29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mgombea urais Chadema kupatikana Agosti

Freeman-MboweNA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinatarajia kumpata mgombea wake wa urais Agosti 4, mwaka huu.
Kupatikana kwa mgombea huyo kutatokana na uamuzi wa mkutano mkuu wa taifa, ambacho ndio chombo cha juu cha uamuzi.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, wakati akitangaza kwa waandishi wa habari uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu kilichoketi kwa siku mbili.
Alisema pamoja na mambo mengine kikao hicho kilijadili ratiba ya kuwapata wagombea wa udiwani, ubunge na urais ambao utaratibu wa kuwapata utaanza Mei 18 hadi Agosti 4.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa ngazi ya udiwani utaanza Mei 28 hadi Juni 25.
“Julai Mosi hadi 10 itakuwa ni kuchukua na kurejesha fomu kwa kata ambazo tuna madiwani na Julai 15 hadi 20 utakuwa uteuzi wa mwisho wa wagombea udiwani wa kata pamoja na wale wa viti maalumu.
“Mei 18, hadi Juni 25 itakuwa ni kuchukua na kurejesha fomu za ubunge kwa majimbo ambayo hatuna wabunge kwa sasa pamoja na viti maalumu, na Julai 6 hadi 10 ni uchukuaji na urejeshaji fomu za ubunge kwa majimbo ambayo tuna wabunge kwa sasa.
“… Julai 20 hadi 25 ni uteuzi wa awali kwa wagombea ubunge kazi itakayofanywa na Kamati tendaji za majimbo. Hata hivyo pia Julai 20 hadi 25 ni kuchukua na kurejesha fomu za mgombea urais ambazo zitasimamiwa na Makao Makuu,” ilionyesha ratiba hiyo iliyotolewa na Chadema.
Pamoja na mchakato huo, Chadema imesema kuwa uteuzi wa mwisho wa wagombea ubunge utafanyika Agosti 1-2 kazi ambayo itafanywa na Kamati Kuu ya chama hicho.
“Agosti 3, mwaka huu kitaketi kikao cha Baraza Kuu chini ya utaratibu wa Kamati Kuu na Agosti 4 utafanyika Mkutano Mkuu wa Taifa ambao utafanya kazi ya kuchagua mgombea urais kwa mujibu wa Katiba ya Chadema,” alisema Mbowe.
Akizungumzia kuhusu maazimio ya kikao cha Kamati Kuu, Mbowe alisema wamepokea, kujadili na kukubaliana makubalino yaliyokwishafikiwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Ukawa – umoja ulioanzishwa Februari mwaka jana ukiwa ni kikundi shinikizi katika mchakato wa Katiba katika siku za mwanzo za Bunge Maalumu la Katiba, inaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu, Mbowe alisema wamebaini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Serikali hawana dhamira ya dhati ya kisiasa wala maandalizi ya kutosha yakiwamo matakwa ya kisheria, kitaalamu na kibajeti ili kuhakikisha unafanyika kwa mujibu wa Katiba.
Kuhusu kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa, alisema baada ya kujadili kwa kina wamebaini kuna haja kura hiyo isogezwe mbele hadi baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Akizungumzia kuhusu uwapo wa Uchaguzi Mkuu, Mbowe alisema kimsingi Chadema imebaini kutokuwapo kwa maandalizi ya vifaa, fedha, kutangaza majimbo, kata mpya pamoja na vituo.
“Kamati Kuu imeazimia kuiomba Serikali kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unafanyika Oktoba kwa mujibu wa Katiba na Serikali ya CCM isijiandae kutumia kisingizio chochote kuahirisha kwa sababu uchaguzi sio jambo la dharura bali limekuwa likijulikana tangu miaka mitano iliyopita,” alisema.
Wakati Chadema wakitangaza ratiba yao ya kuwapata wagombea katika majimbo, vyama wenza vinavyounda Ukawa vya CUF na NCCR-Mageuzi vilishatangaza ratiba zao, lakini hadi sasa vimekuwa kimya kuhusu mchakato wake wa ndani wa kuwapata wagombea wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles