kiongozi wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila haikuwa bure bali ilipangwa na baadhi ya wabaya wake. Mambo haya yote ni ushahidi wa kushuka kwa kiwango cha kuaminiana katika siasa za Tanzania.

Kuhusu nini cha kufanya, inaonekana kuwa ni suala la kuku na yai. Kwa mfano nini kinapaswa kifanyike katika kujenga siasa za kuaminiana wakati ambapo vyama vimepoteza hata imani na mlezi wake yaani Msajili wa Vyama vya siasa? Au, nini kinapaswa kufanyika ili kurejesha kuaminiana kulikopotea kati ya wananchi na viongozi wanaowachagua? Tazama, wananchi walipoiunga mkono Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Warioba lakini wanasiasa wakaichakachua katika ngazi ya Bunge Maalumu la Katiba.

Ona jinsi kwa mfano wananchi na watawala wanavyopishana katika kufikiria namna ya kukabili tatizo la njaa katika Tanzania huku wanasiasa wakipiga marufuku nafaka kuuzwa nje ya mipaka na mikoa au nchi yao?

Kwa kuhitimisha, naona Tanzania imefikia mahali ambapo ni lazima tukamilishe mchakato wa Katiba Mpya kwa kuanzia kwenye Rasimu ya Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na siyo Katiba Inayopendekezwa. Tukifanya hivyo tutakuwa tumeanza kurejesha kuaminiana ambako kunazidi kutoweka siku hadi siku. Migogoro kama ile inayoendelea CUF ni ishara tu kwamba kuna tatizo la kimfumo katika namna tunavyoendesha Siasa Tanzania!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles