27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

Elimu bure bado kitendawili Dar

magufuli1TUNU NASSOR NA ESTHER MNYIKA, DAR ES SALAAM

PAMOJA na serikali ya awamu ya tano kutangaza sera ya elimu bure, Manispaa ya Kinondoni inakabiliwa na changamoto katika kutekeleza sera hiyo, MTANZANIA limebaini.

Uchunguzi uliofanywa kwa wiki kadhaa katika baadhi ya shule za msingi na sekondari kwa nyakati tofauti, umebaini changamoto  mbalimbali ikiwamo wanafunzi kukaa chini, uhaba wa walimu wa sayansi, vitabu, vifaa, baadhi ya masomo kufutwa na kupunguza baadhi ya mitihani.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti, baadhi ya walimu   walisema mfumo huo umeongeza changamoto katika elimu kutokana na fedha hizo kutolewa kila mwezi lakini shule zinashindwa kuzipangia bajeti.

Mwalimu wa Idara ya Fedha wa Shule ya Sekondari Mama Salma Kikwete, Salumu Ummy   alisema fedha za  elimu bure awamu ya pili zilitolewa Februari 2 mwaka huu ambazo ni  Sh 4,475,000 lakini mchanganuo wa fedha hizo bado haujatolewa.

“Kwa awamu  zote mbili  fedha zimetolewa kwa kiasi tofauti, Januari ilikuwa Sh 4,483,000 na Februari  Sh. 4,475,000.

“Fedha zimetolewa kwa kiasi tofauti awamu ya kwanza tulipokea Sh   4,483,000 na mgawanyo wake ulikuwa Sh  2,294,000   fidia ya ada na Sh    2,189,000 ni kwa ajili ya ruzuku,”alisema Ummy.

Ummy  alisema  mchanganuo wa fedha zilizotolewa Januari ulikuwa  asilimia 35 kwa ajili ya uendeshaji wa ofisi , asilimia 30  taaluma , asilimia 10 dawa za binadamu, asilimia 10  matengenezo na asilimia 15 mitihani .

Hata hivyo, alisema mchanganuo huo kwa shule za sekondari bado haukidhi mahitaji kwa shule ambayo ina wanafunzi  1,265.

Ummy alisema fedha hizo hutolewa na mchanganuo ambao baadhi ya mahitaji huwa hayamo hivyo kushindwa kuyaingiza katika bajeti hiyo.

“Katika mchanganuo huo hakuna fedha za kulipia bili za umeme, maji na huduma ya mlinzi ambako awali wazazi walichangia huduma hizo,” alisema Ummy na kuongeza:

“Changamoto nyingine ni  upungufu wa walimu wa sayansi, kwa mfano, kwa sasa tuna mwalimu mmoja wa somo la Hesabu, Kemia wawili, Fizikia mmoja na Baiolojia watatu kwa shule nzima, hivyo vipindi vingi vya masomo hayo havifundishwi”.

Ili kukabiliana na hali hiyo kabla ya kuanzishwa mpango wa elimu bure, alisema walitumia fedha za ada kukodi walimu wa masomo hayo ili kukidhi mahitaji hayo lakini kwa sasa katika mchanganuo wa fedha zinazopelekwa na serikali  hakuna fedha zilizopangwa kwa ajili ya kutafuta walimu hao wa ziada.

Serikali pia iliahidi kununua vitabu vya kufundishia na kujifunzia lakini hadi sasa havijapelekwa shuleni hivyo kuzidisha ugumu katika ufundishaji, alisema.

“Kuna uhaba wa samani za shule yakiwamo madawati na kusababisha wanafunzi wengi wa kidato cha kwanza kukaa chini na kuwafanya  washindwe kuandika na kujifunza vizuri,” alisema Ummy.

Naye Makamu Mkuu wa Shule wa shule hiyo, Lucy Burreta, alisema shule imeamua kufuta masomo ya mchepuo wa biashara kutokana na kukosa walimu wake.

Alisema katika mchanganuo unaotolewa, fedha kwa ajili ya taaluma ni ndogo na zikigawiwa kwa mwezi kuna baadhi ya vifaa kama chaki, wino, karatasi za mitihani hazifiki mwisho wa mwezi.

Wanafunzi ni wengi kiasi ambacho darasa moja linakuwa na zaidi ya 64 hivyo kumpa wakati mgumu mwalimu anayefundisha, alisema.

Lucy alisema nguvu nyingi za mfumo wa elimu bure zimepelekwa katika shule za msingi na kusahau za sekondari.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Manzese,   Linus Mwakasege alisema  serikali ilisimamisha shule kununua vitabu tangu mwaka juzi, lakini tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo vitabu vimekwisha kutolewa mara moja tu.

“Kuna ongezeko kubwa la wanafunzi kwa kuwa wale walioshindwa kuripoti miaka iliyopita  kwa sababu ya kukosa ada wanaomba kuendelea na masomo jambo ambalo linazidi kuongeza idadi,” alisema Mwakasege.

MTANZANIA ilimtafuta Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowera   kulizungumzia suala hilo.

Alikiri kuwapo kwa changamoto katika suala la elimu akisema  zimetokana na sera hiyo kuanzishwa katikati ya mwaka wa fedha hivyo hakukuwa na fedha zilizokuwa zimetengwa katika bajeti.

“Si kwamba changamoto hizo zote zimeletwa na sera ya elimu bure, zilikuwapo tangu michango na ada kwa wanafunzi ilipokuwapo…bado hakukuwa na madarasa ya kutosha, madawati na vitabu,” alisema Mhowera.

Mhowera ambaye alizungumza kwa niaba ya olfisa elimu manispaa hiyo, alisema ili  kupunguza adha hiyo, manispaa imepunguza baadhi ya matumizi katika bajeti yake ili kupata fedha kwa ajili ya kusaidia elimu.

“Kisheria mabadiliko ya bajeti yanatakiwa yaidhinishwe na Baraza la Madiwani wa Manispaa yetu.  Tulichelewa kuanza kutokana na sababu za  siasa  hivyo kushindwa kuidhinisha fedha tulizopunguza katika bajeti ya Sh bilioni 1.5 zitakazosaidia kwa miezi minne katika shule,” alisema Mhowera.

Kuhusu upungufu wa walimu wa sayansi, ofisa huyo alisema liko mikononi mwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambaye ameishauri manispaa kuomba kibali cha kuajiri walimu wa ziada wanaohitajika.

Kuhusu miundombinu ya shule, alisema manispaa ina upungufu wa vyumba vya madarasa 1601 kwa shule za msingi na 466 sekondari ambavyo vinahitajika kabla ya Julai.

“Tuna upungufu wa madawati 18,816, matundu ya vyoo 6,805 na maabara sita,” alisema Mhowera.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles