SAUDI ARABIA-UAE,
MFALME wa Saudi Arabia, Salman amemwambia Rais wa Marekani, Donald Trump katika mazungumzo ya simu jana, taifa hilo la kifalme lina nia ya kufikiwa suluhisho la haki na la kudumu kuhusu mzozo wa Palestina.
Mfalme Salman alisema hilo, ni sehemu kuu ya kuanzia ya juhudi za pendekezo la amani la mataifa za kiarabu.
Viongozi hao walizungumza kwa simu kutokana na makubaliano ya kihistoria yaliyosimamiwa na Marekani mwezi uliopita ambayo Umoja wa Falme za Kiarabu ulikubali kuwa taifa la tatu la kiarabu kurejesha uhusiano wa kawaida na Israel baada ya Misri na Jordan.
Mfalme Salman alimwambia Rais Trump anakubaliana na juhudi za nchi yake kuunga mkono amani na Saudi Arabia inataka kuona suluhisho la kudumu na la haki katika suala hili la Palestina chini ya juhudi za amani za mataifa ya kiarabu zilizopendekezwa na taifa hilo mwaka 2002.
Chini ya pendekezo hilo, mataifa ya kiarabu yamependekeza kwa Israel kurejesha uhusiano wa kawaida ili kufikiwa makubaliano ya kupatiwa Wapalestina taifa lao na Israel kujitoa kabisa kutoka katika ardhi za mataifa ya kiarabu ilizoziteka katika vita vya mwaka 1967 vya mashariki ya kati.
Saudi Arabia, mahali palipozaliwa uislamu na maeneo matakatifu, haiitambui Israel.
Hata hivyo, mwezi huu taifa hilo limesema litaruhusu safari za ndege kati ya Umoja wa Falme za Kiarbu na Israel, ikiwa ni pamoja na shirika hilo la ndege la Israel kutumia anga yake.
Mshauri wa Ikulu ya Marekani, Jared Kushner alisema ana matumaini mataifa mengine ya kiarabu yatarejesha uhusiano wa kawaida na Israel katika muda wa miezi michache.
Hakuna taifa lingine la kiarabu lililosema hadi sasa linatafakari kufuata mfano wa Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mtoto mfalme Salman, mwana mfalme mteule Mohammed bin Salman na Kushner walijadili haja ya Wapalestina na Waisrael kurejea majadiliano na kufikia makubaliano ya kudumu ya amani baada ya Kushner kuzuru Umoja wa Falme za Kiarabu mwezi uliopita.
Makubaliano kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Israel yalipingwa kwa kiasi kikubwa na palestina.