NA MWANDISHI WETU, Dar es Salaam
MEYA wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko (Chadema) ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kudai kuwa ndicho chama anachokipenda kwa dhati .
Kuyeko ambaye pia ni diwani wa Kata ya Bonyokwa alitangaza uamuzi huo jana ambapo pamoja na kuwashukuru viongozi wa Chadema alisema kuwa ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuvutiwa na kazi zinazofanywa na Rais Dk.John Magufuli huku akiwashukuru .
“Kwa kipindi hiki kwa kweli niendelee kumshukuru Rais Dk.Magufuli kwa sababu anafanya kazi ya ajabu iliyotukuka, tuendelee kumsapoti, nirudie tena kuwashukuru chama changu cha sasa Chadema ambao walinipa nafasi ya kugombea kupitia kwao.
“Na mimi sikuwadharau niliendelea kuwaheshimu na nitaendelea kuwaheshimu kwa heshima waliyonipa lakini mimi kwa kweli mapenzi yangu ya dhati yapo CCM kwa sababu nimekulia humo, nimeishi humo,”alisema Kuyeko.
Alisema siku zote alikuwa akitamani Tanzania ipate rais mkali lakini hakujua atakuja nani lakini bahati nzuri alitokea Rais Magufuli ambaye alikuwa akizikubali kazi zake.
“Nilikuwa na kubali kazi yake sana akiwa waziri wa ujenzi na uchukuzi alijenga barabara nyingi na alifanya mambo mengi makubwa kila wizara aliyokwenda.
“ Rais Magufuli kwa kweli ni mtu wa kuigwa ni mtu ambaye Mungu amempa kalama na vipawa mbalimbali vyakufanya kazi ni lazima tukubali kama nilivyotangulia,”alisema Kuyeko.
Alisema pamoja na kwamba alikuwa chama cha upinzani ambacho anawaheshimu viongozi wake kwakumpa nafasi lakini hakuwahi kusema kama serikali iliyopo madarakani mbaya.