Na Balinagwe Mwambungu,
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), leo kinaadhimisha miaka 40 tangu kuzaliwa kwake Februari 5, 1977 baada ya vyama vya Tanganyika African Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP) kuungana. Maadhimisho hayo yamefanyika mkoani Dodoma.
Wakati CCM inatimiza miaka hiyo, ni muhimu kuitazama CCM ya sasa na ile ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Itakumbukwa kuwa Mwalimu Nyerere alipata kuwashangaza wananchi wake pale alipotangaza kujiuzulu miezi miwili tu baada ya kuliongoza Taifa jipya la Tanganyika. Tanganyika ilipata uhuru wake kutoka Uingereza Desemba 9, 1961.
Katika maelezo yake, Mwalimu Nyerere alisema anaachia ngazi kwa sababu anataka atumie muda mwingi kukijenga chama, ili kiweze kutimiza ‘malengo yake mapya’ akimaanisha uundwaji wa nchi ambayo watu wake wanashiriki kikamilifu katika vita dhidi ya umasikini, ujinga na maradhi.
Kuna dhana kwamba huenda Mwalimu Nyerere alikuwa na nia njema na ya dhati kabisa ya kukijenga chama chake cha Tanganyika African Union (TANU) kwa kuwa pamoja na kukubalika kwa wananchi na kukipa nafasi ya kuwa chama cha kwanza cha ukombozi, lakini hakikuwa na wanachama wengi. Wakati Tanganyika inajitawala, ilikuwa na watu milioni 9, TANU ilikuwa na wanachama wangapi wakati huo ukitilia maanani kwamba wananchi wengi walikuwa hawana mwamko wa kisiasa na kwao suala la kujitawala lilikuwa ni ndoto ya mbali sana. Kwa hiyo dhana ya kujijenga chama ilikuwa na mashiko. Wakati huo kulikuwa na vyama vingi na vyenye mitazamo tofauti-hasa chama kikuu cha upinzani cha African National Congress (ANC), kilichokuwa chini ya uongozi wa Zuberi Mtemvu. ANC kilikuwa na sera ambayo ilipingana na ile ya TANU—kwamba Afrika ni kwa Waafrika tu, wakati TANU iliamini kwamba Tanganyika bila kujali dini, kabila au rangi, ilikuwa kwa ajili ya watu wote ambao wanaukubali uraia wa Tanganyika.
Kuna dhana pia kwamba Mwalimu alipatwa na woga wa kutojua yatakayojiri mbele, Waingereza wanaita Fear of the Unknown.
Ikumbukwe kwamba wakati Tanganyika inapata uhuru, haikuwa na wananchi wasomi na wajuzi wa mambo ya utawala. Nyerere mwenyewe, ingawaje alikuwa msomi, alikuwa hana ujuzi wa uongozi, hata alipoachia ngazi ya kazi ya ualimu mwaka 1955, ili atumie muda wake mwingi kuijenga TANU, alikuwa pia na wasiwasi na woga, fear of the unknown.
Mtu yeyote ambaye hajawahi kuongoza watu, Mwalimu Nyerere hakuwahi hata kuteuliwa kuwa mwalimu mkuu, lakini alikuwa mtu makini na aliwapenda watu wake. Hii haikuwa na maana kwamba hakuwa na woga, ifahamike kuwa wakati anaacha kazi ya ualimu, tayari alikuwa na mke na watoto. Sasa unapoacha kazi lazima utawaza namna familia yako itakavyoishi, wewe ukiwa katika harakati hatari za mapambano ya kisiasa na unafanya hivyo bila mshahara, lazima utakuwa na woga kwa kuwa hujui yatakayojiri, fear of the unknown.
Ni viongozi wachache wanaoutafuta uongozi ili waweze kuleta mabadiliko kwa wananchi wao. Uongozi wa sasa, hasa katika chama tawala, CCM, wengi wao wanatafuta nafasi za uongozi kwa manufaa yao na familia zao.
Viongozi wa TANU, wengi wao walikuwa wanafanya kazi kwa kujitolea, kwa sababu kwanza chama chenyewe hakikuwa na fedha za kuwalipa mishahara, lakini walikuwa na ari ya kuona kuwa wanaleta mabadiliko katika maisha ya wananchi wa Tanganyika. Hiki ndicho kilichowaunganisha viongozi.
Kama nilivyoeleza awali kuwa CCM kinatimiza miaka 40 baada ya muungano wa ASP kwa upande wa Zanzibar na TANU upande wa Tanganyika. CCM ni mrithi wa vyama hivyo viwili, vyama ambavyo vilileta uhuru kwa nchi hizo mbili, vikiwa na malengo bayana na yaliyoshabihiana kuwaunganisha wananchi, kulinda uhuru wa nchi na kusimamia maendeleo ya nchi kwa pamoja, vikipambana na ujinga, umasikini na maradhi.
Wakati inatimiza miaka hiyo 40 pia ina miaka 40 ya kutawala, ukiachilia mbali miaka ya nyuma ambayo vyama viwili viliongoza nchi.
Kuna maswali lukuki kuhusu mwenendo wa CCM miongoni mwa maswali hayo je, CCM ya leo ina mwelekeo gani? Je, CCM ni chama kimoja chenye msimamo mmoja, chenye kuwaunganisha wananchi? Je, ndani ya chama hicho kuna mshikamano au kiko mafungu mafungu. Je, viongozi wake wanachaguliwa kwa uhuru na kwa haki.
Je, viongozi wake kwa ujumla wana mitazamo sawia au wanajitazama wao kwanza wananchi baadaye. Maswali haya nawaachia wenyewe waweze kuyatafakari na kuyapatia majibu. Nimewahi kuandika huko nyuma kwamba CCM inabidi ijitathmini na kutengeneza dira mpya kwa sababu uwanja wa kisiasa sasa hivi umebadilika. Miaka 40 ya uongozi wa nchi ni muda mrefu na duniani kuna mabadiliko makubwa tofauti na mwaka 1977 CCM ilipozaliwa.
Miaka 40 ni muda mwafaka wa CCM kurejea dira yake na kuangalia kama inaendana na wakati uliopo. CCM ya Nyerere ilkuwa CCM yenye Dira ya Ujamaa na Kujitegemea. Dira ya CCM ya sasa ni ipi.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Horace Kolima (marehemu), aliwahi kutamka kwamba chama hicho kilikuwa kimepoteza dira, viongozi wenzake hawakumwelewa na wakamdhihaki kwamba alikuwa msaliti. Sasa ni wakati mzuri kwa chama cha Mwalimu Nyerere kujitazama upya wapi kilikwenda mrama.
Nasema bila kupepesa macho kwa sababu nakijua Chama Cha Mapinduzi, nilikuwa miongoni mwa waanzilishi wake.
Sera ya Ujamaa na Kujitegemea ilishafutwa na Azimio la Zanzibar pamoja na miiko ya uongozi. Watu wengine walipojaribu kuwashauri viongozi kwamba miiko ya uongozi ni muhimu ili uongozi usiwe uongozi wa biashara. Ilishauriwa kwamba watu wanaotaka kuwa viongozi, wasiwe wafanyabiashara kwa sababu zilizo wazi, lakini wenye kushika hatamu na kwa sababu ya ubinafsi wao, hawakusikiliza.
CCM sasa hivi inaongozwa na watu ambao hawako pamoja na wananchi, waliutafuta uongozi ili wajinufaishe. CCM ilishapokwa kwa wanachama, ni chama cha matajiri. Bila mtu kuwa na fedha za kununua uongozi haiwezekani ukapata uongozi. Haihitaji kuwa profesa wa siasa kusema ndani ya CCM hakuna uongozi wa pamoja, hakuna mshikamano, hakuna chaguzi za haki na za kidemokrasia. Kuna uongozi wa makundi, mwenye nazo anatumia fedha zake kununua uongozi. Ndani ya chama tawala kuna nyufa zilizotokana na mpasuko wa kutafuta uongozi, kuna mitandao mingi ambayo inatengeneza watu wao ifikapo wakati wa uchaguzi.
Wakati wa Uhuru, Mwalimu Nyerere alisema: Sisi tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro. Umulike nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hapana matumaini, upendo mahali ambapo pana chuki na heshima pale ambapo pana dharau. Hii iwe rejea ya CCM kama itakwenda mapumziko (retreat) ya kujitafakari.
Kabla ya kwenda mapumziko, iunde tume ya wataalamu, wapite kwa wananchi na wawaulize maswali yanayowahusu wao wenyewe na mahusiano na matamanio yao kwa Chama Cha Mapinduzi.
Naweza kusema kwamba chama tawala kina kale kaugonjwa alikokuwa nako Mwalimu Nyerere wakati Tanganyika inajitawala, fear of the unknown.
Historia imetimiza mzunguko wake (it has gone full circle), tulianza na mfumo wa vyama vingi, ukavunjwa na tukabaki na mfumo wa chama kimoja. Mwaka 1993 tukarejea kwenye mfumo wa vyama vingi ili kupanua wigo wa demokrasia. Ishara zinaonyesha kwamba kuna viongozi ambao wanataka kuturejesha kwenye mfumo ule ulioshindwa.
Imepita miaka takribani 30 tuliporejesha mfumo wa vyama vingi, lakini inaonekana watawala hawataki kuachia madaraka ndiyo maana wanaendesha chaguzi zenye figisu figisu na tusiwalaumu, wana kaugonjwa ka fear of the unknown. Itakuwaje kama CCM itaanguka katika uchaguzi?