24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Afrika inafunika kombe mwanaharamu apite Ethiopia

wanamgambo-wa-oromoKINACHOENDELEA Ethiopia kinaiaibisha Afrika yenye hulka ya kunyamazia migogoro ya kisiasa kisha baadaye gharama nyingi hutumika kusuluhisha. Matukio yanayoendelea kwenye nchi hiyo yalipo Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU) katika Mtaa wa Rosevelt jijini Addis yanasadikisha usemi wa ‘funika kombe mwanaharamu apite’.

AU ilitangaza mwaka 2016 kuwa wa kutekeleza mkakati wa Afrika moja yenye amani usemi ambao ni sarakasi zilizokosa mwelekeo kutokana na mzozo endelevu katika kitovu cha makao yake makuu, kutokana na Serikali kutumia mkono wa chuma kuzima upinzani badala ya kutafuta ufumbuzi mwafaka.

 Ethiopia imetawaliwa na viongozi 11 tangu mwaka 1909 kuanzia Mfalme Fitawrari Habte Giyorgis aliyefariki miaka 18 baadaye akiwa madarakani akarithiwa na Rais Tafari Makonnen, kwa mtiririko wa watawala ulioendelea hadi kwa Melez Zenawi Waziri Mkuu aliyefia madarakani Agosti 20, 2012 aliyerithiwa na Waziri Mkuu wa sasa Hailemariam Desalegn. Mzozo wa takriban mwaka mzima kwenye nchi hiyo umechochewa zaidi na hali ya hatari ya miezi sita iliyotangazwa hivi karibuni na Serikali ili kukabiliana na waandamanaji kutoka Oromia na Amhara wanaopinga ukandamizaji.

Demonstrators chant slogans while flashing the Oromo protest gesture during Irreecha, the thanksgiving festival of the Oromo people, in Bishoftu town, Oromia region, Ethiopia Hasira za Waoromia ziliibuka baada ya wenzao 55 kuuawa katika sherehe ya dini yao ya kijadi mwanzoni mwa mwaka huu, wakaharibu miundombinu ya wawekezaji wa kigeni katika vurumai hizo zinazokadiriwa kuua watu 500 tangu zilipoanza Novemba mwaka jana. Lakini badala ya Serikali kusaka suluhu kwa hamkani iliyoianzisha yenyewe kwa kutaka kupanua Jiji la Ethiopia na kumega eneo kubwa la Oromia na kuathiri shughuli za kilimo, imezuia kutumiwa mitandao ya kijamii kuwasiliana na Ughaibuni ikidai kuwa wapinzani wanawasiliana na magaidi na nchi jirani zisizoitakia mema Ethiopia ikiwamo Eritrea wanayoituhumu kuchochea maandamano.

 Chaneli mbili za luninga za Esat na OMN zimepigwa marufuku kuangaliwa nchini humo, maandamano yameharamishwa kwenye maeneo yote zikiwamo shule na vyuo ambako vuguvugu la upinzani wa sasa lilichipukia, hairuhusiwi kuonesha ishara zozote za mwili zenye mrengo wa kisiasa ikiwamo ishara maarufu inayotumika nchini humo ya kupishanisha mikono juu ya kichwa iliyowahi kutumiwa na mwanariadha Feyisa Lilesa wa nchi hiyo, kwenye mashindano ya Olimpiki ya hivi karibuni jijini Rio akionesha kukerwa na ukandamizaji nchini mwake.

Hali ya hatari inazuia pia kukaribia viwanda, mashamba, majengo ya kiserikali na taasisi za kigeni kati ya saa 12 jioni na saa 12 asubuhi na wanadiplomasia wote wa kigeni walioko nchini humo hawaruhusiwi kusafiri zaidi ya kilomita 40 nje ya Jiji la Addis Ababa bila idhini maalumu ya Serikali inayodai kuwa ni kwa ajili ya kulinda usalama wao.

Kama unamiliki silaha huruhusiwi kutembea nayo ndani ya eneo la kilomita 25 karibu na barabara kuu nje ya mji mkuu, au kilomita 50 karibu na mipaka ya nchi hiyo hata kama una kibali halali cha kubeba silaha. Hadi kufikia hatua hiyo ni mwendelezo wa hamkani iliyoanzia katika Jimbo la Oromia mwishoni mwa mwaka jana wanachuo walipopambana na askari, kupinga upanuzi wa Jiji la Addis Ababa unaomega eneo kubwa la jimbo lao.

Baadaye wananchi wa kawaida nao wakajiunga katika kupinga mpango huo wa Serikali na maandamano yakazagaa sehemu nyingi za nchi hiyo licha ya Serikali kusitisha mpango wake wa upanuzi wa mji mkuu. Waoromo wanaosigana vikali na Serikali ndiyo kabila kubwa zaidi nchini Ethiopia linalokadiriwa kuwa na watu milioni 30, ikiwa ni theluthi nzima ya watu wote wa nchi hiyo lakini wakihisi kutengwa na kunyanyapaliwa na awamu mbalimbali za utawala nchini humo kutokana na maendeleo duni ya kiuchumi kulinganisha na maeneo mengine.

Mpango wa kumega jimbo lao ili kutanua Jiji la Addis Ababa kwa Waoromo ni sawa na kupaka chumvi kwenye kidonda, kwa kuwa mashamba yao yangetaifishwa na Serikali na kuwaacha watawala wao wa kijadi wakidhoofishwa kutokana na kupunguzwa kwa himaya zao wanazosimamia. Serikali nayo imekaza mkono wake wa chuma na chini ya sheria ya hali ya hatari zaidi ya watu 1,600 wengi wao kutoka Oromia na Amhara wamewekwa vizuizini, wengine 1000 wametiwa korokoroni jijini Addis Ababa katika ukamataji unaoruhusu vyombo vya dola kumkamata yeyote wakati wowote bila kumfungulia mashtaka ndani ya kipindi chote cha hali ya hatari.

Licha ya Serikali kuwakamata wapinzani lukuki mzozo wa Ethiopia ni bomu kubwa zaidi linalosubiri kulipuka, kwani silaha nyingi zilizokuwa mikononi mwa wananchi bila idhini zimekamatwa katika kinachojidhihirisha kuwa walikuwa na mkakati wa kuingia kwenye mapambano kamili. Ni mwenendo hatari kwa kuwa Waoromo nao wana vikundi vyao vya wanamgambo wapiganaji wenye silaha, ukijumuisha na fukuto la Eritrea ambayo ilipigana kujiondoa mikononi mwa Ethiopia iliyoigeuza jimbo lake enzi za utawala wa Mfalme Haile Selassie na ukabila unaoitafuna nchi hiyo, ambapo kwa miaka 25 iliyopita viongozi wake wengi wanaotawala kwa mabavu na kunyamazisha wapinzani wanatokana na kabila dogo la Watigri lenye watu wasiozidi asilimia sita ya Waethiopia milioni 90.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles