24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Jinsi ajira milioni nane zitakavyozalishwa na JPM

Na NORA DAMIAN

TAFITI mbalimbali za ukosefu wa ajira zinaonyesha ukubwa wa changamoto hiyo hasa kwa vijana ambao ndiyo nguvu kazi inayotegemewa katika mataifa mengi.

Ripoti ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kuhusu mwenendo wa soko la ajira kwa mwaka 2020 inaonyesha zaidi ya watu milioni 470 hawana ajira.

Aidha, utafiti wa nguvu kazi Tanzania ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano, kwa mwaka 2014 ulionyesha ukosefu wa ajira ulikuwa asilimia 10.3 lakini mwaka 2018 ulishuka hadi asilimia 9.7 huku malengo ya Serikali yakiwa ni kupigania ushuke zaidi.

Kulingana na utafiti huo kiwango cha nguvu kazi chenye ujuzi wa chini ni asilimia 7.9 na malengo ya Serikali ni kuhakikisha hakizidi asilimia 54 ambacho ni kiwango cha kimataifa.

Pia kiwango cha juu cha ujuzi wa kati ni kati ya asilimia 16 na malengo ni kukipandisha hadi kufikia asilimia 34 huku kiwango cha juu ambacho ni asilimia 3.6 malengo yakiwa ni kukipandisha hadi asilimia 12.

Tanzania ikiwa ni sehemu ya dunia inalazimika kuweka mikakati kupambana na changamoto ya ukosefu wa ajira ili kuondoa umaskini na kuimarisha maisha ya wananchi wake na kukuza uchumi kwa ujumla.

Ndiyo maana suala hilo limekuwa ni miongoni mwa vipaumbele sita katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2020 ambayo wagombea wa nafasi mbalimbali wakiongozwa na Dk. John Magufuli, wanaendelea kuinadi kwa wananchi.

CCM kinatambua kuwa uwapo wa fursa za ajira ni muhimu katika kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambapo jamii hususan vijana hupewa nafasi ya kuchangia utaalam walionao katika kufanya kazi ili kuchangia katika kukuza maendeleo ya taifa lao.

Dk. Magufuli anasema atatengeneza ajira milioni nane katika kipindi cha miaka mitano ijayo katika sekta rasmi na 

isiyo rasmi kwa ajili ya vijana ambazo zitapunguza tatizo la ajira na umaskini.

Anasema licha ya kwamba wako baadhi ya watu wasioamini kama hilo linatekelezeka lakini anawaomba Watanzania wamuamini kwani uwezo anao.

“Naomba Watanzania mtuamini uwezo wa kuyatekeleza tunao kama ambavyo tumeweza kuyatekeleza yale mengine kwa kipindi cha miaka mitano,” anasema Dk. Magufuli.

AJIRA ZILOZOZALISHWA 2015 – 2020

Dk. Magufuli anasema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita wamefanikiwa kuzalisha fursa za ajira 6,032,299 katika sekta rasmi na isiyo rasmi.

Katika kuongeza fursa hizo mkakati uliwekwa kulinda ajira za Watanzania na kuhakikisha kuwa ajira wanazopewa wageni ni zile tu ambazo Watanzania hawana ujuzi nazo na kuzingatia kuwa wanafundishwa ujuzi ambao hawana ili kuzimudu kazi hizo.

Kati ya fursa hizo, ajira 1,975,723 zimezalishwa katika sekta rasmi ya umma na binafsi ikiwamo miradi ya maendeleo ya Serikali ambayo imezalisha ajira 1,074,958.

Miradi ya maendeleo ya Serikali ya kimkakati imezalisha ajira 163,729 wakati ajira 4,056,576 zilizalishwa katika sekta isiyo rasmi.

Mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) hadi mwaka huu ulikuwa umetoa ajira 14,139 ambapo 11,756 ni kwa Watanzania.

Aidha, mradi wa Ubungo Interchange hadi mwaka jana ulikuwa umetoa ajira 502 ambapo ajira 449 zilikuwa za Watanzania.

Pia upanuzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa kujenga jengo la tatu la abiria hadi mwaka jana ulikuwa umetoa ajira 1,056 ambapo Watanzania walikuwa 997.

Vilevile mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere hadi mwaka huu ulikuwa umetoa ajira 3,412 ambapo Watanzania ni 2,783.

Katika kipindi hicho, pia mikopo ya masharti nafuu yenye thamani ya Sh bilioni 17.9 imetolewa kwa vikundi vya vijana 535 vyenye wanachama 3,745 ili kuwawezesha kupata mitaji ya kuanzisha biashara.

Aidha, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaochangiwa asilimia nne ya mapato ya ndani ya mamlaka za serikali za mitaa umetoa Sh bilioni 14.7 kwa vikundi vya vijana 2,026 vyenye wanachama 20,260.

Aidha, katika kipindi hicho mafanikio mengine yaliyopatikana ni kupitia mpango wa kukuza ujuzi katika sekta muhimu za kipaumbele ikiwamo kilimo, ujenzi, ukarimu, teknolojia ya habari na utalii kwa kuendelea kutoa mafunzo.

Mathalani kupitia programu ya kukuza ujuzi katika maeneo ya kazi kwa njia ya uanagenzi washiriki 28,941 wamepatiwa mafunzo.

Mafunzo mengine ni yale ya uzoefu kazini kwa wahitimu 5,975 wa vyuo mbalimbali ambapo kati yao 1,827 wamepatiwa mafunzo hayo.

Pia mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo yametolewa kwa vijana 14,432.

Mafunzo ya kilimo cha kisasa cha kutumia teknolojia ya vitalu nyumba yametolewa kwa vijana 8,980 katika halmashauri 84 za mikoa 12 nchini.

Aidha, vijana 14,890 walio katika sekta isiyo rasmi wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali kwa kurasimisha biashara.

Mafanikio mengine ni kwa wakulima na wafanyabiashara 9,300 ambao wamepatiwa mafunzo ya uongezaji thamani mazao ya mifugo, kilimo, biashara na masoko.

Vilevile vijana 13,500 wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali pamoja na namna ya uanzishwaji na uimarishaji wa makampuni ikilinganishwa na vijana 5,250 wa mwaka 2015.

MAMBO YATAKAYOZINGATIWA

Kulingana na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, mambo yatakayozingatiwa katika kutekeleza kipaumbele cha ajira ni kuhakikisha miradi mikubwa ya kimkakati inaajiri vijana wengi zaidi wa Kitanzania.

Aidha, kuchochea ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya viwanda vinavyotumia malighafi za kilimo, mifugo, uvuvi, madini, maliasili na sekta ya huduma za kiuchumi pamoja na utalii.

Mambo mengine yatakayozingatiwa ni kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za ujasiriamali ikiwamo kuwapatia mafunzo na kuwaunganisha na taasisi na asasi za utoaji mikopo yenye riba na masharti nafuu.

Pia kuwahamasisha na kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika utamaduni, michezo na sanaa kwa ajili ya afya bora na burudani na kuongeza fursa za ajira na kipato.

MIKAKATI MINGINE

Ili kuongeza fursa za ajira katika sekta rasmi na isiyo rasmi, hatua mbalimbali zinatarajiwa kuchukuliwa zikiwamo kuimarisha utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini ili shughuli za uchumi na biashara ziongezeke na kuzalisha ajira.

Mkakati mwingine ni kuhamasisha na kusimamia halmashauri zote nchini kuendelea kutenga, kurasimisha na kupima na kuweka miundombinu kwenye maeneo maalumu kwa ajili ya uwekezaji na kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili waweze kujishughulisha na uzalishaji mali na biashara.

Aidha, utawekwa mkakati wa makusudi wa kuwawezesha vijana wabunifu na makundi mbalimbali ya vijana na wanawake kuanzisha shughuli za uzalishaji mali na ujasiriamali ili waweze kujiajiri na kuajiri wengine.

Pia kuimarisha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kati ili kuhakikisha vijana wanaohitimu wanapata maarifa na ujuzi wa kazi utakaowawezesha kujiajiri na kuajirika.

Hatua nyingine ni kuimarisha mifumo na kuongeza kasi ya kurasimisha ujuzi ili nguvu kazi ya taifa itumike ipasavyo katika soko la ajira la ndani na nje.

Pia kuimarisha mifumo ya taarifa za soko la ajira na mitaji ili kuwezesha vijana kutumia fursa hizo, kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi na stadi mbalimbali za kazi kwa nguvu kazi ya taifa katika sekta za kipaumbele.

Mkakati mwingine ni kuwawezesha vijana wanaohitimu elimu ya juu na vyuo vya ufundi kuunda kampuni kwa lengo la kuwapatia mitaji na nyenzo kupitia taasisi za fedha na mifuko mingine ya uwezeshaji.

VIPAUMBELE VINGINE

Vipaumbele vingine katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 ni pamoja na kulinda na kuimarisha misingi ya utu, usawa haki na uongozi bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa taifa, kukuza uchumi wa kisasa, fungamishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi.

Pia kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi, kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji, umeme na makazi vijijini na mijini.

Vingine ni kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles