Na ESTHER MNYIKA-DAR ES SALAAM
KAMPUNI za simu za mkononi zimejipatia Sh trilioni 13.07 kupitia miamala ya huduma za fedha katika kipindi cha miezi miwili.
Fedha hizo zimepatikana kwa njia ya mitandao katika miezi miwili ya Novemba na Desemba mwaka jana.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Meneja wa Habari wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala
alisema fedha hizo zimepatikana kutokana na ongezeko kubwa la matumizi ya huduma za fedha kwa njia ya mitandao ya simu nchini.
Alizitaja kampuni zilizohusika na miamala hiyo kuwa ni Zantel kupitia huduma ya (Easy Pesa), Tigo (Tigo pesa), Vodacom (Mpesa), Airtel (Airtel Money na Halotel (Halopesa).
Mwakyanjala hakufafanua Serikali imepata kiasi gani cha kodi kutokana na fedha hizo za miamala pamoja na kiasi ambacho kila kampuni imejipata kutokana na mzunguko wa fedha hizo kwa njia ya mtandao.
“Mwezi Novemba tulikusanya Sh trilioni 6.47 na Desemba Sh trilioni 6.60, jumla ya makusanyo yote kwa miezi hiyo miwili ni wastani wa Sh trilioni 13.07 kupitia miamala ya simu za mkononi.
“Asilimia kubwa ya mzunguko wa fedha hupitia kwenye simu za mkononi kwa sababu watu wengi hivi sasa wanafanya miamala kwa njia ya mitandao ya simu kwa kutuma, kupokea fedha na kulipia huduma mbalimbali za umeme, maji na nyinginezo,”alisema Mwakyanjala.
Mwakyanjala aliwatahadharisha wananchi kuwa makini na matapeli wanaoghushi utaratibu wa mawasiliano kwa kuwalaghai watu kutuma fedha kupitia simu za mkononi.
Alisema katika siku za karibuni, matapeli hao wamekuwa wakituma ujumbe mfupi wa maandishi ambao unaonyesha mtu ametumiwa fedha kwa makosa na baadaye kufuatiwa na ujumbe mwingine unaofanana na ule wa watoa huduma ambako muhusika hutakiwa kurudisha fedha hizo.
“Nawashauri wananchi wasitekeleze maagizo yoyote kutokana na ujumbe wa simu za mkononi unaohusu fedha kwa mawasiliano ya simu.
“Hata kama inatoka kwenye namba ya mtu anayemfahamu, mpigie aliyekutumia ujumbe kwa namba nyingine kufanya uhakiki,” alisema Mwakyamjala.