Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewapandisha kizimbani, mhariri na mwandishi wa gazeti la Dira ya Mtanzania, Musa Mkama na Prince Newton wakidaiwa kuandika habari za uongo zilizoleta mtafaruku kwa jamii.
Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu Respicius Mwijage, Mawakili wa serikali, Timon Vitalis na Hellen Mushi, walidai Juni 20 katika eneo la Biafra Kinondoni, Dar es Salaam, washtakiwa waliandika na kuchapisha habari za uongo katika gazeti la ‘Dira ya Mtanzania’ toleo la 424 la tarehe 20 hadi 26 ambazo zilisababisha hofu na mshtuko kwa jamii kwa kutoa taarifa za uongo kuwa ‘Kifaru cha kivita cha Jeshi la Wananchi(JWTZ), chaibwa’.
Alidai kitendo hicho ni kosa katika sheria na ni kinyume na sheria ya magazeti.
Wakili Vitalis alidai upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.
Hata hivyo, washtakiwa hao walikana shtaka hilo na Hakimu Mwijage aliwataka kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh milioni tano.
Washtakiwa hao walikidhi masharti ya dhamana na Hakimu Mwijage aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 5 mwaka huu itakapotajwa tena.