NA SHABANI MATUTU, DAR ES SARAAM
MEYA wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob, amemlaumu Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, akisema amekuwa na utamaduni wa kuingilia majukumu ya Baraza la Madiwani kinyume cha utaratibu wa utendaji.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Meya Jacob, alisema pamoja na kumvumilia kwa muda mrefu mkuu huyo wa wilaya huingilia shughuli za utendaji bila ya kujali athari zinazoweza kujitokeza.
“Tumekuwa tukivumilia tabia ya Makonda kuingilia masuala ya utendaji ya Baraza la Madiwani.
“Lakini kitendo alichofanya jana (juzi) cha kuchafua hali ya hewa cha kutangaza maazimio ya Kikao cha Kamati ya Fedha cha kupitisha mpango wa kupokea msaada wa Dola za Marekani milioni 300 kutoka Benki ya Dunia (WB) kazi ambayo haikuwa yake, imemfedhehesha sana,” alisema Jacob.
Alisema Makonda ametoa siri hiyo kwa waandishi wa habari wakati akijua wasemaji wa masuala ya Halmashauri ni Meya, Mkurugenzi na Msemaji wa Manispaa huku mambo yanayojadiliwa huwa siri na hairuhusiwi kwa mjumbe yeyote kuyaweka wazi.
“Mambo yote yanayojadiliwa katika kikao hicho ni siri na hairuhusiwi yeyote kusema hadi yatakapofika kwenye Baraza la Madiwani.
“Hivyo uamuzi wa Makonda kutangaza hadharani kwamba wilaya yake ya Kinondoni imepata fedha hizo inasababisha hasira miongoni mwa wajumbe wa kamati ya fedha.
“Makonda alipata taarifa kutoka kwa makatibu tarafa ambao ndiyo wajumbe wanaoingia kwenye kikao hicho jambo ambalo si baya.
“Lakini kosa lake ni kutoka na kutangaza hali inayotafsiriwa kama kujitengenezea nafasi ya kubaki katika nafasi yake Rais Magufuli atakapotangaza wakuu wake wa wilaya,” alisema.
Meya alisema hofu ya tamko hilo la Makonda linaweza kusababisha wajumbe wa Kamati ya Fedha na Baraza la Madiwani kuamua kwa hasira kubadilisha matumizi ya fedha kwa mamlaka waliyonayo kumkomoa mkuu huyo wa wilaya.
“Hivi baraza likifanya mabadiliko Makonda si ataaibika, na je, ataonekanaje kwa jamii na hata Rais aliyemsifia kuwa mchapakazi akagundua kwamba hakuna analolijua zaidi ya kukurupuka. Je, atampa heshima kama aliyokuwa amempa mwanzo?” alihoji Meya huyo.
Alisema athari nyingine inayoonekana ni kuwasababishia hali ya taharuki wananchi wanaoishi eneo la Mto Ng’ombe kwa taarifa yake isiyokuwa ya kweli kwamba wanatarajiwa kubomoa nyumba zao kupisha ujenzi wa mto huo.
Alitaja baadhi ya mambo ambayo Makonda amekuwa akiingilia kuwa ni kutangaza ujenzi wa machinjio ya kisasa itakayofanywa na halmashauri wakati akijua uamuzi huo upo chini ya Meya na Mkurugenzi.
Jingine ni suala la kuwaita wenyeviti na kuwataka kuvunja maeneo ya wazi wakati akijua hana mamlaka hiyo na kujenga shule wakati kazi hiyo anajua si yake.
MTANZANIA ilipomtafu DC Makonda kupata ufafanuzi wake, alijibu kwa kifupi kwamba: “Tatizo linalomsumbua Meya Jacob ni ugeni wake katika kazi hivyo bado anajifunza ila akishaelewa mipaka yake na Mkuu wa Wilaya hatapata shida,”.