
Na KADAMA MALUNDE-Shinyanga
MGANGA wa kienyeji, Kashinje Kashinje (55), mkazi wa Kijiji cha Singita, Shinyanga, ameuawa kwa kupigwa na wananchi baada ya kujaribu kumbaka mwanamke mmoja anayedaiwa kuwa mteja wake aliyekuwa anamtibu ili apate mtoto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Jumanne Muliro, alisema tukio hilo lilitokea Novemba 29, mwaka huu saa tano asubuhi katika Kijiji cha Singita.
Alisema mganga huyo alifariki dunia alipokuwa njiani akipelekwa hospitali baada ya kujeruhiwa kwa kitu chenye ncha kali jicho la kulia na kupigwa kwa fimbo mgongoni na watu waliojichukulia sheria mkononi.
“Watu hao walijichukulia sheria mkononi baada ya mganga huyo kujaribu kumbaka mwanamke (jina linahifadhiwa), mkazi wa Kijiji cha Ishinabulandi, Wilaya ya Shinyanga, ambaye alikuwa akimtibu kwa tiba za asili ili aweze kupata mtoto.
“Inavyoonekana chanzo cha tukio hilo ni tamaa za kimwili na uongo wa kimatibabu wa kutaka kumwingilia kimwili mgonjwa wake baada ya kumlewesha kwa dawa za kienyeji,” alisema Kamanda Muliro.
Alisema wakati wa tukio hilo, mwanamke huyo alipiga kelele za kuomba msaada ndipo wananchi walifika na kuanza kumshambulia mganga huyo na kusababishia kifo chake.