25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

KUBENEA JINA KUBWA, JIMBO TATA

NA EVANS MAGEGE,

JIMBO la Ubungo ni miongoni mwa majimbo yenye hekaheka nyingi za biashara ya uchuuzi, pia ni kitovu cha usafirishaji wa abiria ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam.

Ndani ya jimbo hilo kuna Kituo Kikuu cha mabasi ya abiria (Ubungo Bus Terminal). Kituo hicho kinahudumia mabasi kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na nchi jirani.

Kisiasa jimbo la Ubungo limekuwa na historia ya ushindani mkubwa hasa wakati chaguzi mbalimbali kama wenyeviti wa mitaa, udiwani na ubunge.

Kwa misingi hiyo, jimbo hili kwa sasa  linaongozwa na mbunge wa upinzani ambaye pia ni wanahabari, Saed Kubenea.

Kubenea ambaye ana takribani mwaka moja na miezi miwili tangu achaguliwe kuliongoza jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 aligombea kupitia Chadema akishindana na mpinzani wake wa karibu marehemu Didas Masaburi wa CCM.

Kabla ya jimbo hilo kuzaa Wilaya Mpya ya Ubungo lilikuwa ni sehemu ya Wilaya ya Kinondoni  na kijiografia na katika ramani ya wilaya hiyo jimbo hilo lilitambulika kuwa upande wa Magharibi.

Taarifa ya Novemba mwaka jana iliyotolewa na mtandao wa DAR RAMANI HURIA, inatanabaisha  kuwa Jimbo la Ubungo lina kilomita za mraba 10.17 zinazojumuisha kata nane.  Kilometa za mraba 0.58 sawa na asilimia 6 ya jimbo lote hukumbwa na mafuriko.

Taarifa hiyo ni baada ya jimbo hilo kugawanywa na Serikali na kuzaa jimbo jipya la Kibamba.

Kata zinazounda Jimbo la Ubungo ni Kimara, Ubungo, Sinza, Manzese, Makurumla, Mburahati, Mabibo na Makuburi.

Idadi ya wakazi wa jimbo hilo inakadiriwa kuwa ni zaidi ya 500,000. Kwa mujibu wa taarifa ya DAR RAMAN HURIA Jimbo la Ubungo lina idadi ya majengo 9,282  huku majengo 1,102 zikiwamo shule 12  yapo kwenye hatari ya kukumbwa na mafuriko.

Aidha, mbali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, majengo mengi ndani ya Jimbo la Ubungo yanakabiliwa na tatizo la miundombinu ya mifereji ya kusafirisha maji taka. Hata ile mifereji michache iliyopo haina uwezo wa kusafirisha kiasi kikubwa cha maji taka hasa kipindi cha mvua.

Ongezeko la watu ndani ya Jimbo la Ubungo linatajwa kuongeza mahitaji makubwa ya nyumba za kuishi pamoja na zile za kufanyia biashara.

Mazingira hayo pia yamesababisha ujenzi kufanyika kwenye njia ya maji hivyo matokeo yake kumekuwa na tatizo kubwa la maji kutuwama kwa muda mrefu na wakati mwingine kusababisha mafuriko ya mara kwa mara kwenye makazi ya watu.

KERO ZA WANANCHI

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mtanzania Jumapili wanataja maji na miundombinu kama kero kubwa kwao.

Abbas Juma, mkazi wa Mtaa wa Makoka, Kata ya Makuburi, anasema kero kubwa ni uhaba wa maji pamoja na miundombinu ya barabara.

Anasema kero ya maji imeendelea kuwa changamoto ya maisha ya wakazi wa kata hiyo licha ya mbunge anayeongoza jimbo hilo kwa sasa kutoa ahadi wakati wa kampeni kuwa atatia kipaumbele kutatua tatizo la uhaba wa maji.

“ Huku maji yanatoka mara moja kwa wiki na wakati mwingine wiki nzima inapita bila maji kutoka…maji ya kununua dumu moja linauzwa Sh. 500  sasa jiulize watu.

 wanaoga au wananawa? kama unavyojua familia za Kiafrika ni kubwa sasa haya maji ya kununua tutayamudu vipi na hali hii itakuwa hivi hadi lini? alihoji Juma

Juma anaongeza kwamba mbali na kero ya maji pia barabara ya mchichani ambayo ni kitovu cha mawasiliano kati ya Ubungo na Makoka nayo imekuwa mbovu kwa kipindi kirefu.

Anasema pamoja na ukarabati wa mara kwa mara unaofanywa na serikali hata hivyo barabara hiyo haiwezi kuhimili mvua, mara nyingi udongo husombwa na maji na kukata mawasiliano.

Mary Justine na Adam Mkwepu  kwa nyakati tofauti wanazungumzia ukosefu wa maji kuwa ndiyo kero kubwa katika Kata ya Kimara. Wanasema kero hiyo imedumu kwa miaka mingi ingawa kumekuwa na ahadi nyingi za kisiasa ambazo hazijatoa mwanga wa kutatua tatizo hilo.

“ Tumeona juhudi kwa kiwango fulani lakini tatizo bado lipo na kila mkazi wa Kimara analalamika kwa sababu uhalisia maji bado hayajawafikia wengi,” alisema Adam.

Adrew Anthony na Zena Said wa Mtaa wa Ubungo Kibangu katika Kata ya Ubungo nao wanasema kero ya maji ni kubwa na watu wengi hawapati huduma ya maji ya bomba.

“Mkazi wa  hapa Kibangu hata ukimshitua usingizini usiku wa manane ukamuuliza swali changamoto zetu nini atakujibu bila kupepesa macho kwamba anakerwa na ukosefu wa maji. Hili ni tatizo sugu na mkawambie huko kwamba hata sisi ni binadamu kama hao wanaoishi Masaki, tunahitaji maji,” anasema Zena.

Elisante Shayo mkazi wa Kata ya Mburahati anasema miundombinu ya barabara na ukosefu wa maji ni tatizo katika kata hiyo. Anasema huduma ya maji inayotolewa haitoshelezi mahitaji ya wakazi wa kata hiyo.

Pia anasema eneo hilo linakabiliwa na vibaka maarufu kwa jina la Panyaroad ambao mara kwa mara wamekuwa wakipora na kushambulia watu.

“ Pia barabara inayounganisha Manzese na Mburahati  ilijengwa bila kiwango kwamba ndani ya miaka miwili imeharibika na hivyo naomba barabara hii ikarabatiwe tena,” anasema

MAJIBU YA MBUNGE

MTANZANIA Jumapili lilizungumza Mbunge wa Ubungo, Said  Kubenea ambaye anakiri kuwapo kwa changamoto hizo na kutanabaisha wazi kwamba amefanikiwa kupunguza kero hizo katika baadhi ya maeneo.

Kuhusu hoja ya barabara ya mchichani inayotoka eneo la Ubungo Riverside hadi Makoka, anasema  barabara hiyo ina urefu wa kilomita 3.7 ilishafanyiwa ukarabati mwaka jana .

“Hiyo barabara ya mchichani inapita hapo maeneo ya Kajima, Nova inakwenda mpaka Makoka mwisho. Ni kweli kwamba mvua za masika za mwaka jana ziliharibu kabisa ikawa haipitiki kabisa kwa hiyo baada ya kurudi kwenye Bunge la Bajeti  nikakusanya baadhi ya posho zangu na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni wakati huo  tukaikarabati kwa kupitisha greda na kuweka kifusi kwa sababu ilikuwa haipitiki kabisa.

“ Ukiangalia kabla ya mimi sijawa mbunge na sasa hivi utabaini barabara hiyo imekuwa na mabadiliko makubwa ukilinganisha na wakati ule,” Anasema.

Anasema licha ya kwamba hajaweza kujenga barabara za kudumu kwa maana ya kiwango cha lami au lami nyepesi hata hivyo kwa kipindi hiki barabara nyingi za jimbo lake zinapitika.

KERO YA MAJI

Kuhusu kero ya maji, mbunge huyo alikiri kuwapo na kero hiyo katika jimbo zima la Ubungo.

Anasema wakati amepata nafasi ya ubunge, maeneo ya Kimara yalikuwa hayana maji kabisa lakini kwa sasa amefanikiwa kwa kiasi kidogo kutatua kero hiyo.

“ Ukiangalia Kata ya Makuburi ilikuwa haina maji kabisa lakini kwa sasa hivi karibu asilimia 60 ya kata hiyo inahuduma ya maji. Lakini maeneo kama ya Kajima na kule milimani kama unavyoifahamu jiografia ilivyo ni kweli maji kule hayapandi  na hiyo ni kwa sababu ule mfumo wa mabomba ya mradi wa Wachina haukufanya vizuri.

Anasema Serikali imefanya jitihada za kupanua mfumo wa maji lakini mifumo ya DAWASCO kwa maana ya mashine za kusukuma maji hazina uwezo wa kusambaza maji kwa wakati mmoja kwamba mazingira hayo yamesababisha huduma ya maji itolewe kwa mgawo .

“ Hata hivyo tunajaribu kuibana Serikali ili iweze kutatua tatizo hilo ingawa bado hatujafanikiwa kwa asilimia 100.” Anasema.

Anaeleza kuwa ndani ya mwaka mmoja wa ubunge wake, tatizo la maji katika Jimbo la Ubungo limepungua ukilinganisha na kipindi cha nyuma.

“Asilimia 30 ya wananchi ambao hawakuwa na huduma ya maji kwa sasa wanaipata huduma hiyo.” Anasema.

Anasema Kata ya Manzese haina kero kubwa ya maji kulinganisha na Kata ya Kibangu na Kimara.

Aidha, Kata ya Manzese, Makurumla pamoja na Mburahati zinapata huduma ya  maji ya bomba pia zina visima vingi vya maji.

Pamoja na mambo mengine ameeleza kwamba anajitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kutatua kero zinazowakabili wakazi wa jimbo lake hasa katika miradi ya maendeleo na kuishauri serikali kuelekeza nguvu.

“Ni kweli najitahidi lakini haya mambo yanategemea nguvu ya serikalini na halmashauri . Sasa tangu Halmashauri ya Ubungo ifunguliwe shida kubwa iliyojitokeza ni kwamba shughuli nyingi haziendi vizuri kwa sababu ya haya matatizo tuliyonayo.  Kwa mfano tuna bajeti ambayo tuliipitisha pale Kinondoni sasa tumehama nayo kwa ajili ya kwenda kuitekeleza Ubungo.

“ Bajeti inahitaji fedha sasa vyanzo vingine vya mapato vilikuwa Kinondoni na Kinondoni iko wazi ina vyanzo vingi vya mapato kama hoteli na kadhalika. Leo tumekwenda Ubungo kuanzisha halmashauri mpya unajikuta Ubungo hakuna vitu hivyo. Kwa mfano mpaka sasa hivi Halmashauri ya Ubungo bado haijaitisha kikao cha baraza la madiwani,” anasema.

AFYA

Kubenea anazungumzia sekta ya Afya kuwa imeboreka huku akitolea mfano wa Hospitali ya Wilaya ya Ubungo ambayo ni Sinza Palestina kwamba huduma zake zimeboreshwa zaidi tofauti na siku za nyuma.

“ Ukiangalia majengo, mazingira ya ndani hali ni tofauti kabisa kabla sijakuwa mbunge. Pia tumefanikiwa kuboresha wodi ya wajawazito, tumepeleka vitanda na kwa ujumla kuna maendeleo makubwa,” anasema Kubenea

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles