24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mgogoro kufutwa kwa uchaguzi

Seif_Sharif_HamadBAKARI KIMWANGA NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ametaja athari zilizojitokeza kutokana na kufutwa kusiko halali kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ni za kikatiba, kisiasa na kijamii.

Akitaja athari ya kwanza kuwa ni kutokea kwa mgogoro mkubwa wa kikatiba na kisheria ambao hautambui uhalali wa kuwapo kwa Rais wa Zanzibar.

“Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar chini ya kifungu cha 28(2) kimeeleza wazi kwamba muda wa rais kushikilia wadhifa huo ni miaka mitano na kifungu cha 29 kinaeleza masharti ya kuongeza muda huo wa miaka mitano ambayo ni magumu na yenye ukomo maalumu,” alisema Maalim Seif.

Alisema kwamba hata hivyo washauri wa rais kwa kutumia tafsiri isiyokuwa sahihi ya katiba wamemshauri kwamba kwa kutumia kifungu cha 28(1)(a) anaweza kuendelea kuwa rais hadi rais mpya atakapoapishwa.

Maalim Seif alielezea mipaka ya kifungu 28(1)(a) kinachoruhusu rais aendelee hadi anayefuata atakapokula kiapo kina mipaka ya wazi katika katiba.

“Mpaka wa kwanza unahusu muda wa urais. Katiba chini ya kifungu cha 28(2) kimeweka bayana muda wa urais ni miaka mitano, hili ni sharti muhimu na ndiyo maana Katiba haijaruhusu suala la kuongezwa muda wa miaka mitano lifanywe kiholela au kwa mlango wa nyuma,” alisema Maalim Seif.

Aliongeza kuwa kifungu cha 29 cha Katiba kimeweka sababu na utaratibu wa kuongeza miaka mitano.

“Kifungu hicho kinaeleza kwamba ikiwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imo katika vita na ikiwa rais anaona kuwa ni muhimu kuzuia uchaguzi, Baraza la Wawakilishi linaweza kwa kupitisha azimio, kuzidisha muda wa miaka mitano uliotajwa kwenye kifungu 28 (2) katika kipindi hadi kipindi, lakini hakuna kipindi kitachozidi miezi sita mfululizo,” alisema.

Maalim Seif alionyesha Katiba isivyokuwa na mwanya wa kuonyesha kujiongeza muda kwa kiongozi zaidi ya ukomo wa miaka mitano chini ya kifungu cha 30(1)(b).

Alisema kifungu hicho kinasema “endapo mtu anayemfuata rais kwa madaraka atashika kiti cha rais kwa kipindi kinachopungua miaka mine, ataruhusiwa kugombea nafasi ya rais mara mbili, lakini kama atashika kiti cha rais kwa muda wa miaka minne au zaidi ataruhusiwa kugombea nafasi ya rais mara moja tu”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles