24.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 29, 2023

Contact us: [email protected]

KILICHOIANGUSHA UKAWA UCHAGUZI WA MARUDIO HIKI HAPA

ASHA BANI Na JONAS MUSHI-DAR ES SALAAM


 

UCHAGUZISIKU moja baada ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Dimani visiwani Zanzibar na udiwani katika kata 20 za Tanzania Bara, mengi yameibuka ikiwamo kutajwa kwa sababu ya kuangushwa kwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wasomi, wanasiasa mbalimbali nchini wamezungumzia hatua ya kushindwa kwa Ukawa, huku baadhi ya vyama vikitaka kufanyika kwa mabadiliko na kuwapo tume huru ya uchaguzi.

Katika uchaguzi huo mdogo, vyama vya upinzani vimegaragazwa vibaya.

Katika Jimbo la Dimani, mgombea wa CCM, Juma Ali Juma aliibuka mshindi kwa kura 4,860 huku mpinzani wake wa CUF, Abdulrazak Khatib Ramadhan akipata kura 1,234.

Wakati CCM ikiibuka na ushindi wa kata 19 za udiwani, Chama cha Demokrasisa na Maendeleo (Chadema), kimefanikiwa kutetea kiti chake katika Kata ya Duru mjini Babati, huku Chama cha Wananchi (CUF), kikiambulia patupu baada ya kushindwa pia kutetea kiti chake cha Kimwani wilayani Muleba mkoani Kagera.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya siasa wamesema mara nyingi mshindi wa uchaguzi mdogo huwa ni wa chama kilichokuwa madarakani katika eneo husika, na kwamba vyama vya upinzani havina nguvu vijijini kama ilivyo CCM.

Mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), alisema vyama vya upinzani vina nguvu mijini kuliko vijijini, hivyo ilikuwa vigumu kwao kushinda uchaguzi huo.

“Hadi sasa CCM ina nguvu sana vijijini na haya ni matokeo ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere kukiimarisha chama zaidi kwenye ‘grassroots’ (ngazi za chini) na uhalisia ni kwamba upinzani wana nguvu zaidi mijini japo si miji yote,” alisema Profesa Mpangala.

Alisema ushindi katika uchaguzi mdogo huwa ni wa chama kilichotawala katika eneo husika na kwamba licha ya kwamba CUF ina nguvu Zanzibar, lakini kwa upande wa Unguja CCM ndiyo wana nguvu kwani hata mbunge wa Dimani alikuwa wa chama tawala.

Kutokana na hali hiyo, alisema matokeo hayo hayawezi kutumika kuonyesha kwamba wananchi wanaukubali uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano na badala yake ni matokeo ya mfumo wa siasa uliopo tangu miaka ya nyuma.

Akizungumzia uchache wa wapigakura waliojitokeza kwenye uchaguzi huo, alisema kwa kawaida uchaguzi mdogo huwa hauna hamasa kubwa kama ilivyo kwa Uchaguzi Mkuu.

 

Dk. Bana na udhaifu

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema ushindi waliopata CCM ni dhahiri kwamba upinzani umekwisha nguvu.

Alisema ushindi huo ni njia mojawapo ya mwaka 2020 kwa CCM kuwa na njia nyeupe ya kushinda uchaguzi bila upinzani kupata viti.

Dk. Bana alisema CCM bado ina nguvu, wananchi bado wa imani na ni ushahidi tosha Ukawa wameishiwa nguvu.

“Nilitegemea baada ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 Ukawa wangejipanga na kusajili chama kimoja, lakini wameshindwa kufanya hivyo basi wataendelea kugawana kura.

“Tatizo la Ukawa kwa sasa pia ni kushindwa kufanya kazi na matokeo yake wanamkumbatia mtu mmoja aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

“Lowassa kwa sasa ana mvuto yeye ndani ya Ukawa na sio Ukawa kuwa na mvuto na wananchi na mbaya zaidi hawawezi kufanikiwa kutokana na mparaganyiko uliopo kati ya Zanzibar na Tanzania Bara,’’ alisema Dk. Bana.

 

Dk. Lwaitama

Dk. Azaveli Lwaitama, alisema ni vigumu kusema CCM imeshinda ikiwa hakuna tume huru ya uchaguzi.

Alisema bila tume huru CCM itaendelea kushinda uchaguzi kwani imekuwa ikisaidiwa na dola.

“Katika hali ya kutokuwa na tume huru ya uchaguzi, mtu utaamini vipi kile kinachotangazwa ili ujue kweli kulikuwa na ushindani.

“Kwa hali kama hii ambayo Jeshi la Polisi linaenda kutanda kwenye jimbo la uchaguzi kama ilivyokuwa Dimani, lazima CCM iendelee kutawala, wala hatutafikia walipo wenzetu Kenya ambako chama kikishindwa kinakubali,” alisema Dk. Lwaitama.

 

UVCCM yatamba

Akizungumzia matokeo hayo, Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, alisema ushindi walioupata unaonyesha taswira njema kwa chama hicho tawala kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Alisema wamepokea ushindi huo kwa faraja na umeonyesha dhahiri CCM itaendelea kufanya vizuri kwenye kila uchaguzi kwani kwa sasa Watanzania hawajaona chama mbadala wa kushindana nayo.

Kaimu Katibu Mkuu huyo, alisema CCM ni chama makini na Watanzania wanakiamini pamoja na viongozi wake na ndiyo moja ya sababu iliyowafanya kukipa ushindi wa kishindo.

“Hakuna wa kuzuia nguvu ya CCM, tutaendelea kushinda kwa kuwa ni chama chenye demokrasia ya kweli na kimefanya uchaguzi huo kwenye uhuru, amani na ndiyo maana hata wananchi wanakikubali. Na hiyo ni ishara tosha kwamba mwaka 2020 wataisoma namba kweli kweli,’’ alisema Shaka.

 

Tundu Lissu

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), jana alizungumzia uchaguzi huo kupitia andiko lake na kusema matokeo hayo hayakishangazi chama, na kwamba hawana sababu ya kushangilia wala kuomboleza kwani imekuwa ni kawaida kushindwa kwenye uchaguzi mdogo.

Alisema imekuwa ngumu kushinda uchaguzi mdogo na kwamba historia inaonesha kuwa licha ya kushindwa kwenye uchaguzi huo, lakini hufanya vizuri zaidi kwenye Uchaguzi Mkuu unaofuatia.

Lissu alisema hawajapoteza kitu katika uchaguzi mdogo kwani hawajafanikiwa kuchukua kata za CCM na wala wao kunyang’anywa za kwao.

“Uchaguzi mdogo wa ubunge au udiwani ni mgumu sana kushinda katika mazingira halisi ya nchi yetu. Mifano michache inathibitisha ukweli huu. Katika ‘election cycle’ (mzunguko wa uchaguzi) ya 2005-2010 tulishinda Jimbo la Tarime, lakini tukapigwa Biharamulo Magharibi na Busanda.

“Tarime lilikuwa jimbo letu tangu Uchaguzi Mkuu wa 2005, Busanda lilikuwa la CCM na Biharamulo Magharibi lilikuwa la TLP.

“Sikumbuki vizuri kama tulishinda kata hata moja katika mzunguko wa uchaguzi wa kipindi hicho,” alisema Lissu na kuongeza:

“Hatujanyang’anywa iliyokuwa yetu (kata/jimbo), hatujanyakua zilizokuwa zao. Hata hivyo, funzo kubwa zaidi la historia ya uchaguzi huu ni kwamba licha ya kupigwa kwenye uchaguzi mdogo, tumeendelea kufanya vizuri zaidi katika kila Uchaguzi Mkuu uliofuatia kipigo cha uchaguzi mdogo,” alisema Lissu.

 

Mtatiro na mgogoro

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF ambaye hatambuliwi na Msajili wa Vyama vya Siasa, Julius Mtatiro, hakutofautiana sana kimtazamo na Lissu.

Alisema kuwa huwa ngumu kwa upinzani kushinda huku akimtupia lawama Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, kuivuruga Ukawa.

Alisema haoni uhusiano kati ya matokeo hayo ya uchaguzi mdogo na utendaji wa Serikali, kwani imekuwa kawaida CCM kushinda kwenye uchaguzi mdogo kutokana na kutumia nguvu nyingi za rasilimali na dola.

Alibainisha kuwa kulikuwa na uwezekano wa upinzani kushinda kata saba kama ungeungana, huku akikitaka Chama cha ACT-Wazalendo kufikiria kujiunga Ukawa.

 

CCM kufunguka leo

MTANZANIA ilipomtafuta Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kuzungumzia uchaguzi huo, alisema asingeweza kuzungumza  na badala yake chama hicho kitazungumza leo.

“Ilikuwa tuzungumze leo (jana), lakini tumeona ni vema kwanza tumpe nafasi Rais Dk. John Magufuli na ugeni wake (Rais wa Uturuki),” alisema.

 

Vijana CUF

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jumuia ya Vijana wa Chama cha Wananchi (JUVICUF), Hamidu Bobali, alisema kuwa sasa umefika wakati wa Mwenyekiti wa NEC, Jaji  Semistocles Kaijage kujitafakari kwa yaliyotokea.

Alisema katika zama za demokrasia haiingii akilini katika uchaguzi mdogo Jimbo la Dimani, kusiwepo na kura hata moja iliyoharibika.

Alisema kwa sasa vita iliyopo ni kubwa ya vyama vya upinzani, hivyo vinapaswa kuelekeza nguvu zake katika kudai tume huru ya uchaguzi na Katiba mpya.

Bobali ambaye pia ni Mbunge wa Mchinga, alisema bila kuwa na tume huru ya uchaguzi,  CCM ni ngumu kuiondoa madarakani kwa kuwa tayari imejitengenezea ushindi kabla hata ya kuingia katika masanduku ya kura na kupiga kura.

“JUVICUF tunapenda kuutangazia umma kuwa ni wazi sasa vita kubwa ya vyama vya upinzani inapaswa ielekezwe katika kudai Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, katika hili JUVICUF kutoka sasa tutakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha tume huru inapatikana,” alisema Bobali.

Aliongeza kuwa mawakala wao walitolewa nje kutokana na msimamizi wa uchaguzi kutumia daftari  jingine kinyume na lile ambalo lilitolewa na Tume ya Uchaguzi kwa mawakala wote.

Akizungumzia uchaguzi wa madiwani, alikiri udhaifu kutokea kutokana na mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho.

Bobali alisema kuwa CUF ilikuwa na uwezekano wa kushinda kata zaidi ya nne ambazo ni Kimwani ambayo walikuwa wakiitetea, Kiwanja cha Ndege, Nkome na Malya

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles