30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Meya Bukoba amrushia kombora Kagasheki

Balozi Khamis Kagasheki
Balozi Khamis Kagasheki

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM

MEYA wa Manispaa ya Bukoba, Chief Kalumuna, amesema kukwama kwa mradi wa viwanja uliokuwa unaendeshwa na Taasisi ya Miradi na Maendeleo ya Miundombinu (UTT-PID), kulichangiwa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Balozi Khamis Kagasheki.

Amesema hatua hiyo imeifanya manispaa hiyo kupita katika kipindi kigumu ikiwamo kubadilishiwa wakurugenzi tisa wa halmashauri jambo ambalo liliwafanya washindwe kufikia malengo.

Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam katika mkutano wa wadau na mipango miji ulioandaliwa na UTT-PID.

Kalumuna alisema kuwa pamoja na kupimwa kwa viwanja 5,000 vya awamu ya kwanza, walijikuta wakiingia katika malumbano yaliyohatarisha kuvunjwa kwa halmashauri hiyo.

“Mgogoro pale Bukoba ulianzia kwenye viwanja na suala kubwa lilikuwa ni vita ya ubunge, Balozi Kagasheki alimua kutumia nafasi yake kutugawa madiwani na kikubwa alikuwa akihisi kama mradi wa viwanja ungefanikiwa basi yeye angemalizika kisiasa.

“Na wote tunajua, tena alikuwa waziri na si hilo, pia alikuwa akisaidia na aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI, Hawa Ghasia. Sasa tunashukuru Mungu tumetoka huko na madiwani wote tunaimba wimbo mmoja wa maendeleo,” alisema Kalumuna.

Meya huyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kahororo kwa tiketi ya Chadema, alisema kuwa mradi wa viwanja umewaingiza UTT katika malumbano wasiyohusika ikiwamo kushambuliwa bila sababu jambo ambalo halikuwa sahihi.

“Tena tunashukuru UTT-PID wao ndiyo walioleta fedha kwetu zaidi ya shilingi bilioni 2 na sisi kama halmashauri tulitoa shilingi milioni 700 tu na kama fedha zile zingekuwa chini ya mikono ya halmashauri vita yake ingekuwa kubwa, ila tunashukuru Benki ya Posta Tanzania waliziweka vizuri na kwenye mikono salama,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mipango Miji na Ardhi ambaye pia ni Meneja wa mradi wa viwanja 5,000, Catres Rwegasira, alisema kuibuka kwa mgogoro huo uliochangiwa na wanasiasa, kulisababisha baadhi ya watu waliopewa viwanja kushindwa kufanya malipo kwa hofu ya kupoteza fedha zao.

“Tunashukuru tumevuka salama na sasa tupo katika matumaini makubwa, na sasa mradi wa viwanja unatekelezwa na tunaamini tutapima pia vingine. Ila kila mmoja wetu anajua wapi tulipotoka hasa Manispaa ya Bukoba na sasa tunasonga mbele,” alisema Rwegasira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles