31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, December 2, 2023

Contact us: [email protected]

Maalim Seif: CCM wanategemea nguvu ya dola

NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema jeuri ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatokana na wao kutegemea dola huku wakisahau nguvu ya umma.

Amesema hatua hiyo inatokana na viongozi wa chama hicho hasa kwa upande wa Zanzibar, kuibuka hadharani na kuwataka Wazanzibari wajiandae na uchaguzi wa marudio jambo ambalo alilipinga.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Maalim Seif alisema anajua hivi sasa kuna kila hila zinafanywa za kupotosha umma.

“Hili la kwanini CCM wanazungumzia uchaguzi, nafikiri waulizwe wao. Lakini nataka kusema labda kwa sababu wao wanategemea dola, lakini nataka kuwaambia dola haiwezi kufua dafu mbele ya nguvu ya umma.

“Umma una nguvu na ukiamua hakuna wa kuwazuia, pamoja na kujiamini kwa kuwa na vyombo vya dola wajue kwamba nguvu ya umma ikiamua hakuna wa kuweza kuizuia kwa namna yoyote ile ingawa CUF hawana mpango wa kuruhusu yatokee yaliyotokea mwaka 2011,” alisema Maalim Seif.

Kuhusu taarifa za makubaliano ya kurudiwa uchaguzi huku akiogopa kuitwa msaliti na wafusi wa chama chake kwa kukubali uamuzi huo, alisema hakuna makubaliano ya kurudia uchaguzi ila kilichopo ni taarifa za mitaani.

“Mimi ni mtu ninayejiamini, sina hofu, nikichukua maamuzi sijali. Je, wanasahau yaliyotokea mwaka 2000? Na hata CUF wanajua. Ninaongozwa na masilahi ya nchi na si woga na kama kuna maneno haya ni uzushi, uchakubimbi na unafiki.

“Sina imani na marudio ya uchaguzi Zanzibar na katu kurudia ni kuipeleka katika vurugu ambapo hatutaki tufike huko,” alisema Maalim Seif.

Katika mazungumzo yake alionyesha kumwamini Rais Dk. John Magufuli katika kutatua mgogoro hali iliyofanya kuulizwa kuhusu imani yake wakati akijua kiongozi huyo ni mwanachama wa CCM.

Akijibu swali hilo, alisema imani yake inatokana na dhamira ya Rais Magufuli aliyoionyesha kwake katika mazungumzo aliyofanya naye Ikulu Dar es Salaam.

“Kama Rais Magufuli angekuwa na mtazamo wa kutaka kurejewa kwa uchaguzi asingetaka mazungumzo na mimi kisha kuzungumza na Shein,” alisema.

 

LOWASSA AONGOZA Z’BAR

Maalim Seif alisema katika kile alichokiita Wazanzibari wameamua kwa kufanya mabadiliko, hata aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa, alishinda katika matokeo ya uchaguzi ya urais visiwani humo.

Alisema kuwa CCM ilishindwa vibaya katika uchaguzi uliopita na hilo limedhihirisha kwenye kura za urais Lowassa akiongoza kwa kura 211,033 sawa na asilimia 50.50, akifuatiwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Magufuli ambaye alipata kura 194,317 sawa na asilimia 46.5.

“Matokeo haya yote yanaonyesha namna CCM ilivyoshindwa na matokeo zaidi yanayothibitisha hilo ni kura za ubunge, uwakilishi na udiwani yote yanaonyesha CCM ilishindwa. CCM imeweza kupata viti sawa na CUF katika uwakilishi na ubunge kwa sababu ya mbinu zilizotumika katika ukataji wa majimbo,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif alisisitiza kwamba hoja ya kurudia uchaguzi haina msingi na haiwezekani kutekelezwa kwa sababu ya kukosekana uhalali wa msingi wa kurejea uchaguzi.

“Kama ilivyoelezwa kwamba hatua ya mwenyekiti wa ZEC kufuta uchaguzi haikuwa halali na ina kasoro nyingi za kikatiba na kisheria, kurejea uchaguzi ni sawa na kuhalalisha kitendo batili alichofanya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi na kuweka ‘Precedent’ mbaya kwamba uchaguzi unaweza kufutwa kwa sababu zozote zile japo kama si halali,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles